Faida Za Maziwa Ya Mama Kwa Mtoto.

Maziwa ya mama ni chakula bora na cha asili kabisa kwa watoto wachanga punde wanapozaliwa.

Prolactin ni homoni muhimu katika kuchochea uzalishaji wa maziwa kwenye tezi za maziwa za mama wakati wa ujauzito na baada ya kujifungua.

Maziwa ya mama ya kwanza kutolewa baada ya kujifungua yanaitwa “colostrum” na yanajulikana kwa kuwa na kinga nyingi na kuwezesha utumbo wa mtoto kufanya kazi vizuri.

Maziwa ya mama yanabadilika kadri mtoto anavyoendelea kunyonya na kukua ili kumtosheleza kwa mahitaji yake ya lishe na kinga ya mwili. Maziwa ya mama ni muhimu sana kwa afya na maendeleo ya mtoto.

kunyonyesha

Leo katika mada yetu ya blogu hii tutazungumzia faida kadhaa za maziwa ya mama kwa mtoto, na vyakula vinavyosaidia kuongeza uzalishaji wa maziwa kwa mama anayenyonyesha.

1) Lishe Kamili.

Maziwa ya mama yana virutubisho vyote muhimu ambavyo mtoto anahitaji kwa ukuaji wake, ikiwa ni pamoja na protini, mafuta, wanga, vitamini, na madini.

2) Kinga Dhidi Ya Magonjwa.

Maziwa ya mama yanajumuisha kinga ya asili ikiwa ni pamoja na kinga za mwili (antibodies)  ambazo husaidia kumlinda mtoto dhidi ya maambukizi mbalimbali kama vile magonjwa ya njia ya hewa, magonjwa ya njia ya utumbo, na hata magonjwa hatari kama vile kuhara.

3) Kupunguza Hatari Ya Mzio.

Watoto wanaonyonyeshwa maziwa ya mama wana uwezekano mdogo wa kuwa na mzio (allergy) wa chakula kulinganisha na wale wanaotumia maziwa ya formula.

4) Kukuza Uhusiano Wa Karibu Kati Ya Mama Na Mtoto.

Mchakato wa kunyonyesha unachochea uzalishaji wa homoni ya oxytocin ambayo husaidia kujenga upendo na uhusiano wa karibu kati ya mama na mtoto.

5) Kupunguza Hatari Ya Unene Na Magonjwa Ya Moyo.

Watoto wanaonyonyeshwa maziwa ya mama wanaweza kuwa na hatari ndogo ya kupata unene na magonjwa ya moyo katika maisha yao ya baadaye.

6) Kuboresha Maendeleo Ya Ubongo Wa Mtoto.

Maziwa ya mama yana virutubisho muhimu kama vile asidi ya arachidonic (ARA) na asidi ya docosahexaenoic (DHA), ambayo inasaidia katika maendeleo ya ubongo wa mtoto.

Vyakula Vinavyoongeza Uzalishaji Wa Maziwa Kwa Mama Anayenyonyesha:

Kuna vyakula kadhaa ambavyo vinaweza kusaidia kuongeza uzalishaji wa maziwa kwa mama anayenyonyesha. Baadhi ya vyakula hivyo ni pamoja na:

1) Matunda na mboga za majani.

Kwa mama anayenyonyesha, mboga za majani na matunda ni sehemu muhimu ya lishe yake kwani zina virutubisho muhimu ambavyo vinaweza kusaidia afya yake na kuongeza uzalishaji wa maziwa. Mfano spinach ina kiwango kikubwa cha folate (asidi ya foliki), chuma, na vitamini A na C hivyo inaweza kusaidia kuongeza kiwango cha hemoglobin na pia inaweza kusaidia katika uzalishaji wa maziwa, matunda kama vile avokado na nazi ni chanzo kizuri cha mafuta yenye afya, ambayo inaweza kusaidia katika kudumisha nishati ya mama na inaweza kuwa na athari nzuri kwa uzalishaji wa maziwa kwa mama anayenyonyesha.

Matunda na mboga za majani

2) Maji.

Kupungua kwa kiwango cha maji mwilini kunaweza kusababisha kupungua kwa uzalishaji wa maziwa. Kwa hivyo, kunywa maji ya kutosha ni muhimu sana kwa mama anayenyonyesha.

maji

3) Vyakula Vya Protini.

Vyakula vya protini kama vile mayai, maharage, nyama, samaki, maziwa ni muhimu sana kwa mama anayenyonyesha kwa sababu vinasaidia katika ujenzi na ukarabati wa tishu za mwili, pamoja na tishu za tezi za maziwa ambazo zinahusika katika uzalishaji wa maziwa kwa mama anayenyonyesha.

protini

4) Nafaka.

Nafaka kama vile ulezi, mtama, mchele wa ‘brown, karanga ni sehemu muhimu ya lishe ya mama anayenyonyesha na inaweza kusaidia katika uzalishaji wa maziwa ya mama. Nafaka ni chanzo kizuri cha wanga wenye nguvu, fiber, protini, vitamini, na madini ambayo ni muhimu kwa afya ya mama na mtoto anayenyonya.

nafaka

 

HITIMISHO:

Kwa ujumla, maziwa ya mama yana faida nyingi kwa afya na ustawi wa mtoto. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), inashauriwa kumpa mtoto maziwa ya mama peke yake angalau kwa miezi sita ya mwanzo ya maisha yake (exclusive breastfeeding) ndipo kuendelea kumpatia vyakula vingine laini kama vile uji wa lishe pamoja na maziwa ya mama.

Lakini pia, kwa uhitaji wa updates, vitabu (e-books) bure kuhusu afya jisajili (subscribe) kupitia email yangu kwa kubonyeza hii link: https://isayafebu.beehiiv.com/subscribe

Ni mimi mwenye kujali afya yako Dr. Isaya Febu, nikutakie siku njema.