Yajue Mambo Muhimu Kuhusu Ugonjwa Wa Figo.

Figo ni miongoni mwa viungo muhimu katika mwili wa binadamu. Kwa kawaida binadamu ana figo mbili ambazo ni figo ya kulia na figo ya kushoto, figo ya kushoto ni kubwa kidogo kuliko figo ya kulia. Viungo hivi vyenye kazi kubwa ya kuchuja damu mwilini huwa na umbo linalofanana na maharage.

Upande wa sehemu za juu ya figo zimehifadhiwa na ubavu wa kumi na moja na wa kumi na mbili, katika kila figo pamoja na tezi ya adrenali zimefunikwa na ngozi zenye mafuta na renal fascia inayosaidia kuimarisha figo.

Watu wachache wamezaliwa na figo moja tu, hali hiyo hujulikana kwa kitaalamu kama “unilateral agenesis” pia kuna watu wachache waliozaliwa bila figo lolote, hali hiyo inajulikana kwa kitaalamu kama “bilateral agenesis”.

figo

Kazi Za Figo Katika Mwili:

Figo hufanya kazi muhimu mwilini ambazo ni pamoja na;

1) Kudhibiti na kuhifadhi virutubishi na maji na kuondoa mabaki kupitia mkojo.

2) Kuchuja damu ili kuondoa mabaki ambayo ni sumu mwilini. Baadhi ya mabaki hayo ni urea, uric acid, creatinine na ammonia.

3) Kudhibiti viwango vya electrolyte mwilini, yaani Sodium (Na+) na Potassium (K+). Sodium husaidia kudhibiti wingi wa maji mwilini na pia huwezesha mawasiliano kati ya mfumo wa fahamu na misuli (enhances communication between brain/nerves and muscles). Potassium husaidia mapigo ya moyo (regulates heart beats) na kazi ya misuli (muscle function). Viwango vya kawaida kwa Sodium ni 135 – 145 mmol/ L na Potassium ni 3.5 – 5 mmol/L.

4) Kudhibiti shinikizo la damu kupitia mfumo wa renin – angiotensin.

5) Kutengeneza kichocheo cha erythropoietin ambacho huchochea utengenezaji wa chembechembe nyekundu za damu.

6) Kuchochea vitamini D ambayo hutumika katika kudhibiti kiwango cha Calcium na Phosphorous kwenye mifupa.

Kumbuka: Iwapo mtu atapata ugonjwa wa figo ambao utaathiri figo zote mbili, kazi zote hizo hapo juu huathirika au kushindwa kufanyika kwa ufanisi na madhara hutokea kutegemea kiwango cha athari. Figo zinaweza kushindwa kufanya kazi aidha kwa sababu za kipindi kifupi (acute renal failure) au kwa sababu za muda mrefu (chronic renal failure).

Sababu Zinazoweza Kufanya Figo Zishindwe Kufanya Kazi:

A) Katika Muda Mfupi:

1) Upungufu mkubwa wa ujazo wa damu (kupoteza damu kwa kiasi kikubwa).

2) Upungufu wa maji mwilini kutokana na kutapika, kuhara, na homa. 

3) Matumizi ya baadhi ya dawa kama diuretics. 

4) Mawe kwenye figo (kidney stones).

5) Maambukizi kwenye figo mfano sepsis. 

6) Uvimbe-uchungu (inflammation) kwenye mfumo wa uchujaji kwenye figo (acute glomerulonephritis).

7) Uvimbe mkubwa wa tezi dume (prostatic hypertrophy).

8) Saratani ya tezi dume (prostate cancer).

B) Katika Muda Mrefu:

1) Kisukari kisichodhibitiwa.

Soma pia hii makala: Soma Hii Kama Unataka Kutibu Ugonjwa Wa Kisukari Ndani Ya Siku 30.

2) Shinikizo kubwa la damu lisilodhibitiwa (uncontrolled hypertension).

Soma pia hii makala: Yajue Mambo 5 Muhimu Kuhusu Shinikizo La Juu La Damu.

3) Uvimbe – uchungu wa kudumu kwenye mfumo wa uchujaji wa figo (chronic glomerulonephritis).

4) Mawe kwenye figo.

