Yajue Magonjwa Ya Zinaa, Dalili, Tiba, Madhara Na Jinsi Ya Kujikinga.

Magonjwa Ya Zinaa:

Magonjwa ya zinaa ni magonjwa ya maambukizi zaidi ya 25 ambayo kimsingi husambazwa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine kwa kujamiiana, kulawiti au kulamba sehemu za siri. Magonjwa ya zinaa hujulikana kwa kitaalamu kama Sexually Transmitted Diseases (STDs).

Magonjwa ya zinaa ni miongoni mwa maambukizi yanayofahamika sana na yaliyoleta madhara makubwa hasa katika nchi zinazoendelea ambazo nyingi ziko barani Afrika.

Kwa mujibu wa takwimu za shirika la afya duniani (WHO), zaidi ya watu milioni moja duniani kote wanaambukizwa magonjwa ya zinaa kila siku. Kulingana na WHO, magonjwa ya zinaa huathiri uwezo wa kujamiiana na uzazi, na huongeza hatari ya ugumba, matatizo ya ujauzito, saratani na VVU/UKIMWI.

Visababishi Vya Magonjwa Ya Zinaa:

Magonjwa ya zinaa huambukizwa na wakala wa magonjwa – bakteria, virusi, fungi na protozoa wakaao katika sehemu vuguvugu na zenye unyevunyevu katika mwili kama vile sehemu za siri, mdomoni na kooni. 

Magonjwa mengi ya zinaa husambaa wakati wa kijamiiana (katika uke au mkunduni), lakini aina nyingine za kukutana kimapenzi kama kwa kutumia midomo (oral sex) zinaweza kusambaza magonjwa.

Magonjwa mengine ya zinaa yanaweza kusambazwa kwa njia nyingine zaidi ya kujamiiana. Magonjwa fulani ya zinaa yanayosababishwa na virusi kama UKIMWI yanaweza kuambukizwa kwa kukutana na damu iliyoathirika. Kwa mfano, magonjwa yanayosababishwa na virusi yanaweza kusafiri miongoni mwa watu wanaochangia sindano zilizo na maambukizi, na mtu anaweza kupata maambukizi kwa kupokea dawa iliyoambukizwa. Baadhi ya magonjwa ya zinaa huambukiza kwa kutoka kwa mama hadi kwa mtoto. 

Maambukizi yanaweza kutokea kabla ya kuzaliwa, wakati vijidudu vikifanikiwa kupita katika kondo la uzazi (placenta, ogani katika mji wa mimba wa mwanamke mjamzito ambayo huunganisha mfumo wa damu ya mama na wa mtoto) na kuingia katika mkondo wa damu wa mtoto.

 Maambukizi pia huweza kutokea wakati wa kujifungua, wakati mtoto anapopita katika njia ya uzazi au baada kujifungua, wakati mtoto anapotumia maziwa yaliyoambukizwa.

Magonjwa ya zinaa hayawezi kuambukizwa kwa kupeana mikono au kugusana, au kugusa nguo au katika viti vya chooni.

magonjwa ya zinaa

Leo katika makala yetu tutazungumzia baadhi ya magonjwa ya zinaa ambayo yanaweza kuambukizwa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine kupitia ngono isiyo salama na tiba zake.

Magonjwa Ya Zinaa Na Tiba Zake:

Yafuatayo ni baadhi ya magonjwa ya zinaa ambayo yanaweza kuambukizwa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine kupitia ngono isiyo salama na jinsi ya kutibu.

1) Kaswende.

Huu ni ugonjwa wa zinaa unaosababishwa na bakteria anayejulikana kama Treponema pallidum. Ugonjwa huu unajulikana kwa kitaalamu kama Syphilis.

 Treponema pallidum

Katika hatua za mwanzo, vipele katika sehemu za uzazi huanza kujitokeza muda mfupi baada ya maambukizi ambavyo baadaye hupotea vyenyewe.

Kama ugonjwa hautatibiwa, maambukizi huendelea kwa miaka, yakishambulia mifupa, ubongo na moyo na kusababisha madhara mengine yanayotokana na matatizo katika mfumo wa fahamu kama vile homa ya uti wa mgongo na magonjwa ya moyo na kiharusi (stroke).

