Yajue Mambo 7 Muhimu Kuhusu Ugonjwa Wa Kiharusi.

Maana Ya Kiharusi:

Kiharusi ni ugonjwa wa dharura na hatari ambao hutokea pale seli za ubongo zinapokufa kwa kukosa hewa ya oksijeni na chakula kutokana na kuziba au kupasuka kwa mishipa ya damu kwenye ubongo.

Ugonjwa wa kiharusi (stroke) pia hujulikana kwa kitaalamu kama cerebrovascular accident (CVA).

Kwa mwaka 2015 kulingana na ripoti maalumu ya Shirika la Afya duniani WHO kuhusu sababu za vifo ilionesha kiharusi kinashika nafasi ya pili kati ya magonjwa yote kwa kusababisha vifo vingi.

Kiharusi kinashika nafasi ya tatu kati ya visabibishi vya ulemavu duniani. Waathirika wengi huishia kuwa walemavu.

kiharusi

Aina Za Kiharusi:

Kuna aina kuu mbili za Kiharusi ambazo ni pamoja na:

1) Kiharusi kinachotokana na kuziba kwa mishipa ya damu ya damu ya ubongo.

Aina hii ya kiharusi hujulikana kwa kitaalamu kama ischemic stroke.

ischemic stroke

2) Kiharusi kinachotokana na kupasuka kwa mishipa ya damu ya ubongo.

Aina hii ya kiharusi hujulikana kwa kitaalamu kama hemorrhagic stroke.

hemorrhagic stroke

Kumbuka:

Sababu Za Kiharusi:

Yafuatayo ni mambo yanayomuweka mtu katika hatari ya kupata ugonjwa wa kiharusi ikiwemo:

1) Kisukari.

Wagonjwa wa kisukari wana hatari kubwa ya kupata kiharusi kutokana na athari za ugonjwa huu kwenye mishipa ya damu.

kisukari

2) Shinikizo La Juu La Damu.

Hii ni sababu kuu inayochangia kiharusi, hususan aina ya kiharusi ijulikanayo kama hemorrhagic stroke. Shinikizo la juu la damu (Hypertension) linaweza kuharibu mishipa ya damu na kuongeza hatari ya kutokwa na damu kwenye ubongo.

hypertension

3) Umri Na Jinsia.

Hatari ya kiharusi huongezeka kadri umri unavyoongezeka, na wanaume wako katika hatari kubwa zaidi ya kupata kiharusi kuliko wanawake.

kiharusi

4) Uvutaji Wa Sigara.

Uvutaji wa sigara unachangia sana kuongezeka kwa hatari ya kiharusi kwa sababu unaharibu mishipa ya damu na kuongeza shinikizo la damu.

uvutaji wa sigara

5) Historia Ya Kiharusi Katika Familia.

Ikiwa kuna historia ya kiharusi katika familia, hatari ya kupata kiharusi inaweza kuongezeka.

6) Kutofanya Mazoezi.

Kukosa mazoezi kunaweza kuongeza hatari ya kupata shinikizo la juu la damu (Hypertension) na magonjwa mengine ya moyo ambayo pia huongeza hatari ya kupata ugonjwa wa kiharusi.

7) Unene Kupita Kiasi.

Unene kupita kiasi (obesity) huongeza hatari ya mtu kupata shinikizo la juu la damu, kisukari, na matatizo mengine ya afya ambayo pia yanaweza kuongeza hatari ya kiharusi.

unene kupita kiasi

8) Matumizi Ya Pombe Kupita Kiasi.

Kunywa pombe kupita kiasi kunaweza kuongeza shinikizo la damu na hivyo kuongeza hatari ya kiharusi.

pombe

9) Magonjwa Ya Moyo.

Magonjwa ya moyo kama vile ugonjwa wa mtetemo wa moyo (atrial fibrillation) yanaweza kusababisha damu kuganda kwenye mishipa ya damu inayoelekea kwenye ubongo, hali inayoweza kuongeza hatari ya kupata kiharusi.

10) Tatizo La Mafuta Mengi Kwenye Damu.

Kiwango cha juu cha cholesteroli kwenye damu (Hypercholesterolemia) kinaweza kuchangia kuziba kwa mishipa ya damu na kusababisha kiharusi.

hypercholesterolemia

Dalili Za Kiharusi:

Dalili za kiharusi ni pamoja na:

1) Ganzi.

Mtu anayepata kiharusi hupata ganzi inayoanza ghafla na mara nyingi huathiri upande mmoja wa mwili. Mfano: Upande mmoja wa uso kufa ganzi na kushindwa kuongea vizuri au kutabasamu.

2) Kupata Shida Kuongea.

