Ujue Ugonjwa Wa Genital Warts (Kuota Vinyama Sehemu Za Siri) Na Tiba Yake.

Ugonjwa wa genital Warts ni hali ya kuota vinyama kwenye ngozi au utando laini unaozunguka maeneo ya sehemu za siri, vinyama hivyo Vinaweza kutokea kwenye uume, uke, mrija wa mkojo (urethra), vulva, shingo ya kizazi (cervix), au maeneo ya kuzunguka njia ya haja kubwa au ndani yake, ni ugonjwa unaoenezwa kwa njia ya kujamiiana.

Ugonjwa huu pia hujulikana kwa kitaalamu kama “Condyloma acuminatum.”

Ugonjwa huu husambazwa kwa mgusano wa ngozi kwa ngozi hasa wakati wa ngono, japo migusano mingine ya maeneo athirika isiyohusisha ngono inaweza pia kuwa chanzo cha kusambaa kwake.

Virusi wanaosababisha ugonjwa huu huwa na uhusiano wa moja kwa moja na kutokea kwa saratani ya mlango wa kizazi, saratani ya koo, uke, uume pamoja na saratani ya njia ya haja kubwa, hivyo ni vyema wagonjwa wakatibiwa haraka na kwa usahihi ili kuepusha changamoto hizi.

Mara baada ya kuambukizwa, ugonjwa huu huweza kuchukua mpaka muda wa wiki sita hadi miezi 6 kwa masundosundo kuwa dhahiri, ingawa baadhi ya wagonjwa wanaweza kukaa hata miaka kadhaa bila kuwa na dalili yeyote ile.

human papilloma virus

Kisababishi Cha Ugonjwa Wa Genital Warts:

Ugonjwa wa genital warts husababishwa na virusi wajulikanao kwa kitaalamu kama Human papilloma virus (HPV). 

Ripoti ya shika la afya duniani (WHO) zinasema kwamba kuna aina zaidi ya 100 ya virusi wa papilloma waliokwisha kugunduliwa mpaka sasa ambapo kati ya hao ni aina mbili tu, HPV-6 na HPV-11 ambao ndio husababisha genital warts.

Kumbuka: Tafiti kadhaa zimeonesha kuwa baadhi ya aina za virusi wa HPV pia husababisha saratani ya shingo ya kizazi (carcinoma of the cervix) kwa wanawake au saratani ya njia ya haja kubwa (anal cancer) kwa jinsia zote mbili. Aina hii ya virusi hujulikana pia kama high-risk HPV.

Picha ya vinyama ukeni:

vinyama ukeni
Genital Warts

Tabia Hatarishi Zinazoweza Kupelekea Kupata Ugonjwa Wa Genital Warts:

Zifuatazo ni tabia hatarishi zinazomuweka mtu katika hatari ya kupata ugonjwa wa genital warts ambazo ni pamoja na;

1) Kuwa Na Wapenzi Wengi.

Ikiwa una wapenzi wengi (multiple sexual partners) na hautumii kinga (condom) wakati wa kushiriki ngono basi unajiweka katika hatari ya kupata ugonjwa wa genital warts.

2) Kufanya Ngono Isiyo Salama Na Mwathirika Wa Hpv.

Ikiwa unashiriki ngono isiyo salama na mtu aliyeathirika na virusi wa Hpv basi unajiweka katika hatari kubwa ya kupata ugonjwa wa genital warts. Pia kufanya ngono kwa kutumia mdomo inakuweka katika hatari ya kupata warts au kuota vinyama sehemu za mdomo.

3) Ngono katika umri mdogo.

Watu wanaoanza ngono mapema wapo kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata genital warts kutokana na kinga za mwili kua chini sana.

4) Matumizi Makubwa Ya Sigara Na Pombe.

Tafiti zinaonesha kwamba watu wenye matumzi makubwa ya pombe na sigara wanajiweka katika hatari ya kupata ugonjwa wa genital warts.

5) Upungufu wa kinga mwilini (immunosuppression).

Kuwa na upungufu katika mfumo wa kinga mwilini kutokana na magonjwa mbalimbali kama vile kisukari, HIV, cancer au kwa sababu ya matumizi ya dawa fulani humuweka mtu katika hatari kubwa ya kupata ugonjwa wa genital warts. Pia hali ya kuwa na lishe duni (malnutrition) husababisha kushuka kwa kinga ya mwili hivyo kupelekea mtu kuwa katika hatari ya kupata ugonjwa wa genital warts.