Kaswende wakati wa ujauzito inaweza kuwa hatari kubwa kwa kiumbe aliye tumboni, kama vile kusababisha kutoumbika vizuri (deformity) na kifo.

Wanawake wengi wajawazito katika nchi zilizoendelea huchunguzwa kwa uwepo wa ugonjwa huu katika majuma ya kwanza ya mimba ili kutibu ugonjwa kabla kitoto hakijaathirika.

kaswende

Tiba Ya Kaswende.

Kaswende hutibiwa kwa antibiotiki, Penisilini ya Benzathine (Benzathine penicillin) ndiyo chaguo la kwanza la tiba kwa hatua zote za kaswende.

Machaguo mengine, haswa ikiwa mtu aliyeathirika ana mzio (Allergy) wa penisilini, ni doxycycline na ceftriaxone. Penisilini ya Benzathine kwa kawaida ni sindano inayochomwa kwenye misuli (Intramuscularly), wakati doxycycline na ceftriaxone kwa kawaida huchomwa kwenye mishipa ya damu (Intravenously) au misuli (Intramuscularly). Dawa zote tatu hutolewa kwa dozi kubwa, kwa siku moja au siku kadhaa mfululizo. Penisilini ya Benzathine inaweza kutolewa katika dozi tofauti, kulingana na hatua iliyofikia kaswende inayotibiwa.

Soma pia hii makala: Mambo Muhimu Usiyo yajua Kuhusu Ugonjwa Wa Kaswende.

2) Klamidia.

Huu ni ugonjwa wa zinaa unaosababishwa na bakteria anayejulikana kama Chlamydia trachomatis. Ugonjwa huu unajulikana kwa kitaalamu kama chlamydia.

Chlamydia trachomatis

Mara nyingi ugonjwa huo huwa hauonyeshi dalili za wazi kwa karibia asilimia 75 ya wanawake na asilimia 50 ya wanaume, hivyo maambukizi mengi hushindwa kufahamika mapema.

Watu ambao hawajafahamu kuwa wameambukizwa klamidia wanaweza wasitafute tiba na hivyo wakaendelea kufanya ngono, bila ya kujua kuwa wanaeneza ugonjwa.

Wakati dalili zinapoanza kujitokeza wanaume husikia maumivu wakati wa kukojoa au kutokwa usaha katika uume. Wanawake wanaweza kutokwa damu nje ya kipindi chao (hedhi), maumivu wakati wa kukojoa, kutokwa usaha katika uke, au maumivu chini ya kitovu.

Kama utaachwa bila kutibiwa kwa wanawake, klamidia inaweza kuleta madhara makubwa kwa afya binafsi na ya jamii. Klamidia uharibu tishu za uzazi za mwanamke na kusababisha uvimbe katika mfupa wa nyonga (pelvic inflammatory disease, PID). PID inaweza kusababisha maumivu makali sana katika mfupa wa nyonga, utasa/ugumba au utata katika ujauzito ambao unaweza kusababisha kifo.

Watoto waliozaliwa na mama aliyembukizwa klamidia huwa na hatari ya kupata upofu au maambukizi katika mapafu.

Uchunguzi wa maambukizi ya klamidia hufanyika kwa kuchunguza mfupa wa nyonga na kiwango kidogo cha majimaji kutoka katika uke au uume ambayo huchunguzwa kwa uwepo wa Chlamydia trachomatis.

Uchunguzi mpya kama ule wa mkojo ili kufahamu uwepo wa bakteria wa klamidia umekuwa ukitumika pia ili kufanya uchunguzi rahisi zaidi wa watu ambao hawaonyeshi dalili za ugonjwa.

Tiba Ya Klamidia.

Matibabu ya chlamydia yanahusisha matumizi ya antibiotics, doxycycline, azithromycin, amoxicillin, ofloxacin au erythromycin. Mara nyingi matumizi ya antibiotics katika kutibu ugonjwa wa klamidia huhusisha mchanganyiko wa dawa zaidi ya moja, hivyo ni vyema ukawasiliana na daktari wako ili kujua mchaganyiko wa dawa unaokufaa.