Mgonjwa wa kiharusi hushindwa kuongea vizuri, utoaji wa maneno huwa sio wa kawaida. Mfano: Mgonjwa kushindwa kumaliza sentensi au kuongea kama amelewa sana.

Pia hali hii huweza kuambatana na kutoka mate (udenda) kwa wingi mdomoni.

3) Kushindwa Kuona.

Mgonjwa wa kiharusi anaweza kushindwa kuona, hali hii hutokea ghafla. Inaweza kuhusisha jicho moja au macho yote mawili.

4) Pia Mgonjwa Anaweza Kupoteza Fahamu Au Kupata Degedege. 

5) Mgonjwa Anaweza Kushindwa Kuzuia Haja Kubwa Au Ndogo Au Vyote Viwili.

Jinsi Ya Gundua Kiharusi Haraka Ili Uokoe Maisha Ya Mpendwa, Ndugu Au Jamaa:

Kiharusi ni tatizo la dharura linaloweza kusababisha madhara makubwa ikiwemo kifo au ulemavu kama mtu asipopata matibabu mapema. Hivyo ni vyema kila mtu akafahamu dalili za kiharusi ili iwe rahisi kuzitambua. na kuchukua hatua mapema.

Ili kurahisha kumbukumbu za dalili za kiharusi kifupisho FAST (Face Arm Speech Time) hutumika kama ifuatavyo:

1) Face (Uso).

Angalia kama upande mmoja wa uso uko tofauti na mwingine. Mwambie mgonjwa. anyanyue kope au akunje ndita au atabasamu. Upande ulioathrika utashindwa kufanya hivyo.

2) Arm (Mkono).

Mwambie mgonjwa anyanyue mikono juu kwa mbele au juu mara nyingi mkono wa upande ulioathirika hushindwa kunyanyuka au hudondoka unaporudishwa chini.

3) Speech (Uongeaji).

Mwambie mgonjwa atamke jina lake, mtu mwenye kiharusi hushindwa kuongea, au huongea kama mlevi au hupata shida kutafuta maneno kama mtu aliyepoteza kumbukumbu.

4) Time (Muda).

Muda ni mali, chukua maamuzi ya kutafuta msaada wa kitabibu haraka maana kadri unavyochelewa ndio kiharusi kinaharibu sehemu muhimu za ubongo.

fast

Matibabu Ya Kiharusi:

Matibabu ya kiharusi hutegemea pia aina na visababishi vyake ambayo hujumuisha:

A) Matibabu Ya Kiharusi Kinachotokana Na Kuziba Kwa Mishipa Ya Damu Ya Damu Ya Ubongo (Ischemic Stroke).

Mgonjwa hutibiwa kwa kutumia dawa za kuyeyusha damu iliyoganda (thrombolytics) au kwa kuondoa damu iliyoganda kwa njia mbalimbali (thrombectomy). Dawa nyingine kama vile junior Aspirin na Clopidogrel hutolewa kwa ajili ya kuzuia chembe sahani kukusanyika na kuganda.

B) Matibabu Ya Kiharusi Kinachotokana Na Kupasuka Kwa Mishipa Ya Damu Ya Ubongo (Hemorrhagic Stroke).

Aina hii ya kiharusi huitaji tathmini ya upasuaji wa neva ili kuchunguza na kutibu sababu ya damu kuvuja. Angalizo: ni hatari kumpa mgonjwa wa aina hii ya kiharusi dawa za kuyeyusha damu iliyoganda au za kuzuia kuganda maana uhatarisha maisha ya mgonjwa badala ya kumsaidia. Kwahiyo ni vizuri kwa wataalamu kufanya ufanya uchunguzi wa kutosha ili kuwa na uhakika na tatizo.

Kinga Ya Kiharusi:

Mabadiliko ya mienendo ya maisha (lifestyles) kama vile kula vyakula vyenye manufaa kiafya, kufanya mazoezi kila siku, kuacha kuvuta sigara na kupunguza matumizi ya pombe huweza kupunguza uwezekano wa kupata kiharusi cha muda mfupi na kiharusi kwa ujumla.

Udhibiti mzuri wa shinikizo la damu, kiwango cha kolesteroli na kisukari husaidia kuzuia hali hii. Watu wenye magonjwa yanayoongeza uwezekano wa damu kuganda kwenye moyo kama vile hitilafu za mapigo ya moyo wanapaswa kuzingatia kutumia dawa za kufanya damu iwe nyembamba.

HITIMISHO:

Kiharusi cha muda mfupi hakisababishi madhara ya kudumu kwenye ubongo. Hata hivyo hali hii ni ishara ya kuwa kuna hatari kubwa ya kupata kiharusi hivi karibuni. Watu wenye hali hii wanapaswa kumuona daktari na kushauriwa hatua za kuchukua ili kupunguza uwezekano wa kupata kiharusi.