Yafahamu Magonjwa ya Moyo Na Jinsi Ya Kujikinga.

Magonjwa ya moyo yanahusisha yale magonjwa yote yanayoathiri moyo na mishipa yake. Magonjwa ya moyo yanajumuisha coronary heart diseases, myocardia infaction (heart attack), congestive heart failure na atherosclerosis.

Tafiti zimeonesha kuwa magonjwa ya moyo huanza pale ambapo sehemu ya ndani ya kuta za mishipa ya damu zimeharibiwa. Mambo yanayochangia katika kuharibu mishipa ya damu ni pamoja na: Uvutaji wa sigara (nikotini), kuwepo na kiwango kikubwa cha aina fulani za mafuta na lehemu (cholesterol) katika damu, kuwa na uzito uliozidi au unene uliokithiri, shinikizo kubwa la damu, na  Kuwa na kisukari. 

Kuta za mishipa ya damu zikiharibiwa, mafuta hujikusanya katika sehemu ya mishipa iliyoharibiwa na kutengeneza utando wa mafuta (plaque). Kadiri muda unavyoendelea ndivyo mafuta haya yanavyozidi kujijenga katika sehemu hiyo hadi kufanya mishipa kuwa myembamba na hivyo kupunguza kiasi cha damu kinachobeba hewa ya oksijeni na virutubishi kwenda kwenye misuli ya moyo.

atherosclerosis

Hatimaye sehemu hiyo ya mshipa inaweza kupasuka. Kama sehemu hiyo ikipasuka, chembe-sahani (platelets) ambazo husaidia mwili kuponya kidonda hujigandisha kwenye mpasuko na hivyo kuanza kujikusanya. Hali hii huongeza mkusanyiko wa chembe-sahani, hivyo kuendelea kufanya mishipa hiyo kuwa myembamba zaidi na hali hiyo husababisha moyo kushindwa kufanya kazi na mtu hupata ugonjwa wa moyo uitwao shambulio la moyo (heart attack).

Mkusanyiko wa mafuta na chembesahani wakati mwingine huweza kumeguka kama mabonge madogo madogo na kusafiri kwenda kuziba mishipa midogo ya damu ya kichwani. Hali hii ikitokea mtu hupata kiharusi na mabonge yakienda kwenye mishipa ya moyo mtu hupata shambulio la moyo.

Hali ya kujijenga kwa mafuta na chembe-sahani hutokea polepole, huchukua muda mrefu na huweza kujitokeza kwa dalili kama kupanda kwa shinikizo la damu.

Mambo Yanayoongeza Uwezekano Wa Kupata Magonjwa Ya Moyo:

Mambo yanayoongeza uwezekano wa kupata magonjwa ya moyo ni pamoja na;

1) Uvutaji wa sigara au utumiaji wa tumbaku kwa kutafuna au kunusa (ugoro).

2) Kutozingatia ulaji bora, ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi, sukari nyingi, chumvi nyingi, lehemu nyingi na kutokula mbogamboga na matunda ya kutosha.

3) Unywaji wa pombe

4) Kuwa na uzito uliozidi au unene uliokithiri.

5) Kutokufanya mazoezi ya mwili mara kwa mara.

6) Kuwa na shinikizo kubwa la damu (Hypertension).

Soma pia hii makala: Yajue Mambo 5 Muhimu Kuhusu Shinikizo La Juu La Damu.

7) Kuwa na ugonjwa wa kisukari.

Soma pia hii makala: Soma Hii Kama Unataka Kutibu Ugonjwa Wa Kisukari Ndani Ya Siku 30.

8) Kuwa na umri zaidi ya miaka 50.

9) Kuwa na historia ya ugonjwa wa moyo katika familia.

Dalili Za Magonjwa Ya Moyo:

Dalili za magonjwa ya moyo hutofautiana kutegemeana na aina ya ugonjwa wa moyo. Hata hivyo, dalili za magonjwa haya ni pamoja na;

1) Maumivu ya kifua (hii ni dalili kuu ya ugonjwa wa moyo).

2) Kujisikia udhaifu, kuchoka sana.

3) Moyo kwenda mbio na kukosa pumzi/ kushindwa kupumua.

4) Kuvimba miguu, tumbo na mishipa ya shingo hujitokeza.

5) Kukohoa.