Matibabu haya ya ugonjwa wa klamidia yanatakiwa kutolewa kwa mtu na mpenzi wake aliyeshiriki nae ngono. Pia ikiwa mwathirika wa ugonjwa huu ana wapenzi wengi, wote wanabidi watumie dawa hizo au kuacha kushiriki nao ngono ili kuepuka maambukizi mapya.

Soma pia hii makala: Mambo 7 Muhimu Usiyo yajua Kuhusu Ugonjwa Wa Pangusa.

3) Kisonono.

Huu pia ni ugonjwa wa zinaa unaosababishwa na bakteria anayejulikana kama Neisseria gonorrhoeae. Bakteria hizo hushambulia utandotelezi unaozunguka sehemu za sirii. Ugonjwa huu unajulikana kwa kitaalamu kama Gonorrhea.

 Neisseria gonorrhoeae

Kama ilivyo klamidia, kisonono nayo huwa haionyeshi dalili. Kisonono ikiwepo huwa na dalili kama zile za klamidia ambazo huhusisha maumivu wakati wa kukojoa na kutokwa kwa maji yanayonuka au usaha katika uke au uume.

Kisonono huonekana kwa urahisi kwa wanaume ambao hutoa usaha kutoka katika mfereji wa mkojo (urethra). Huanza kidogo, lakini huongezeka na huwa mwingi na kusababisha kusikia haja ya kukojoa mara kwa mara huku kukiwa na maumivu.

Kisonono isiyotibiwa inaweza kusababisha PID (Pelvic Inflammatory disease) kwa wanawake. Watoto wanaozaliwa na mama wenye kisonono huwa na hatari ya kuambukizwa wakati wa kuzaliwa; maambukizo haya yanaweza kusababisha magonjwa ya meno kwa wachanga.

 Gonorrhea

Jinsi Ya Kupima Kisonono.

Uchunguzi wa ugonjwa wa kisonono hufanywa kwa kuchunguza usaha kutoka katika uke au uume au mkojo kwa uwepo wa Neisseria gonorrhoeae.

Tiba Ya Kisonono.

Kuna malengo mawili katika kutibu ugonjwa wa kisonono.  Lengo la kwanza ni kutibu maambukizi ya mgonjwa. Lengo la pili ni kuwatafuta na kuwapima watu wengine wote ambao wamefanya ngono na mgonjwa, ili kuwatibu na kuzuia maambukizi zaidi. Usijitibu mwenyewe bila kuonwa na daktari kwanza. Mtoa huduma wa afya ataamua ni matibabu gani yaliyo bora zaidi. Matibabu yanayopendekezwa ni pamoja na;

a) Sindano moja ya ceftriaxone 125 mg au kumeza dozi moja ya cefixime 400mg.

ceftriaxone

b) Dozi moja ya Azithromycin 2g inaweza kutumika kwa watu wenye mzio (allergy) wa ceftriaxone, cefixime, au penicillin.

Azithromycin

Kumbuka: Mgonjwa anapaswa kurejea hospitalini baada ya siku 7. Vipimo vitafanywa tena, kuhakikisha maambukizi yamekwisha. Watu wote waliofanya ngono na mgonjwa wanapaswa kutafutwa ili wapimwe na kutibiwa. Hii hupunguza kuenea kwa kisonono.

Soma pia hii makala: Haya Ndiyo Mambo 7 Muhimu Usiyo yajua Kuhusu Ugonjwa Wa Kisonono.

4) Malengelenge Sehemu Za Siri.

Ugonjwa wa malengelenge katika sehemu za siri husababishwa na maambukizi ya Herpes Simplex Virus (HSV). Aina nyingi za malengelenge huwa ni kutokana na aina ya pili ya HSV (HSV type 2).

Herpes Simplex Virus

Hata hivyo, maambukizi kutokana na aina ya kwanza ya HSV (HSV type 1) nayo yapo. Malengelenge katika sehemu za siri husababisha vivimbe vinavyouma vinavyojirudia kila mara, ingawa mara nyingi ugonjwa huwa hauonyeshi dalili kwa muda mrefu.

Upimaji wa damu huweza kuonyesha uwepo wa maambukizi ya HSV, hata kama mtu bado hajaanza kuonyesha dalili.

Kumbuka:

Kuna aina mbili za herpes zinazosababisha maambukizi haya.

