Ujue Ugonjwa Wa Malaria Na Jinsi Ya Kujikinga.

Malaria ni ugonjwa unaosababishwa na maambukizi ya vimelea vinavyoitwa Plasmodium, ambavyo husambazwa kwa kung’atwa na mbu jike aitwaye anopheles ambaye hubeba vimelea hivyo. 

Malaria inatokea katika maeneo ya kitropiki na yanayokaribia tropiki ikiwa ni pamoja na sehemu za Amerika, Asia na Afrika. Malaria ni moja ya changamoto kubwa za kiafya ambazo dunia inakabiliana nazo hivi sasa. Kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni ya Shirika la Afya Duniani (WHO), watu 409,000 walikufa kutokana na ugonjwa huu mwaka 2019, na takriban watu milioni 229 wameambukizwa hivi karibuni. Na haya yote ni pamoja na ukweli kwamba ugonjwa wa malaria unatibika na unaweza kuzuilika.

Ikiwa unaishi au unapanga kutembelea maeneo ambayo yana tishio kubwa la malaria, kuelewa ugonjwa huu kunaweza kukusaidia kuitunza afya yako. 

Malaria ni mojawapo ya magonjwa yaliyoenea sana na ni tatizo kuu la afya ya umma. Kwa kawaida huhusishwa na umaskini, lakini pia ni sababu ya umaskini] na kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya uchumi.

Sababu Za Malaria:

Malaria kwa binadamu husababishwa na aina 5 tofauti za Plasmodium ambazo ni pamoja na plasmodium falciparum, plasmodium vivax, plasmodium ovale, plasmodium malariae na plasmodium knowlesi. Plasmodium falciparum ndiyo iliyoenea zaidi na huchangia takriban 80% ya maambukizi yote ya malaria, na pia inahusishwa na karibu 90% ya vifo vinavyotokana na malaria. Vimelea vya spishi ya Plasmodium huambukiza pia ndege, mitambaazi, nyani, sokwe na panya.

plasmodium

Jinsi Malaria Inavyosambaa:

Karibu mara zote, malaria husambaa kwa kuumwa na mbu jike wa jamii ya anopheles. Kuna spishi tofauti zaidi ya 400 za mbu huyu, na spishi yapata 30 ni wasambazaji wa malaria wanaojulikana. Mbu hawa wasambazaji huanza kuuma giza linapoingia hadi kunapopambazuka. Kasi ya usambazaji hutegemea aina ya kimelea, aina ya mbu msambazaji, binadamu anayeumwa, na mazingira.

Anopheles hutaga mayai yao kwenye maji, ambayo hujiangua na kuwa larvae, na baadaye kutoka kama mbu kamili. Mbu jike huhitaji mlo wa damu ili kutunza mayai yake. Kila jamii ya mbu ana mazingira anayoyapenda zaidi, kwa mfano, wengine hupenda vidimbwi vidogo visivyo na kina kama alama za nyayo, vinavyopatikana vipindi vya mvua kwenye nchi za tropiki.

Katika maeneo mengi, usambaaji ni wa msimu, ukifikia kilele wakati fulani na mara nyingi baada ya msimu wa mvua. Mlipuko wa malaria unaweza kutokea pale hali ya hewa na vitu vingine vitakapochangia usambaaji kwenye maeneo yenye watu wenye kinga za mwili dhaifu au wasio na kinga dhidi ya malaria. Milipuko pia hutokea watu wenye kinga dhaifu wanapoingia maeneo yenye malaria kwa wingi, pale wanapokwenda kutafuta kazi, au kama wakimbizi.

Baada ya kuumwa na mbu, kuna siku 7 hadi 30 ndipo dalili zitakapoanza kujionyesha, hali hii hujulikana kwa kitaalamu kama incubation period (kipindi kati ya kuambukizwa na dalili kutokea). Incubation period ya P.vivax ni siku 10-17 ingawa inaweza kuwa ndefu zaidi (kama mwaka mmoja, au mara chache hadi miaka 30). P.falciparum kwa kawaida ana incubation period fupi zaidi (siku 10-14). Spishi nyingine za plasmodium zinazoleta malaria zina incubation period sawa na ile ya P.vivax.

Vimelea wa malaria wakiisha ingia ndani ya mwili wako, husafiri hadi kwenye maini, ambako watakua na kukomaa. Baada ya siku chache, vimelea wataingia ndani ya mfumo wa damu na kuanza kuambukiza chembechembe nyekundu za damu. Katika muda wa saa 48 hadi 72, vimelea ndani chembechembe nyekundu za damu huzaliana na kusababisha chembechembe hizo kupasuka.

Vimelea huendelea kushambulia chembechembe nyekundu za damu, na kuleta dalili zinazojirudia kwenye vipindi vya siku mbili hadi tatu.