Dalili Za Ugonjwa Wa Genital Warts:

Ugonjwa wa genital warts huonekana kama vioteo laini vinavyojitokeza juu ya ngozi ingawa wakati mwingine vinaweza kuwa vidogo mno kiasi cha kutoweza kuonekana vizuri kwa macho ya kawaida.

Kwa wanaume, vioteo hivi hutokea zaidi kwenye uume, ngozi ya pumbu, eneo la mitoki, mapajani pamoja na maeneo ya kuzunguka nje ya njia ya haja kubwa au ndani yake; wakati kwa wanawake hutokea ndani ya uke au njia ya haja kubwa, nje ya uke au ngozi ya nje kuzunguka njia ya haja kubwa, au ndani ya uke kuzunguka eneo la shingo ya kizazi.

Kwa wale wanaopenda kufanya ngono ya mdomoni (oral sex), wanaweza kupatwa na masundosundo/genital warts kwenye maeneo ya kuzunguka mdomo (lips), kwenye ulimi na hata kwenye utando unaozunguka koo.

Dalili nyingine ya ugonjwa wa genital warts ni kama vile mgonjwa kujihisi kukosekana kwa hisia (kufa ganzi) maeneo yaliyozungukwa na masundosundo.

kwa wanawake kuongezeka kwa utoko/ uchafu sehemu za siri, kuwashwa sana maeneo ya siri na wakati mwingine kutokwa na damu ukeni mara baada ya tendo la ngono. Hata hivyo dalili hizi hutokea mara chache sana.

Wanawake wengi vijana wanaojihusisha na vitendo vya ngono [sexually active] huambukizwa sana ugonjwa huu lakini wengi wao hupona bila hata kuhitaji matibabu, wakati wanaume wanaoambukizwa, wengi wao huwa hawaoneshi dalili zozote za ugonjwa ingawa wanaweza kuwaambukiza wenzi wao bila ya wao kujua.

Soma pia hii makala: Haya Ndiyo Mambo 7 Muhimu Usiyo yajua Kuhusu Ugonjwa Wa Kisonono.

Uchunguzi Na Vipimo Vya Ugonjwa Wa Genital Warts:

Kwa wanawake, uchunguzi wa ugonjwa wa genital warts/masundosundo hujumuisha uchunguzi wa maeneo ya nyonga (pelvic examination) ambapo daktari huchunguza eneo hilo kwa kutumia vifaa maalum vinavyomuwezesha kuona uwepo wa masundosundo na wapi vilipo. Wakati fulani, kunyunyizia dawa yenye tindikali ya acetic acid husaidia kufanya masundosundo kuonekana kwa urahisi zaidi. Wakati mwingine daktari anaweza pia kufanya kipimo cha pap smear kwa ajili ya uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi (kwa vile kama tulivyoona hapo awali, zipo aina fulani za HPV ambazo husababisha saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake).

Kwa wanaume, uchunguzi wa maeneo ya siri ni muhimu sana ili kufahamu kama kuna masundosundo au la.

Matibabu Ya Ugonjwa Wa Genital Warts:

Ni vema genital warts zitibiwe hospitali na daktari, haishauriwi kutumia dawa za kununua kujitibu mwenyewe kwa vile kuna uwezekano mkubwa wa kuchanganya aina ya dawa zinazotumika maalum kutibu aina nyingine za warts kwa ajili ya kujitibu genital warts.

Matibabu ya genital warts hufanyika hospitali kwa kuondoa vioteo juu ya ngozi iliyoathirika au kwa kutumia dawa utakazoandikiwa na daktari na kuelekezwa namna ya kuzitumia mwenyewe nyumbani kwa siku kadhaa mpaka majuma kadhaa. Dawa zinazotumika ni pamoja na Podophyllin na podofilox, Trichloroacetic acid (TCA) au Imiquimod.

Jinsi Ya Kutumia Podophyllin:

Chukua kiasi kidogo cha podophyllin cream, paka kwenye genital warts kwa kutumia pamba safi, subiri podophyllin cream ikae kwenye genital warts angalau kwa muda wa saa1 mpaka masaa 4 baada ya hapo osha eneo lilioathiriwa na genital warts kwa kutumia maji safi. Rudia hayo matibabu kila wiki kwa muda wa wiki nne mpaka wiki sita au mpaka pale genital warts zitakapokuwa zimeondoka kabisa.

