Madhara Ya Mtoto Kuzaliwa Na Uzito Mkubwa.

Kwanini Si Afya Nzuri Kwa Mtoto Kuzaliwa Na Uzito Mkubwa?

Sehemu kubwa watu ya katika jamii zetu za kitanzania wamejijengea dhana kuwa mtoto anayezaliwa na uzito mkubwa (bonge) ndiye mtoto mwenye afya njema na ndugu kumfurahia sana ilihali jambo hilo ni tofauti kabisa kwa wataalamu wa afya.

Utakapoingia wodi ya kujifungulia ambapo mama anayetarajiwa kujifungua inakisiwa/kufahamika kuwa atajifungua mtoto mwenye uzito mkubwa macho na masikio ya wahudumu wa afya muda wote yatakuwa kwake, vile vile jambo hilo litakuwepo kwenye wodi ya watoto wachanga alikolazwa mtoto wa hivyo.

Umakini huu unasababishwa na hofu juu ya yale yanayoweza kutokea wakati wa kujifungua na kuhatarisha afya ya mama na mtoto na afya ya mtoto mara baada ya kuzaliwa na afya yake ajapokuwa mtu mzima.

Ili kuepuka hilo ni vizuri kufahamu jambo hili kwa undani na kuchukua hatua stahiki.

Leo katika mada yetu ya blogu hii tutazungumzia kuhusu madhara ya mtoto kuzaliwa na uzito mkubwa. Ungana nami katika somo hili.

Hali ya mtoto kuzaliwa na uzito mkubwa hujulikana kwa kitaalamu kama macrosomia, lakini mtoto aliyezaliwa na uzito mkubwa anajulikana kwa kitaalamu kama macrosomic baby.

Mtoto anayezaliwa na uzito mkubwa ni yule anayezaliwa na uzito wa kilo 4 au zaidi ya hapo bila kujali umri wa mimba.

Kwa kawaida watoto wa kiume huzaliwa na wastani wa uzito wa  kilo 3.3, wakati wale wa kike huzaliwa na wastani wa kilo 3.2

Sababu Zinazochangia Mtoto Kuzaliwa Na Uzito Mkubwa:

Baadhi ya sababu zinazopelekea mama kujifungua mtoto mwenye uzito mkubwa ni pamoja na:

1) Kisukari Cha Ujauzito.

Wanawake walio na kisukari cha mimba (Gestational Diabetes) wana uwezekano mkubwa wa kuzaa watoto wenye uzito mkubwa. Hii ni kwa sababu kiwango cha juu cha sukari katika damu ya mama kinaweza kwenda kwa mtoto kupitia kondo la nyuma (placenta), na kumfanya mtoto kuzalisha insulini zaidi, ambayo huchangia ukuaji wa haraka.

Kisukari Cha Ujauzito

2) Kisukari Cha Aina Ya 2.

Kama ilivyo kwa kisukari cha mimba, wanawake wenye kisukari cha aina ya 2 (Type 2 Diabetes) pia wana hatari kubwa ya kuzaa watoto wenye uzito mkubwa kutokana na viwango vya juu vya sukari kwenye damu.

Type 2 Diabetes

3) Uzito Wa Mama Kupita Kiasi Kabla Ya Ujauzito. 

Wanawake wenye uzito kupita kiasi kabla ya kupata mimba wana uwezekano mkubwa wa kuzaa watoto wenye uzito mkubwa. Uzito wa ziada wa mama unaweza kuathiri ukuaji wa mtoto kupitia mabadiliko ya homoni na viwango vya sukari.

4) Uzito Wa Mama Kupita Kiasi Wakati Wa Ujauzito.

Ongezeko la uzito wa mama kupita kiasi wakati wa mimba linaweza kuchangia uzito mkubwa wa mtoto wakati wa kuzaliwa.

5) Mimba Iliyopitiliza Umri Wa Kujifungua.

Mimba inayodumu zaidi ya muda wa kawaida (zaidi ya wiki 40) inaweza kusababisha mtoto kuendelea kukua na hivyo kuwa na uzito mkubwa wakati wa kuzaliwa.

6) Umri Wa Mama.

Wanawake wenye umri mkubwa (zaidi ya miaka 35) wana hatari kubwa ya kuzaa watoto wenye uzito mkubwa, ingawa sababu halisi bado hazieleweki kikamilifu.

7) Jinsia Ya Mtoto.

Kwa kawaida, watoto wa kiume huwa na uwezekano mkubwa wa kuzaliwa na uzito mkubwa ikilinganishwa na watoto wa kike.

Kwa maana hiyo, mimba za watoto wa kiume huwa na nafasi (chance) kubwa ya mtoto kuzaliwa na uzito mkubwa kuliko wa kike.

Madhara Ya Kujifungua Mtoto Mwenye Uzito Kubwa:

A) Madhara Kwa Mama.

Yafuatayo ni baadhi ya madhara yanayoweza kujitokeza wakati mama anapojifungua mtoto mwenye uzito mkubwa:

1) Uchungu Na Kujifungua Kwa Muda Mrefu.

Watoto wenye uzito mkubwa wanaweza kusababisha uchungu na kujifungua kuchukua muda mrefu zaidi, hali inayoweza kuhitaji upasuaji wa dharura.

2) Kujifungua Kwa Upasuaji (C-Section).

Uzito mkubwa wa mtoto unaweza kufanya kujifungua kwa njia ya kawaida kuwa ngumu, na hivyo kuongeza uwezekano wa mama kujifungua kwa upasuaji (Caesarean section delivery).

3) Kuchanika Kwa Njia Ya Uzazi.