Mara chache sana, malaria huweza kusambazwa kutoka mtu mmoja hadi mwingine, bila ya mbu kuhusika. Hii huweza kutokea kupitia damu tu, kwa mfano katika matukio yafuatayo;

1) Kupandikizwa kiungo

2) Kuongezewa damu.

3) Kutumia sindano na mtu mwingine.

4) Kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wake ambaye bado hajazaliwa.

Visa vya malaria kutokana na kuongezewa damu iliyoambukizwa ni nadra sana.

Kumbuka:

Sio kila wakati mbu wenye maambukizi anapomng’ata mtu, mtu huyo atapata malaria. Idadi ya vimelea ambavyo mbu anabeba huathiri uwezekano wa mtu kupata maambukizi ya malaria. Baadhi ya mbu huweza kuwa na idadi kubwa ya vimelea, na kuwafanya kuwa na uwezekano mkubwa wa kuusambaza ugonjwa huu. 

Malaria iliyosambazwa na mbu pia hutegemea mambo fulani ya hali ya hewa, kama vile joto na unyevu wa kutosha unaomwezesha mbu wa Anopheles kuzaana na kuishi. Hii ndo sababu malaria hutokea kwenye maeneo ya tropiki.

Hali ya hewa ya joto pia huchochea tabia za binadamu zinazoweza kuongeza uwezekano wao wa kung’atwa na mbu kati ya mida ya jioni na alfajiri, mida ambayo mbu wanaosababisha malaria hung’ata watu zaidi. Mifano hujumuisha shughuli za nje kama vile camping, kulala nje na pia kuvaa nguo nyepesi na fupi zinazosababisha ngozi nyingi zaidi kuwa wazi na katika hatari ya kung’atwa na mbu.

jinsi malaria inavyosambaa

Dalili Za Malaria:

Dalili za malaria kwa kawaida huanza kuonekana siku 10 hadi wiki nne baada ya kuambukizwa. Wakati mwingine dalili zinaweza zisionekane kwa miezi kadhaa. Jamii zingine za vimelea huweza kuingia mwilini na zikatulia kwa muda mrefu. Dalili za kawaida za malaria ni pamoja na;

1) Kutetemeka kwa baridi (chills).

2) Homa kali.

3) Kutoka jasho jingi.

4) Kichwa kuuma.

5) Kichefuchefu.

6) Kutapika.

7) Maumivu ya tumbo.

8) Kuharisha.

9) Kupungukiwa damu.

10) Maumivu ya misuli au viungo (Joints).

11) Degedege.

12) Kupoteza fahamu.

13) Macho kuwa ya njano (jaundice).

malaria symptoms

Soma pia hii makala: Yajue Maambukizi Ya Homa Ya Ini Na Jinsi Ya Kujikinga.

Tiba Ya Malaria:

Matibabu ya malaria ambayo daktari wako atapendekeza yatategemea mambo yafuatayo;

1) Aina halisi ya plasmodium inayosababisha malaria.

 2) Ukali wa dalili.

3) Umri, na kama mtu anatarajia mtoto au la.

Orodha Ya Dawa Za Malaria:

Madaktari hutumia dawa mbalimbali kutibu malaria ikiwa ni pamoja na;

1) Chloroquine/Hydroxychloroquine.

Ikiwa dalili si kubwa na unaishi katika eneo ambalo vimelea havijapata upinzani dhidi ya klorokwini, daktari anaweza kukupa mojawapo ya dawa hizi.

hydroxychloroquine

2) Tiba Ya Mchanganyiko Inayotokana Na Artemisinin (Artemisinin Combination Therapy).

Hu ni mchanganyiko wa dawa mbili zinazofanya kazi kwa njia tofauti. Hutumika kutibu hali zisizo kali zaidi za malaria au kama sehemu ya mkakati wa matibabu kamili kwa kesi mbaya zaidi.

Artemisinin Combination Therapy

3) Atovaquone-Proguanil, Artemether-Lumefantrine (ALU).

Mchanganyiko huu hutoa uwezekano mwingine katika maeneo ambayo vimelea vimekuza upinzani dhidi ya klorokwini. Wanaweza pia kupewa watoto.

4) Mefloquine.

Ikiwa klorokwini haiwezekani, dawa hii imehusishwa na athari zisizo za kawaida lakini kubwa kwenye ubongo na inapaswa kuchukuliwa tu kama suluhu la mwisho.

Mefloquine

5) Artesunate.

