Yajue Mambo 5 Muhimu Kuhusu Msongo Wa Mawazo (Sonona).

Maana Ya Msongo Wa Mawazo (Sonona):

Msongo wa mawazo ni mfadhaiko wa akili anaoupata mtu kutokana na shida, taabu, dhiki, matatizo au changamoto zinazomkabili katika maisha ya kila siku. 

Msongo wa mawazo hujulikana kwa kitaalamu kama Depression.

Kwa kawaida mtu hupata msongo wa mawazo pale anaposhindwa au kukosa namna ya kukabiliana na jambo linalomsumbua.

Visababishi Vya Msongo Wa Mawazo:

Kuna sababu nyingi zinazosababisha mtu kupata msongo wa mawazo, baadhi ya sababu hizo ambazo zimegawanyika katika makundi mawili ambayo ni kibiologia na kisaikolojia.

1) Sababu Za Kibiologia.

Sababu za kibiologia zinazosababisha mtu kupata msongo wa mawazo ni pamoja na;

a) Mtu kurithi vinasaba kutoka kwa mzazi/ wazazi.

b) Magonjwa ya muda mrefu kama vile UKIMWI, figo, ini, moyo nk. 

2) Sababu Za Kisaikolojia.

Sababu za kisaikolojia zinazosababisha mtu kupata msongo wa mawazo ni pamoja na;

a) Matukio yasiyofurahisha kama vile ubakaji, uvamizi, ajali au kufiwa, au kutekwa nyara. 

b) Majanga kama vile kimbunga, mafuriko, tetemeko la ardhi n.k

c) Changamoto za kila siku za maisha kama vile ugoni, talaka, mimba kuharibika, kutoa mimba, kutengana, kufungwa, kuuguza au kukosa kazi.

d) Matatizo sehemu za kazi kufukuzwa kazi / chuo, migogoro kazini au kustaafu kazi.

e) Mambo ambayo yanategemewa mtu kufurahi yanaweza kumsababishia msongo wa mawazo kama vile kuoa au Kuolewa, kuzaliwa mtoto, kufaulu mtihani, ajira mpya, kuhamia nyumba mpya, kupata ujauzito n.k

Dalili Za Msongo Wa Mawazo:

Zifuatazo ni dalili za msongo wa mawazo ambazo ni pamoja na;

a) Maumivu ya sehemu mbalimbali za mwili hasa kichwa na kifua.

b) Kuwa na huzuni na kujisikia mnyonge.

c) Kusahau na kukosa uwezo wa kufikiri vyema.

d) Kujihisi kuchoka na kukosa ari (mood) ya kufanya kazi.

e) Kuwa na hofu na kutokujiamini.

 f) Kushindwa kufanya maamuzi sahihi.

g) Kushindwa kula au kula sana.

h) Kukosa hamu ya tendo la ndoa.

 i) Kupungua uzito au kuongezeka uzito.

 j) Kubadilika kwa siku za hedhi au kutokuona kabisa.

k) Kulala muda mfupi na muda mwingi kuwa macho usiku.

 l) Kukosa choo kwa muda mrefu.

m) Kutaka kujiua au kuwa na mawazo ya kujiua.

msongo wa mawazo

Madhara Ya Msongo Wa Mawazo Kiafya:

Athari za msongo wa mawazo zinaweza kuwa za kihisia au kitabia.

1) Athari Za Kihisia.

Zifuatazo ni athari za kihisia za msongo wa mawazo ambazo ni pamoja na;

a) Kuwa na hofu kupita kiasi.

b) Kuwa na mfadhaiko.

c) Kuwa na hisia za kukosa ulinzi.

d) Kusahau na kushindwa kufikiria ipasavyo.

e) Kukosa utulivu na kuwa na huzuni.

2) Athari Kitabia.

Zifuatazo ni athari za kitabia za msongo wa mawazo ambazo ni pamoja na;

a) Kula sana/-kushindwa kula.

b) Kubagua aina za vyakula.

c) Kuwa na hasira.

d) Kunywa pombe kupita kiasi.

e) Kutumia madawa ya kulevya.

 f) Kupenda kuwa mwenyewe na kujitenga na jamii.

g) Kuwa na huzuni na kulia.

h) Kutoelewana na jamii.

Jinsi Ya Kupunguza Msongo Wa Mawazo:

Zifuatazo ni njia za kupunguza msongo wa mawazo ambazo ni pamoja na;

a) Tafuta chanzo cha msongo na epuka nalo au kubaliana nalo.

b) Kuwa na mtizamo chanya kwamba hiyo changamoto inayokukabili kwani huo sio mwisho wa maisha.

c) Fanya mazoezi ili kupunguza mzigo wa hisia unaokuelemea na huondoa msongo wa mawazo.

d) Epuka kuwa peke yako, washirikishe watu wa karibu matatizo yako kwa kuomba ushauri.

e) Pata muda wa kutosha wa kupumzika ikiwa ni pamoja na kulala

f) Epuka mazoea mabaya kama kunywa pombe au kutumia dawa kwa imani kwamba zitakupunguzia msongo wa mawazo.

g) Jitahidi Kula vizuri kwani mwili unategemea chakula ili uweze kufanya kazi vizuri.

h) Fanya vitu ambavyo vitakupa starehe kama vile kusoma vitabu, kusikiliza mziki, kwenda sehemu za burudani, na kuwa na mtu wa kukufariji.

i) Badilisha mazingira kwa kutembelea sehemu mbalimbali kama vile fukwe za bahari, mbuga za wanyama, bustani n.k

j) Pata ushauri wa wataalam (daktari, mwanasaikolojia n.k)

k) Kutumia dawa kwa usahihi kila wakati.

l) Kuhudhuria kiliniki kila wakati kama ulivyopangiwa na wataalam wa afya.

Soma pia hii makala: Yajue Magonjwa Ya Akili, Dalili Zake Na Jinsi Ya Kutibu.

HITIMISHO:

Kwa msaada wa ushauri na tiba ya magonjwa ya afya ya akili tembelea kituo cha afya/hospitali iliyo karibu nawe.