5) Magonjwa ya tezi dume (Prostate disease).

Dalili Za Ugonjwa Wa Figo:

Mwanzoni, ugonjwa wa figo hauoneshi dalili yeyote. Mara utendaji kazi wa figo unapopungua, dalili hujitokeza kuendana na udhaifu wa kudhibiti maji na electrolyte mwilini; kuondoa mabaki mwilini, kutengeneza erythropoetin ambayo huchochea utengenezaji wa chembechembe nyekundu za damu, na pia udhaifu wa kuchochea Vitamini D ambayo ni muhimu katika kuweka viwango sahihi vya calcium – phosphorous kwenye mifupa, misuli na neva.

Dalili za mwanzo ni kama;

1) Kudhoofika. 

2) Kuchoka mara kwa mara. 

3) Kukosa nguvu.

4) Kukosa pumzi/kupumua kwa shida.

5) Kuvimba mwili (hasa usoni).

6) Homa isiyokuwa kali.

Kumbuka:

1) Hali hii isipogundulika mapema huweza kusababisha hatari ya kupoteza maisha.

2) Udhaifu wa kutoa Sodium (Na+) mwilini husababisha wingi wa Sodium mwilini (hypernatremia) ambao huambatana na kujaa kwa maji mwilini (generalized oedema) kuongezeka uzito ghafla, ongezeko la shinikizo la damu, kushindwa kupumua na mwisho husababisha ugonjwa wa moyo (congestive heart failure).

3) Udhaifu wa kutoa Potassium (K+) mwilini husababisha wingi wa potassium mwilini (hyperkalemia) ambao husababisha misuli kukosa nguvu au kuwa dhaifu na mapigo ya moyo kuenda ovyo ovyo (arrhythmias) na ikizidi huweza kusababisha kifo cha ghafla.

4) Kushindwa kutolewa kwa urea mwilini husababisha uharibifu kwenye ubongo (encephalopathy).

5) Udhaifu kwa ujumla husababishwa na upungufu mkubwa wa damu ambao husababishwa na kushuka kwa uwezo wa figo kutengeneza erythropoietin hivyo chembechembe nyekundu za damu kupungua.

6) Kukosekana kwa uwiano unaotakiwa kati ya phosphorus na calcium, huweza kufanya mifupa kuwa miepesi kuvunjika.

Ushauri Wa Ulaji Kwa Wagonjwa Wa Figo:

Ulaji wa mtu mwenye ugonjwa wa figo unapaswa kudhibitiwa kwa kiasi kikubwa kwani figo haziwezi tena kutoa mabaki ya protini, maji, chumvi na potassium kwa urahisi inapozidi mwilini. Vyakula vyenye chumvi na potassium nyingi viepukwe. Mambo ya kuzingatia katika ulaji ni pamoja na;

1) Punguza Kiasi Cha Nishati–Lishe. 

Kiasi cha nishati–lishe na protini kinapozidi mwilini huzipatia figo ambazo zimeathirika kazi kubwa. Tambua na kuepuka vyakula vyenye mafuta yaliyojificha na pia badili njia za mapishi zinazotumia mafuta mengi.  

2) Punguza Kiasi Cha Vinywaji/Vimiminika.

Ili kupunguza kujaa kwa maji mwilini ambako husababishwa na kushindwa kwa figo kutoa maji mwilini.

Maji yakizidi mwilini husababisha kushindwa kupumua, shinikizo kubwa la damu, kuvimba mwili na huweza kusababisha ugonjwa wa moyo (heart failure). Dhibiti ongezeko la uzito wa mwili kwani huweza kuonesha kuwa maji yamezidi mwilini. 

soft drinks

3) Punguza Kiasi Cha Sodium.

Kiasi cha maji mwilini hudhibitiwa na sodium. Pale sodium inapozidi mwilini husababisha maji kubaki mwilini. Hali hii huweza kusababisha ongezeka la uzito ghafla, kuvimba kwa viungio vya mwili, shinikizo kubwa la damu, kushindwa kupumua na huweza kusababisha ugonjwa wa moyo. Vyakula vyenye sodium kwa wingi ni vyakula vilivyosindikwa kwa chumvi (nyama, samaki, soseji, bacon) Jenga tabia ya kutoongeza chumvi kwenye chakula wakati wa kula.

low sodium foods

4) Punguza Kiasi Cha Potassium.