1) HSV type 1- husababisha vidonda vya mdomo (oral herpes).

2) HSV Type 2- husababisha malengelenge sehemu za siri (genital herpes).

Tiba Ya Malengelenge Sehemu Za Siri.

Dalili za HSV zinaweza kutibika kwa kutumia madawa ya yanayopambana na virusi kama vile acyclovir, lakini HSV hawawezi kutoka katika mwili – hawatibiki.

 acyclovir

5) Ukimwi.

UKIMWI, Ukosefu wa Kinga Mwilini, ni matokeo ya maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU) vijulikanavyo kwa kitaalamu kama Human immunodeficiency virus (HIV). 

Human immunodeficiency virus (HIV). 

UKIMWI ni ugonjwa wa zinaa hatari na usitibika ambao hushambulia mfumo wa kinga ya mwili na kumwacha mgonjwa akiwa hana hata uwezo wa kujikinga dhidi ya maambukizi madogo.

Maambukizi ya VVU haimaanishi kuwa mtu ana UKIMWI. Baadhi ya watu na maambukizi ya VVU na wasionyeshe hali ya kuumwa ile inayotambulika kama UKIMWI kwa miaka kumi au zaidi.

Watabibu hutumia neno UKIMWI pale mtu anapokuwa katika hatua za mwisho, zinazotishia uhai za maambukizi ya VVU.

Wakati VVU wanaweza kuenezwa kwa njia nyingine, kujamiiana ndiyo njia hasa ya maambukizi ya virusi hivi. Wanawake ambao wameathirika na virusi vya UKIMWI wanaweza kumwambukiza mtoto wakati wa ujauzito, kujifungua, au mara kadhaa wakati wa kuwanyonyesha.

Njia mbadala ya kupunguza makali ya VVU ni pamoja na kutumia madawa yanayozuia kuzaliana kwa VVU (protease inhibitors), ambayo husaidia kwa kiasi kikubwa kurefu maisha.

anti retro viral therapy

6) Genital Warts.

Huu ni ugonjwa wa zinaa unaosababishwa na virusi vinavyofahamika kama Human papillomavirus (HPV) ambavyo kwa ujumla wake, hupatikana katika aina tofauti zaidi ya 100.

Hivi ni vinyama vidogo vinavyoota kwenye ngozi au utando laini unaozunguka maeneo ya sehemu za siri.

Ugonjwa huu unaweza kudhuru uume, uke, mlango wa uzazi, sehemu ya haja kubwa, mrija wa mkojo, midomo, koo, pamoja na kibofu cha mkojo.

Husambazwa kwa mgusano wa ngozi kwa ngozi hasa wakati wa ngono, japo migusano mingine ya maeneo athirika isiyohusisha ngono inaweza pia kuwa chanzo cha kusambaa kwake.

Dalili kubwa ni kuota kwa nyama kwenye sehemu za siri ambazo zinaweza kuwa ndani ya uke, nje ya uke, mlango wa kizazi, sehemu ya haja kubwa pamoja na sehemu inayopatikana kati ya uke na sehemu ya haja kubwa.

Dalili zingine ni pamoja na;

1) Muwasho sehemu husika.

2) Kuchomwachomwa sehemu husika.

3) Kutokuhisi maumivu (kufa ganzi) maeneo yanayozunguka masundosundo.

4) Kuvuja damu ukeni baada ya tendo la ndoa.

Tiba Ya Genital Warts.

Unaweza kutibiwa kwa kutumia madawa mfano Podophyllotoxin, Podophyllin, 5-fluorouracil na Thiotepa.

Mhudumu wa afya atakuelezea matumizi sahihi ya dawa pamoja na dozi sahihi kwa kadri atakavyoona inafaa.

Masundosundo yanaweza pia kutibiwa kwa upasuaji mdogo, kukausha kwa njia ya barafu, umeme au kwa mionzi maalumu.

Podophyllin cream

Soma pia hii makala: Ujue Ugonjwa Wa Genital Warts (Kuota Vinyama Sehemu Za Siri) Na Tiba Yake.

Dalili Za Magonjwa Ya Zinaa Kwa Mwanaume:

Zifuatazo ni baadhi ya dalili za magonjwa ya zinaa kwa mwanaume ambazo ni pamoja na;

1) Kuwashwa au kuungua kwenye uume.