Kuna hatari ya mama kuchanika njia yake ya uzazi (perineal tear) wakati wa kujifungua kutokana na ukubwa wa mtoto hali inayoweza kupelekea mama kupoteza damu nyingi (Ikumbukwe kuwa upoteaji wa damu nyingi ndio kisababishi namba moja cha kifo kwa akina mama wanaojifungua).

4) Kuongezewa Njia Ya Uzazi (Episiotomy).

Uzito mkubwa wa mtoto unaweza kufanya kujifungua kwa njia ya kawaida kuwa ngumu, na hivyo kuongeza uwezekano wa mama kuongezewa njia yake ya uzazi (episiotomy) ili kusaidia mtoto kutoka hali inayoweza kupelekea mama kupoteza damu nyingi.

5) Kutokwa Na Damu Nyingi.

Kujifungua mtoto mwenye uzito mkubwa kunaweza kuongeza hatari ya kutokwa na damu nyingi baada ya kujifungua hali inayojulikana kwa kitaalamu kama postpartum hemorrhage (PPH).

6) Mfuko Wa Uzazi Kushindwa Kurudi Kwenye Size Yake.

Kujifungua mtoto mwenye uzito mkubwa kunaweza kuongeza hatari ya mfuko wa uzazi (uterus) kushindwa kurudi kwenye size yake kwa wakati mara baada ya kujifungua (uterine atony) na kupelekea upotevu wa damu nyingi.

7) Mfuko Wa Uzazi Kuchanika (Uterine Rupture).

Kama mama alishawahi kujifungua kwa operation hapo awali ni rahisi mfuko wa uzazi kuchanika hali inayojulikana kwa kitaalamu kama uterine rupture kabla ya kufikia muda wa uchungu kwa sababu ya mtoto mkubwa ambayo ni hali ya hatari sana kwa mama.

B) Madhara Kwa Mtoto.

Mbali na madhara anayopata mama wakati wa kujifungua, mtoto anayezaliwa na uzito mkubwa ana uwezekano wa kupata madhara yafuatayo:

1) Majeraha Wakati Wa Kuzaliwa.

Mtoto mwenye uzito mkubwa anaweza kupata ugumu wakati wa kutoka kupitia ya uzazi, ambapo kichwa kinatoka lakini bega la mtoto linakwama kwenye nyonga za mama na hivyo kupelekea kuvunjika kwa mfupa wa bega (clavicle/ collar bone) na kusababisha hali inayojulikana kwa kitaalamu kama Shoulder dystocia.

Shoulder dystocia

2) Kushuka Kiwango Cha Sukari Kwenye Damu (Hypoglycemia).

Watoto wenye uzito mkubwa wanaweza kuwa na hatari kubwa ya kupata kiwango cha chini cha sukari kwenye damu (hypoglycemia) mara tu baada ya kuzaliwa.

Hii inapelekea watoto hao wahitaji kulishwa kwa drip za sukari maana miili yao inahitaji energy nyingi sana lakini kiwango cha maziwa cha mama mara baada ya kujifungua hakitoshi kumlisha mtoto. Ili kumlisha mtoto huyo lazima mishipa itafutwe ili awekewe drip, hivyo unene hukwamisha jambo hili, na hii inaweza kusababisha mtoto kupoteza uhai haraka sana.

3) Kupata Manjano (Jaundice).

Mtoto mwenye uzito mkubwa ni rahisi sana kupata manjano (jaundice), hii inatokana na kuvunjwa kwa seli nyekundu za damu ambazo hazitolewi mwilini kwa kasi inayotakiwa kwani ini bado halijakomaa. Bilirubin ambayo ni matokeo ya kuvunjwa kwa seli nyekundu za damu ikizidi na Kwenda kwenye ubongo huathiri ukuaji wa akili ya mtoto.

4) Hatari Ya Kupata Magonjwa.

Kuzaliwa kwa mtoto mwenye uzito mkubwa kunaweza kuwa na athari kwa afya yake hapo baadaye. Baadhi ya magonjwa na matatizo yanayoweza kuhusishwa na kuzaliwa kwa mtoto mwenye uzito mkubwa ni pamoja na: kisukari, magonjwa ya moyo, presha, shida ya kimetaboliki (metabolic syndrome) nk.

5) Kupata Alama Ndogo Kwenye Dakika 1 Na Ya 5 Baada Ya Kuzaliwa (Apgar Score).

Apgar score ni mfumo unaotumika kupima hali ya mtoto mara tu baada ya kuzaliwa, hasa kwenye dakika 1 na 5 baada ya kuzaliwa. Mfumo huu hupimwa kwa alama za 0 hadi 10, ambapo alama za juu zinaashiria hali nzuri ya mtoto na alama za chini zinaashiria hali mbaya.

Hivyo basi, watoto wengi wanaozaliwa na uzito mkubwa wanapata alama ndogo kwenye dakika 1 na ya 5 baada ya kuzaliwa (Apgar score). Kadiri alama hizi zinavyokuwa ndogo ndivyo mtoto huyu anavyokuwa na ugumu wa kucopy na mazingira mapya ya nje na ukuaji wa akili yake kwa ujumla.

HITIMISHO:

Hivyo ni muhimu sana kwa mwanamke kuhakikisha anachukua hatua zote stahiki za kupunguza uzito kupita kiasi kabla ya ujauzito, kuhakikisha uzito hauongezeki kupita kiasi kipindi cha ujauzito na kutumia dawa stahiki ikiwa ni mgonjwa wa kisukari au amepata kisukari cha ujauzito.

Lakini hata mara baada ya kujifungua ni vizuri kwa mama kuepuka vyakula vitakavyomuongezea uzito sana yeye na mtoto aliyezaliwa na kuhakikisha mtoto huyu anapata muda wa kuushughulisha mwili sawasawa ili kutoishia kwenye matatizo zaidi hapo baadae.