Ikiwa dalili ni kali, daktari anaweza kufikiria kutumia dawa hii kwa saa 24 za kwanza na kisha kubadili matibabu ya mchanganyiko ya artemisinin kwa siku tatu zijazo.

artesunate

Madhara Ya Malaria:

Yafuatayo ni baadhi ya madhara yanayoweza kutokea endapo mgonjwa mwenye malaria atashindwa kupata matibabu mapema;

 1) Kuvimba kwa mishipa ya damu ya kwenye ubongo, au malaria ya ubongo (Cerebral malaria).
2) Kujaa maji kwenye mapafu (Pulmonary edema).
3) Kushindwa kufanya kazi kwa figo, maini, au bandama.
4) Upungufu wa damu (anemia) kutokana na kuharibiwa kwa seli za damu.
5) Upungufu wa sukari mwilini (Hypoglycaemia).

Jinsi Ya Kujikinga Na Malaria:

Shirika la Afya Duniani (WHO) linashauri kanuni tano zinazojulikana kama ABCDE za kuzuia malaria ambazo ni pamoja na;

1) Awareness (Ufahamu).

Unaposafiri kwenda kwenye eneo lenye malaria, fahamu hatari ya kupata malaria, muda unaochukua dalili za malaria kutokea, na uwezekano wa dalili hizi kuchelewa kutokea pamoja na dalili kuu.

2) Bite Prevention (Kuzuia Kung’atwa). 

Kutumia dawa ya mbu yenye ufanisi, kama vile diethyltoluamide (DEET), na vyandarua wakati wa kulala.

3) Chemoprophylaxis (Kutumia Dawa Kuzuia Maambukizi).

Tumia dawa dhidi ya malaria ikiwa zinahitajika, kuanzia wiki mbili kabla ya kuingia kwenye eneo lenye malaria na kufuata dozi ya dawa ya kila siku au kila wiki.

4) Diagnosis (Utambuzi). 

Inapaswa kufanyiwa utambuzi na kupata matibabu ikiwa homa inatokea wiki moja au zaidi baada ya kufika kwenye eneo linalojulikana kuwa na malaria na hadi miezi mitatu au hata zaidi baada ya kuondoka kwenye eneo hili, ingawa ni nadra sana kwa dalili kutokea baada ya miezi mitatu.

5) Environments (Mazingira). 

Epuka kuwa ndani ya au karibu na maeneo ambayo mbu huzaliana, kama vile mabwawa, haswa katika mida ya jioni na usiku.

Mara nyingi sana, wasafiri hupata malaria kutokana na kutotumia dawa zao kwa usahihi, aidha kwa sababu wamekosa baadhi ya dozi au dawa hazijatumika kwa muda ulioshauriwa kabla na baada ya kuondoka kwenye eneo lenye malaria.

Dawa za kuzuia kupata malaria kwa kawaida hazina madhara, lakini kwa baadhi ya watu madhara huweza kutokea. Madhara yanayotokea sana kutokana na dawa hizi ni pamoja na kichefuchefu na kuharisha. Baadhi za dawa dhidi ya malaria huweza kuongeza athari ya mionzi ya jua, kwa hiyo ni muhimu kutumia mafuta ya kujikinga dhidi ya mionzi ya jua, wakati kwa wengine wanaweza kupata matatizo ya kulala na maumivu ya kichwa.

Dawa dhidi ya malaria sio wakati wote zina ufanisi wa asilimia 100, ndio maana ni muhimu kuwa na tabia ya kujikinga dhidi ya kung’atwa na mbu ukiwa kwenye eneo lenye malaria. Diethyltoluamide (DEET) ni kati ya dawa ya mbu yenye ufanisi zaidi, na ikiwa dawa hii ina kati ya 10% hadi 30% ya DEET inaweza kutumika kwa watoto wachanga na watoto wenye umri zaidi ya miezi miwili, na wakati wa kunyonyesha.

Kwa watu wazima, viwango vikubwa vya DEET vinaweza kuzuia mbu kwa muda mrefu zaidi. Hata hivyo, viwango vinavyozidi 50% haviongezi kinga ya ziada. 

Tabia nyingine zinazoweza kupunguza hatari ya mtu kung’atwa na mbu ni pamoja na;

1) Kutumia vyandarua wakati wa kulala, haswa vile vyenye dawa za mbu, na kuhakikisha havina matobo.

2) Kujifunika vizuri ikiwa upo nje usiku.

3) Kalala kwenye chumba chenye kiyoyozi, kwa kuwa baridi hupunguza mbu.

4) Kuweka nyavu kwenye milango, madirisha na maeneo mengine ambayo mbu huweza kuingia ndani.

5) Kupulizia dawa ya mbu kabla ya kulala ili kuua mbu wowote walioingia chumbani wakati wa mchana.

6) Kutumia kifaa kinachotumia umeme kuyeyusha kidonge chenye pyrethroid na kutengeneza mvuke chumbani wakati wa usiku.

HITIMISHO:

Kwa msaada wa ushauri, vipimo na tiba ya magonjwa ya afya ya uzazi kwa wanaume na wanawake wasiliana nasi kwa simu namba 0625 305 487.

vipimo