2) Kutokwa na uchafu kwenye uume.

3) Maumivu kwenye nyonga.

4) Vidonda kwenye uume, mkundu, au mdomoni, chunusi au malengelenge sehemu za siri.

5) Kuungua na usumbufu wakati wa kupitisha mkojo au kinyesi.

6) Kulazimika kutumia choo mara kwa mara.

Dalili Za Magonjwa Ya Zinaa Kwa Wanawake:

Zifuatazo ni baadhi ya dalili za magonjwa ya zinaa kwa wanawake ambazo ni pamoja na;

1) Kuwashwa au kuungua kwenye uke.

2) Kutokwa na uchafu au harufu kutoka eneo la uke.

3) Maumivu kwenye nyonga.

4) Kutokwa na damu ukeni ambayo si ya kawaida.

5) Maumivu wakati wa ngono.

6) Vidonda ukeni, mkunduni, chunusi, malengelenge sehemu za siri, au vidonda mdomoni.

7) Maumivu wakati wa kukojoa.

8) Kulazimika kutumia choo mara kwa mara.

Soma pia hii makala: Jinsi Ya Kupima Magonjwa Ya Zinaa.

Madhara Ya Magonjwa Ya Zinaa:

Magonjwa ya zinaa yana athari mbalimbali katika mwili wako na yanaweza kuleta ugumba, utasa, maumivu ya kiuno ya muda mrefu, kuharibu muonekano wa sehemu za siri na mengine kuongeza hatari ya kupata saratani za shingo ya uzazi au koo.

Jinsi Ya Kujikinga Na Magonjwa Ya Zinaa:

Tofauti na magonjwa mengine hatari, hatua rahisi zinaweza kutumika kuzuia maambukizi ya magonjwa ya zinaa ambazo ni pamoja na;

1) Kuepuka Ngono Kabisa.

Hatua ambayo ni madhubuti kuliko zote ni kuepuka ngono kabisa. Bila ya kukutana kimwili hakuna uwezekano wa kupata maambukizi ya zinaa.

2) Epuka Kuwa Na Mpenzi Zaidi Ya Mmoja.

Kuwa na mwenzi mmoja tu katika ndoa na kwa wale wanaojiingiza katika mahusiano pia husaidia kupunguza hatari ya maambukizi. Acha michepuko! Baki njia kuu. Itakulinda usipate magonjwa ya zinaa na VVU.

3) Tumia Kondomu Kila Unapofanya Mapenzi.

Kondomu inakinga dhidi ya maambukizi ya zinaa lakini si kinga kamili kwa asilimia mia moja. Kondomu huvaliwa kwenye uume au kwenye uke na huwa kama kizuizi kwa vijidudu vinavyosababisha magonjwa ya zinaa. Hata hivyo kondomu huwa haifuniki sehemu yote ya siri ambayo hukutana wakati wa kufanya ngono, na uwezekano wa kupata maambukizi ya zinaa bado upo, hasa malengelenge sehemu za siri.

4) Weka Utaratibu Wa Kupima Vvu Na Magonjwa Ya Zinaa Wewe Na Mpenzi Wako Mara Kwa Mara.

Uchunguzi wa awali na matibabu kamili huzuia madhara zaidi ya maambukizi ya zinaa, wakati huohuo huzuia uambukizaji kati ya mtu mmoja kwenda kwa mwingine. Hii ni muhimu sana kwa magonjwa ya zinaa ambayo huwa hayaonyeshi dalili, kwa sababu wale walioambukizwa huwa hawajui kuwa wana hatari ya kuwaambukiza wenzi wao.

Matibabu yote lazima yafuatwe hata kama matumizi ya awali ya dawa yalipelekea dalili zote kutoweka. Maambukizi yanaweza kuendelea bila ya kuwa na dalili na hivyo kupelekea aliyeambukizwa bila kujua kusambaza ugonjwa.

HITIMISHO:

Kwa msaada wa ushauri, vipimo na tiba ya magonjwa ya afya ya uzazi kwa wanaume na wanawake wasiliana nasi kwa simu namba 0625 305 487.

vipimo vya mfumo wa uzazi