Yajue Mambo 6 Muhimu Kuhusu Kisukari Cha Ujauzito.

Kisukari cha ujauzito ni aina ya kisukari kinachojitokeza wakati wa ujauzito kwa wanawake ambao hawakuwa na kisukari kabla ya kupata ujauzito.

Ugonjwa huu hujulikana kwa kitalaamu kama Gestational diabetes.

Wataalamu wanaeleza kuwa ugonjwa huo unashika kasi duniani na kwamba wanawake wajawazito ambao huongezeka uzito kwa kasi katika miezi 3 ya mwanzo ya ujauzito (first trimester) wao wanakabiliwa na hatari zaidi ya kupata kisukari cha mimba.

Kisukari Cha Ujauzito

Jinsi Kisukari Cha Ujauzito Kinavyotokea:

Kisukari cha ujauzito hutokea kwa sababu mwili wa mwanamke unashindwa kutengeneza insulini ya kutosha au kutumia insulini kwa ufanisi ili kudhibiti viwango vya sukari kwenye damu. 

Wakati wa ujauzito, kondo la uzazi (placenta) hutoa homoni zinazoingilia utendaji kazi wa insulini ya mwili wa mwanamke na kusababisha kiwango cha sukari kwenye damu kupanda juu ya viwango vya kawaida. 

Kisukari cha ujauzito kinaweza kutokea katika kipindi chochote cha ujauzito lakini kwa kawaida, hutokea katika miezi 6 au miezi 9 ya ujauzito ( trimesta ya pili au ya tatu ya mimba).

Baada ya kujifungua, mara nyingi kiwango cha sukari kwenye damu hurudi katika viwango vya kawaida, lakini wakati wa ujauzito ugonjwa huu unaweza kuwa na athari kwa afya ya mama na mtoto aliye tumboni ikiwa hautadhibitiwa vizuri.

Mambo Yanayoongeza Hatari Ya Kupata Kisukari Cha Ujauzito:

Yafuatayo ni baadhi ya mambo yanayoongeza hatari zaidi kwa mwanamke kupata kisukari cha ujauzito ambayo ni pamoja na:

 1. Historia ya kuwa na kisukari katika familia
 2. Uzito au unene kupita kiasi kabla ya ujauzito
 3. Ugonjwa wa vivimbe maji katika ovari  (Polycystic ovarian syndrome)
 4. Historia ya kisukari cha ujauzito
 5. Kuwa na umri wa zaidi ya miaka 35
 6. Kutofanya mazoezi

Dalili Za Kisukari Cha Ujauzito:

Wanawake wengi wenye kisukari cha ujauzito hawapati dalili zinazoonekana. Hata hivyo, ikiwa viwango vya sukari kwenye damu vitabaki juu kwa muda fulani, basi mwanamke anaweza kupata dalili zifuatazo:

 1. Kukojoa mara kwa mara
 2. Kiu kupita kiasi
 3. Njaa iliyokithiri
 4. Uchovu
 5. Maono kuwa hafifu
 6. Kinywa kikavu
 7. Maambukizi ya mara kwa mara kwenye uke

Utambuzi Wa Kisukari Cha Ujauzito:

Kisukari cha ujauzito kawaida hugunduliwa kati ya wiki 24 na 28 za ujauzito kwa kutumia kipimo cha sukari kwenye damu.

Kwa kawaida Kuna vipimo viwili vikuu vinavyotumika kutambua kiwango cha sukari kwenye damu ambavyo ni pamoja na:

1) Kiwango Cha Sukari Kwenye Damu Cha Kufunga.

Hiki ni kipimo kinachopima kiwango cha sukari kwenye damu baada ya kufunga usiku kucha.

Kipimo hiki kinajulikana kwa kitaalamu kama Fasting Plasma Glucose Test (FPGT).

2) Kipimo Cha Ustahimilivu Wa Mwili Kwenye Sukari.

Hiki ni kipimo kinachopima kiwango cha sukari kwenye damu kabla na baada ya kula gramu 70 za sukari.

Kipimo hiki kinajulikana kwa kitaalamu kama Oral Glucose Tolerance Test (OGTT).

Oral Glucose Tolerance Test

Matibabu Ya Kisukari Cha Ujauzito:

Matibabu ya kisukari cha ujauzito yanaweza kuhusisha:

1) Mabadiliko Ya Mitindo Ya Maisha.

Kubadilisha mitindo ya maisha utasaidia katika kutibu ugonjwa wa kisukari cha ujauzito. Mfano: Kula lishe bora wakati wa ujauzito, mazoezi ya mara kwa mara kama vile kutembea kwa kasi, kuogelea, au yoga ya ujauzito, husaidia mwili kutumia insulini kwa ufanisi zaidi.