Madini ya potassium yanapozidi mwilini husababisha misuli kuwa dhaifu na mapigo ya moyo kubadilika na yakizidi sana huweza kusababisha kifo cha ghafla. Ni muhimu kudhibiti kiasi cha potassium kwa ukaribu.

Vyakula vyenye potassium kwa kiasi kikubwa ni pamoja na maparachichi, ndizi mbivu, maboga, machungwa, pichesi, peasi, matunda yaliyokaushwa na maharage.

Vyakula vyenye potassium kwa kiasi kidogo ni pamoja na zabibu, machenza, mahindi mabichi, cauliflower, na matango.

Unaweza kupunguza kiasi cha potassium kwenye chakula kwa kuchemsha na kumwaga maji ya ziada. Kiasi cha potassium kinachoshauriwa kwa siku kwa mtu wa kawaida ni gramu 4.7 (miligramu 4,700). Kwa mgonjwa wa figo inashauriwa gramu 1.5-2.7 (miligramu 1500-2700) kwa siku na kila mlo asizidishe gramu 0.25 (miligramu 250).

5) Punguza Kiasi Cha Protini.

Ni muhimu kuepuka vyakula venye protini nyingi kwani metaboli ya protini huzidisha mabaki kama vile urea, amonia na creatinine ambayo tayari yako juu kwa mtu mwenye ugonjwa wa figo na huleta madhara mwilini.

Inashauriwa kula protini ambazo zinatumiwa na mwili kwa ufanisi bila kuacha mabaki mengi. Vyakula vyenye protini hizo ni pamoja na mayai, samaki, nyama, kuku, maziwa na jibini. Vyakula vyenye protini ambazo huacha mabaki mengi ni pamoja na mbogamboga, matunda, maharage, kunde, mbaazi, mahindi, mtama, karanga, mkate.  

6) Punguza Kiasi Cha Phosphorus. 

Uwiano wa calcium na phosphorus mwilini ni muhimu kuwezesha afya njema ya mifupa, misuli na neva. Phosphorus inapozidi mwilini mifupa huwa myepesi kuvunjika (brittle) na rahisi kuvunjika.

Hii inatokana na mwili kutoa calcium kwenye mifupa ili kukidhi uwiano wa phosphorous iliyozidi. Vyakula ambavyo vina phosphorous kwa wingi ni pamoja maziwa na mazao yake, nyama, shellfish, bran, vyakula ambavyo havijakobolewa, maharage, karanga, korosho na chokoleti.

7) Vitamini Na Madini Ya Nyongeza.

Wagonjwa wa figo huhitaji vitamini na madini ya nyongeza kutokana na kutokula aina mbalimbali za vyakula na hivyo kuweza kusababisha upungufu wa baadhi ya virutubishi.

Damu inapochujwa (dialysis) pia huondoa vitamini kwenye damu. Virutubishi vya nyongeza vitolewe kwa mgonjwa wa figo kwa ushauri wa daktari.

Wagonjwa Ambao Damu Inasafishwa Kwa Mashine (Dialysis):

Figo zinaposhindwa kabisa kufanya kazi mashine ya kuchuja damu hutumika kuondoa mabaki mwilini. Mgonjwa unatakiwa kuendelea kufuata ushauri wa ulaji kama alivyoshauriwa.

Mambo Ya Kuzingatia Kwa Mgonjwa Anayefanyiwa Dialysis:

1) Kutumia vyakula vyenye protini inayotumika na mwili kwa ufanisi.

2) Kumeza vidonge vya madini chuma kufidia damu kidogo inayopotea mwisho wa dialysis.

3) Kufanya mazoezi ya mwili.

4) Kuepuka matumizi ya pombe na sigara.

5) Kuepuka msongo wa mawazo.

HITIMISHO:

Kwa ushauri na tiba ya magonjwa ya afya ya uzazi wasiliana nasi kwa simu namba 0625 305 487.

Ni mimi mwenye kujali afya yako Dr. Isaya Febu.