6) Maumivu ya mgongo, mabega, shingo na taya.

7) Tumbo kujaa, kichefuchefu na kutapika.

8) Matatizo ya usingizi.

9) Kupoteza fahamu.

Kumbuka: Katika shambulio la moyo hakuna dalili inayojitokeza hadi pale moyo unaposhindwa kufanya kazi ghafla (heart attack), au mtu anapopata kiharusi (stroke). Hata hivyo, hadi mtu anapoanza kupata dalili hizo huwa anakuwa ameishi na ugonjwa huo kwa muda mrefu. Hivyo, njia bora ya kugundua mapema dalili ya ugonjwa ni kuchunguzwa afya yako mara kwa mara kabla hujaugua.

Ulaji Unaoshauriwa Kwa Watu Walioathirika Na Magonjwa Ya Moyo:

Ni muhimu sana kwa mgonjwa wa moyo kufuata kwa makini taratibu za matibabu kama alivyoshauriwa na daktari. Mtindo bora wa maisha utachangia sana kupunguza tatizo. Punguza mambo yanayoongeza uwezekano wa kupata ugonjwa wa moyo ikiwa ni pamoja na kufanya yafuatayo;

1) Kupunguza matumizi ya mafuta na epuka mafuta yatokanayo na wanyama, pamoja na nyama yenye mafuta.

2) Kupunguza ulaji wa nyama hususan nyama nyekundu (isizidi nusu kilo kwa wiki).

3) Kupunguza vyakula vyenye lehemu (cholesterol) kwa wingi kwa mfano mayai, maini, moyo, figo, mafuta yenye asili ya wanyama (kama samli na siagi) na nyama nyekundu.

4) Kuepuka vyakula au vinywaji vinavyosababisha ongezeko la uzito, ikiwa ni pamoja vyakula vyenye sukari nyingi au mafuta mengi, soda, juisi bandia na pombe.

5) Kupunguza kiasi cha chumvi unachotumia na epuka vyakula vyenye chumvi nyingi.

6) Kufanya mazoezi ya mwili angalau dakika 30 kila siku.

7) Kuhakikisha una uzito unaoshauriwa kutegemeana na urefu wako.

8) Epuka vyakula vilivyosindikwa kwa mafuta na chumvi nyingi.

9) Kula mbogamboga na matunda kwa wingi katika kila mlo.

10) Kupendelea zaidi kula vyakula vya nafaka zisizokobolewa kama dona na ngano (kama unga wa atta); vilevile ulezi na mtama.

11) Kupendelea zaidi kula vyakula vya jamii ya kunde.

Jinsi Ya Kujikinga Na Magonjwa Ya Moyo:

Unaweza kupunguza uwezekano wa kupata magonjwa ya moyo kwa kufuata mtindo bora wa maisha, ikiwa ni pamoja na;

1) Kutumia mafuta kwa kiasi kidogo na kuepuka yale yanayotokana na wanyama.

2) Kupunguza ulaji wa nyama nyekundu, hususan zenye mafuta.

3) Kuongeza matumizi ya nafaka hasa zile zisizokobolewa kama unga wa dona, unga wa atta, ulezi na mtama.

4) Kuongeza ulaji wa vyakula vya jamii ya kunde, mbogamboga na matunda.

5) Kufanya mazoezi ya mwili angalau dakika 30 kila siku.

6) Kudhibiti uzito wa mwili.

7) Kuepuka msongo wa mawazo.

8) Kuepuka uvutaji wa sigara au utumiaji wa tumbaku.

9) Kutumia dawa za shinikizo kubwa la damu bila kukosa kama ilivyoelekezwa na mtaalamu wa afya.

10) Kuepuka au kupunguza matumizi ya pombe.

11) Kuwa na tabia ya kupima afya yako mara kwa mara ili kujua hali yako ya afya na kugundua mapema kama kuna tatizo.

Kumbuka: Inawezekana usiweze kutimiza yote kwa mara moja, lakini kila unapopiga hatua ni mchango mzuri kwa maisha yako. Jiwekee malengo na anza kuyatimiza hatua kwa hatua. 

HITIMISHO:

Kwa ushauri na tiba ya magonjwa ya afya ya uzazi wasiliana nasi kwa simu namba 0625 305 487. Ni mimi mwenye kujali afya yako Dr. Isaya Febu.