2) Ufuatiliaji Wa Viwango Vya Sukari Kwenye Damu.

Ufuatiliaji wa mara kwa mara wa viwango vya sukari kwenye damu husaidia kurekebisha mpango wa dawa, chakula na mazoezi ikiwa inahitajika.

Mama mjamzito mwenye kisukari anatakiwa kuwa na kipimo cha sukari nyumbani ambapo atakuwa anajipima na kurekodi viwango vya sukari kwenye damu.

glucometer

3) Dawa.

Ili kudhibiti viwango vya sukari kwenye damu, daktari anaweza kuagiza dawa za kumeza ambazo zitasaidia pia kurekebisha viwango vya sukari kwenye damu kuwa sawa.

Ikiwa lishe na mazoezi vitashindwa kudhibiti viwango vya sukari kwenye damu, sindano za insulini zinaweza kuhitajika pia. Asilimia ndogo tu ya wanawake walio na ugonjwa wa kisukari cha ujauzito wanahitaji insulini ili kurekebisha viwango vya sukari kwenye damu.

Madhara Ya Kisukari Cha Ujauzito:

Yafuatayo ni madhara ya kisukari cha ujauzito kwa mama na mtoto aliye tumboni ambayo ni pamoja na:

A) Kwa Mama Mjamzito.

Wanawake wajawazito waliopata kisukari cha ujauzito huwa kwenye kihatarishi cha muda mfupi cha kupata matatizo ya ujauzito kama vile:

 1. Kifafa cha mimba
 2. Kupata uchungu kabla ya muda (preterm labor)
 3. kujifungua kwa upasuaji
 4. Ongezeko la hatari ya kupata ugonjwa wa kisukari aina ya 2 kwa baadaye maishani
 5. Maji mengi kwenye chupa ya uzazi (polyhydramnios)

B) Kwa Mtoto Aliye Tumboni.

 1. Majeraha wakati wa kuzaliwa, Kuongezeka kwa hatari ya mtoto kupata shoulder dystocia (kukwama kwa bega la mtoto wakati wa kuzaliwa).
 2. Mtoto kuzaliwa amekufa
 3. Mtoto kuzaliwa na uzito mkubwa (Macrosomia)
 4. Kushuka kwa kiwango cha sukari kwenye damu kwa mtoto baada ya kuzaliwa, hii Inaweza kusababisha matatizo ya kupumua.
macrosomic baby

HITIMISHO:

Hata kama kisukari cha ujauzito kitakwisha baada ya kujifungua, wanawake waliowahi kukipata wana hatari kubwa ya kupata ugonjwa wa kisukari aina ya 2 baadaye maishani. Kwa hiyo, kwa mwanamke ni muhimu kuendelea na mitindo bora ya maisha yenye afya baada ya ujauzito, ikiwa ni pamoja na:

 • Kudhibiti uzito 
 • Kula lishe bora
 • Kufanya mazoezi ya mwili mara kwa mara
 • Kupima sukari kwenye damu mara kwa mara

Kwanini mtu mwenye kisukari, kidonda chake hakiponi haraka?

Kuna sababu kuu mbili za kisukari kuchelewesha kupona kwa vidonda:
KWANZA: Viwango vya juu vya sukari kwenye damu.
Viwango vya sukari kwenye damu vikiwa juu, vinaweza kuharibu mishipa ya damu na neva mwilini. Hii inaweza kusababisha mzunguko wa damu kuwa mbovu kwenye viungo, hasa kwenye miguu na vidole. Mzunguko mbovu wa damu unamaanisha kuwa majeraha hayatapata oksijeni na virutubisho vinavyohitajika kupona vizuri.

Vilevile, viwango vya juu vya sukari kwenye damu vinaweza pia kudhoofisha mfumo wa kinga, na hivyo kufanya iwe vigumu kwa mwili kupambana na maambukizi.

PILI: Mfumo dhaifu wa kinga ya mwili.
Kisukari kinaweza kudhoofisha mfumo wa kinga ya mwili, na hivyo kufanya iwe vigumu zaidi kupambana na bakteria ambao husababisha maambukizi kwenye majeraha.

Udhaifu wa kinga unatokana na mambo kadhaa, ikiwa ni pamoja na viwango vya juu vya sukari kwenye damu huweza kuathiri utendaji wa seli nyeupe za damu.

HIVYO: Ukiwa na kisukari, ni muhimu kuwa mwangalifu zaidi kuhusu kuangalia miguu yako. Chunguza kama una michubuko, au vidonda. Hata jeraha ndogo linaweza kuwa tatizo kubwa.