Yajue Mambo 5 Muhimu Kuhusu Shambulio La Moyo.

Maana Ya Shambulio La Moyo:

Shambulio la moyo, ambalo pia hujulikana kwa kitaalamu kama myocardial infarction (MI)/heart attack ni hali ambayo tishu za moyo hukosa kupata oksijeni ya kutosha kutokana na kukata kwa mtiririko wa damu kwenda kwenye moyo.

Hali hii mara nyingi husababishwa na kuziba ghafla kwa mshipa wa damu unaopeleka damu kwenye moyo (coronary artery). Kuziba huku kunaweza kusababishwa na utengenezwaji wa mafuta mbaya (atherosclerotic plaque) kwenye ukuta wa mshipa wa damu, na hivyo kuzuia mtiririko wa damu.

heart attack

Mambo Yanayoongeza Hatari Ya Kupata Shambulio La Moyo:

Kuna mitindo kadhaa ya maisha ambayo inaweza kuongeza hatari ya kupata shambulio la moyo, ikiwemo:

1) Kula Lishe Isiyofaa.

Lishe yenye kiwango kikubwa cha mafuta yasiyo na afya, sukari iliyosindikwa, chumvi nyingi, na kalori nyingi inaweza kuongeza hatari ya magonjwa ya moyo.

Kula vyakula vya afya kama matunda, mboga, protini zenye afya, na nafaka nzima inaweza kusaidia kupunguza hatari hii.

hamburger

2) Kutofanya Mazoezi.

Kuwa na mtindo wa maisha uliobanwa na ukosefu wa mazoezi ya kutosha huchangia unene uliopitiliza na hivyo kuongeza hatari kupata ya shambulio la moyo. Mazoezi ya kawaida husaidia kuimarisha moyo na mishipa ya damu.

kutofanya mazoezi

3) Kuvuta Sigara.

Kuvuta sigara ni moja ya sababu kuu za hatari ya magonjwa ya moyo. Nikotini na kemikali zingine katika sigara husababisha uharibifu kwenye mishipa ya damu (coronary artery) na kusababisha uwezekano mkubwa wa kupata shambulio la moyo.

sigara

4) Kunywa Pombe kupita Kiasi.

Kunywa pombe kupita kiasi kunaweza kuongeza hatari ya kupata shinikizo la juu la damu (hypertension) na kusababisha uwezekano mkubwa wa kupata shambulio la moyo. Matumizi ya pombe kupita kiasi yanaweza kuchangiwa na msongo wa mawazo.

pombe

5) Unene Kupita Kiasi.

Unene uliopitiliza husababisha shinikizo kubwa kwenye moyo na mishipa ya damu (hypertension), na hivyo kuongeza hatari ya kupata shambulio la moyo.

6) Msongo Wa Mawazo. 

Msongo wa mawazo huchangia tabia hatarishi kama vile kunywa pombe kupita kiasi ambayo huongeza shinikizo la damu na kusababisha uwezekano mkubwa wa kupata shambulio la moyo.

Dalili Za Shambulio La Moyo:

Dalili za shambulio la moyo zinaweza kujumuisha:

 1. Maumivu ya kifua ambayo yanaweza kusambaa kwenye mkono wa kushoto, mgongo, shingo, au chini ya taya
 2. Mapigo ya moyo kwenda mbio (palpitations)
 3. Kupumua kwa shida
 4. Kutokwa jasho baridi (cold sweat) jingi
 5. Kuchoka haraka sana (fatigue)
 6. Kizunguzungu
 7. Kichefuchefu
 8. kutapika
 9. Kupoteza fahamu

Matibabu Ya Shambulio La Moyo:

Shambulio la moyo ni tatizo linalohitaji matibabu ya dharua. Lisipotibiwa kwa haraka husababisha kifo katika muda mfupi sana tangu mgonjwa apatwe na tatizo. Matibabu ya tatizo hili hujumuisha:

 1. Kumpa mgonjwa hewa ya oksijeni
 2. Mgonjwa hupewa vidonge vya Aspirini ndogo kuzuia damu kuganda (thrombolytic) kwa ajili ya kuyeyusha damu iliyaganda na hivyo kuzibua mirija midogo ya damu katika moyo iliyozibwa na kuganda huku kwa damu.
 3. Vile vile mgonjwa hupewa dawa za kuweka chini ya ulimi kiitwacho nitrogylycerin (glyceryl trinitrate) ambazo husaidia kutanua mishipa ya damu (vasodilation)
 4. Dawa ya kutuliza maumivu kwa mfano morphine
 5. Dawa ya kuyeyusha mafuta katika mishipa ya damu kama vile clopidogrel
 6. Kuzibua mishipa ya damu inayosambaza damu katika moyo kwa kutumia – Percutaneous coronary intervention (PCI)
 7. Upasuaji (Coronary Artery Bypass Grafting)

Madhara Ya Shambulizi La Moyo:

Yafuatayo ni madhara yanayoweza kutokea ikiwa mgonjwa mwenye shambulio la moyo atashindwa kupata matibabu haraka:

 1. Moyo kushindwa kufanya kazi (heart failure)
 2. Matatizo katika mfumo wa mapigo ya moyo (Atrial fibrillation) ambayo hatimaye hupelekea kifo
 3. Shambulizi la moyo kurudia mara ya pili (recurrent heart attack)
 4. Kifo cha ghafla (sudden death)

HITIMISHO:

Kubadilisha mitindo hii ya maisha kwa kufanya mazoezi mara kwa mara, kula lishe bora, kuacha uvutaji wa sigara, kupunguza unywaji wa pombe, na kushughulikia mbinu za kupunguza msongo wa mawazo kunaweza kupunguza hatari ya kupata shambulio la moyo.

Ni muhimu pia kufanya vipimo vya afya ya moyo mara kwa mara na kushauriana na daktari kuhusu afya yako ya moyo.