Ukiachilia mbali matumizi ya dawa, masundosundo yanaweza pia kutibiwa kwa njia ya upasuaji mdogo kama vile kwa kuvikata, au kuvimaliza kwa kutumia njia ya baridi/barafu (Cryosurgery), njia ya umeme (Electrocauterization) au kuvikausha kwa kutumia mionzi maalum ya laser (Laser therapy).

Matibabu ya masundosundo, kama yalivyo matibabu ya magonjwa mengine yanayosambaa kwa njia ya ngono, ni lazima yahusishe pia tiba kwa mwenza wa mgonjwa. Wakati mwingine hata kama utajihisi huna dalili za waziwazi, ni vema kumuona daktari ili uchunguzwe na kutibiwa kuepusha kusambaza ugonjwa kwa watu wengine au kuachia ugonjwa mpaka ukakuletea madhara zaidi.

Aidha matibabu yanaweza kuhitaji kurudiwa rudiwa mara kadhaa mpaka masundosundo yatakapokuwa yametoweka kabisa. 

Kwa wanawake ambao wametibiwa genital warts na kupona au wale ambao wamewahi kuwa na wenza waliowahi kuugua ugonjwa huu, wanashauriwa sana kufanya uchunguzi wa mara kwa mara wa shingo za kizazi (pap smear). Kwa wanawake waliowahi kuugua genital warts, ni vema kufanya pap smear walau kila baada ya miezi 3 mpaka 6 tangu kupata matibabu ya awali ya genital warts.

Madhara Ya Ugonjwa Wa Genital Warts:

Kwa baadhi ya wagonjwa, masundosundo yanaweza kuwa mengi na makubwa sana kiasi cha kuhitaji matibabu ya muda mrefu na ghali zaidi pamoja na ufuatiliaji wa kina.

Jinsi Ya Kujikinga Na Ugonjwa Wa Genital Warts:

Njia mojawapo ya uhakika kabisa ya kujiepusha na ugonjwa wa genital warts pamoja na magonjwa mengine ya ngono/zinaa ni kujiepusha na matendo ya ngono na zinaa kabisa. 

Lakini kwa wale ambao ni ngumu kufanya hivyo, wanaweza kupunguza uwezekano wa kupatwa na ugonjwa huu kwa kujihusisha kingono na mwenza mmoja tu ambaye una uhakika kuwa hajaambukizwa wala hayupo katika hatari ya kuambukizwa magonjwa haya.

Tofauti na magonjwa mengine ya zinaa, matumizi ya condom hayana uhakika wa asilimia mia moja katika kukukinga dhidi ya HPV kwa sababu virusi wa HPV au hata masundosundo yanaweza kuwa nje nje kwenye ngozi ambayo uwezekano wa kugusana ni mkubwa.

Pamoja na hayo, bado condom inaweza sana kupunguza hatari ya kuambukizwa masundosundo ikiwa tu itatumika vema na inashauriwa kuitumia mara zote unapokutana kingono na mwenza usiye na uhakika naye. Tukumbuke kila wakati kuwa HPV inaweza bado kuambukizwa kwa mtu hata kama mwenza hana masundosundo yanavyoonekana au hana dalili zozote zile. 

Ikiwa kuna uwezekano, ni vyema kwa wanawake wote wenye umri wa miaka kati ya 9 mpaka 26 kupata chanjo dhidi ya virusi wa HPV ili kuzuia uwezekano wa kuambukizwa virusi hao ambao hatimaye husababisha saratani ya shingo ya kizazi.

HITIMISHO:

Ikiwa utahitaji virutubisho kwa ajili ya kutokomeza changamoto ya kuota vinyama sehemu za siri, genital warts bonyeza hapa: “Jinsi Ya Kutibu Ugonjwa Wa Kuota Vinyama Sehemu Za Siri Bila Kufanya Upasuaji.”

Lakini pia, kwa uhitaji wa updates, vitabu (e-books) bure kuhusu afya jisajili (subscribe) kupitia email yangu kwa kubonyeza hii link: https://isayafebu.beehiiv.com/subscribe