Yajue Magonjwa Ya Akili, Dalili Zake Na Jinsi Ya Kutibu.

Magonjwa Ya Akili:

Magonjwa ya akili ni matatizo ya ubongo ambayo humfanya mtu kuwa na hisia, fikra na matendo tofauti na yale yanayotarajiwa na jamii na kushindwa kukabiliana na changamoto za maisha.

Sababu Za Magonjwa Ya Akili:

Magonjwa ya akili yanaweza kusababishwa na sababu za kibaiolojia au kisaikolojia.

A) Sababu Za Kibaiolojia.

Zifuatazo ni sababu za kibaiolojia zinazoweza kusababisha magonjwa ya akili ambazo ni pamoja na;

1) Kurithi vinasaba kutoka kwa wazazi (genetic factor).

2) Magonjwa ya muda mrefu kama vile degedege (convulsion), malaria kali (severe malaria), ukimwi n.k

3)  Matumizi ya dawa za kulevya.

B) Sababu Za Kisaikolojia.

Zifuatazo ni sababu za kisaikolojia zinazoweza kusababisha magonjwa ya akili ambazo ni pamoja na;

1) Majanga, ubakaji, uvamizi, ajali, utekaji nyara, kukosa elimu, kukosa ajira n.k.

2) Kufiwa, kutengana, talaka, ugoni, kufungwa.

3) Kufukuzwa kazi, kukosa mishahara, kustaafu kazi n.k

4) Kutofanya vizuri kwenye masomo na kufukuzwa shule/chuo.

5) Matatizo yanayowaathiri watoto.

6) Kunyanyaswa kingono.

7) Kupigwa na kutengwa.

8) Kutothaminiwa.

9) Kutokupata matunzo stahiki.

Dalili Za Magonjwa Ya Akili:

Magonjwa ya akili yapo ya aina nyingi na dalili zake zinatofautiana kati ya ugonjwa mmoja na mwingine.

A) Dalili Za Kihisia.

1) Kusikia sauti ambazo watu wengine hawazikii.

2) Kuona vitu ambavyo watu wengine hawavioni.

3) Kuhisi kufuatiliwa na watu.

4) Wivu uliopitiliza.

5) Kuhisi mawazo yake yanajulikana na watu wengine au yanazungumzwa kwenye vyombo vya habari.

6) Kuhisi kuwa mtu anatumia mawazo yake kufanya mambo fulani.

7) Kuhisi harufu ambayo watu wengine hawaisikii.

8) Kuhisi maisha hayana thamani na kuona bora kufa kuliko kuishi.

B) Dalili Za Kimwili.

1) Kukosa furaha au kuwa na furaha kupita kiasi.

2) Kuwa na wasiwasi au woga kupita kiasi.

3) Kupunguza kuongea au kuongea kupita kiasi.

4) Hasira za haraka na kufikia hatua ya kudhuru watu au kuharibu vitu.

5) Kuwa na msongo wa mawazo.

6) Kujitenga na watu na kupenda kukaa mwenyewe muda mwingi.

7) Kutokuwa na ari (mood) ya kufanya kazi au kufanya kazi nyingi kwa wakati mmoja bila kuzikamilisha.

8) Kutokujijali usafi na muonekano wake.

9) Kutokuonyesha hisia yoyote usoni mwake (furaha au uzuni).

10) Maumivu sehemu mbalimbali za mwili ambayo vipimo vya hospitali havionyeshi tatizo lolote la kimwili.

C) Dalili Za Kiakili.

1) Kukosa umakini wa shughuli zake za kila siku.

2) Kusahau kwa haraka au kupoteza kumbukumbu.

3) Kukosa uwezo wa kupambanua mambo kwa mitazamo tofauti.

4) Kutokujali.

5) Kuwa na imani zisizo za kawaida kama vile;

     i) Kuwa mtu maarufu au nabii.

     ii) Kupokea taarifa kutoka kwenye redio au mitandao ya simu.

     iii) Imani ya kuwasiliana na watu maarufu.

     iv) Kuamini kuwa na nguvu ya ziada kutoka nje ya mwili.

      v) Imani kuwa kuna watu wanamfuatilia au wanataka kumdhuru.

6) Mawazo yake hayana mtiririko unaoeleweka.

memory loss

Tiba Ya Magonjwa Ya Akili:

Matibabu ya magonjwa ya akili hutofautiana kati ya ugonjwa mmoja na mwingine.

Matibabu hayo ni pamoja na;

1) Elimu kwa jamii kuhusiana na  magonjwa ya akili ni kitu cha muhimu sana katika kuzuia kujirudia au kupata ugonjwa wa akili, juu ya matibabu na msaada anaohitaji mgonjwa ili kuendelea na maisha yake ya kila siku.

2) Kupatiwa uchunguzi mapema ili apatiwe tiba sahihi na ya mapema.

3) Tiba ya kisaikolojia (kujitambua aliko, anapotaka kuwa na kuamua kufanya mabadiliko kwa kutegemea uwezo wake mwenyewe).

4) Tiba kimwili kutumia dawa za hospitali.

5) Matibabu kwenye nyumba za upataji nafuu (sober house).

6) Ushirikiano kati ya mgonjwa, familia na wataalamu wa tiba huleta mafanikio makubwa sana katika matibabu.

7) Kutokutumia madawa ya kulevya ikiwa ni pamoja na vilevi.

8) Kupata muda mrefu wa kupumzika.

9) Fanya mazoezi.

10) Usijitenge na jamii.

11) Kujibidisha kwenye shuguli za kuleta kipato.

HITIMISHO:

Kwa msaada wa ushauri na tiba ya magonjwa ya afya ya akili, tembelea hospitali iliyokaribu nawe uonane na daktari bingwa wa magonjwa ya afya ya akili (psychiatrist).

Ni mimi mwenye kujali afya yako Dr Isaya Febu.