Ujue Ugonjwa Wa Virusi Vya Marburg Ulioua Watu 5 Mkoani Kagera.

Ugonjwa wa virusi vya Marburg, au zamani ukijulikana kama homa ya kutokwa na damu inayosababishwa na Virusi vya Marburg ni ugonjwa hatari sana unaoweza kuambukiza binadamu na wanyama wengine. Ugonjwa huu unajulikana kwa kitaalamu kama Marburg Virus Disease (MVD).

Kihistoria milipuko miwili mikubwa iliyotokea kwa wakati mmoja Marburg na Frankfurt huko Ujerumani, na huko Belgrade, Serbia, mnamo mwaka 1967, ilisababisha utambuzi wa kwanza wa ugonjwa huo.

Mlipuko huo ulihusishwa na kazi ya maabara kwa kutumia nyani wa Kiafrika (Cercopithecus aethiops) walioagizwa kutoka Uganda.

Baadae, milipuko na visa vingine vimeripotiwa nchini Angola, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kenya, Afrika Kusini na Uganda.

Mnamo mwaka 2008, visa vingine viwili vya ugonjwa huu viriripotiwa kwa wasafiri huru waliotembelea pango linalokaliwa na makoloni ya popo wa Rousettus nchini Uganda. Lakini hivi karibuni ugonjwa huu umeripotiwa kutokea nchini Tanzania, mkoani kagera na kusababisha vifo vya watu 5.

Soma pia hizi makala:

Kisababishi Cha Ugonjwa Wa Virusi Vya Marburg:

Ugonjwa huu husababishwa na maambukizi ya Virusi vya Marburg vyenye sifa ya RNA kutoka familia ya Filoviridae. Virusi vya ugonjwa huu hupatikana katika familia moja na virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Ebola.

.

Njia Za Maambukizi Za Ugonjwa Wa Virusi Vya Marburg:

Kwa mara ya kwanza, binadamu hupata maambukizi ya virusi vya ugonjwa huu kutoka kwa wanyama hasa popo, kwa kula au kugusa mzoga wake.

Mara mtu anapopata maambukizi hayo kutoka kwa mnyama, maambukizi ya virusi vya ugonjwa huu kati ya binadamu na binadamu mwingine huanza kutokea kupitia mguso wa moja kwa moja.

Virusi vya Marburg vinaweza kupenya na kuingia mwilini kupitia sehemu za wazi kama vile vidonda, au kupitia ngozi laini za sehemu ya macho, midomo na pua kutoka kwenye;

1) Damu au majimaji ya mwili kama vile Mkojo, mate, jasho, choo, matapishi, maziwa na shahawa.

2) Vifaa vilivyoguswa na majimaji kutoka kwenye mwili wa mgonjwa, au mtu aliyefariki kwa ugonjwa huu kama vile matambara, nguo, shuka, viwembe pamoja na sindano.

3) Kwa kushiriki tendo la ndoa kwa namna yoyote na mwanaume aliyeambukizwa ugonjwa huu. Taarifa za kina kuhusu njia hii hazipo wazi sana, lakini inafahamika kuwa virusi vya Marburg huwa na uwezo wa kubaki kwenye korodani za mwanaume kwa siku kadhaa baada ya kupona kama ilivyo kwa virusi vya Ebola.

Kutokana na njia ambayo ugonjwa huu huambukizwa, wahudumu wa afya na watu wengine wanaohudumia wagonjwa na marehemu wenye changamoto hii ikiwemo ndugu huwa kwenye hatari kubwa ya kupatwa na maambukizi.

Dalili Za Ugonjwa Wa Virusi Vya Marburg:

Ugonjwa unaosababishwa na virusi vya Marburg huanza ghafla kwa homa kali, maumivu makali ya kichwa pamoja na maumivu ya misuli. Dalili zingine ni pamoja na;

1) Kuhara.

2) Maumivu makali ya tumbo.

3) Kichefuchefu na kutapika.

4) Maumivu ya kifua.

5) Kuwasha kwa koo.

6) Upele usiowasha.

Wagonjwa wengi hupata udhihirisho mkubwa wa kutokwa na damu ndani ya siku 7 kwenye sehemu mbalimbali za mwili ikiwemo machoni, kwenye ngozi, fizi, macho, uke pamoja na kujisaidia choo na mkojo wenye damu.

Mwonekano wa wagonjwa katika awamu hii hufafanuliwa kuwa huonesha “sifa zinazofana na mzimu” huku macho yakirudi ndani, uso ukikosa nuru na mwili mzima ukiwa na uchovu mkubwa.

Katika hatua mbaya za ugonjwa, homa huwa kubwa kiasi cha kuathiri mfumo wa kati a fahamu hivyo kusababisha kuchanganyikiwa, kuweweseka na ukorofi. Kwa wanaume, korodani zinaweza kuvimba.

Hatua ya mwisho inayoelekea kifo kawaida hutokea kati ya siku 8 na 9 baada kuambukizwa. Husababishwa na upotevu wa damu nyingi, kufeli kwa ini pamoja na kusimama kufanya kazi kwa viungo muhimu vya mwili.

Uchunguzi Wa Maabara Wa Ugonjwa Wa Virusi Vya Marburg:

Ni ngumu kutambua kirahisi pamoja na kutofautisha maambukizi ya ugonjwa huu na magonjwa mengine ya kuambukiza mfano Malaria, homa ya matumbo (Typhoid), homa ya uti wa mgongo pamoja na homa zingine zinazosababishwa na virusi.

Njia zifuatazo zinaweza kufanyika kwenye maabara ili kuthibitisha uwepo wa ugonjwa huu;

1) Antibody enzyme-linked immunosorbent assay (ELISA).

2) Antigen detection tests.

3) Serum neutralization tests.

4) Reverse-transcriptase polymerase chain reaction (RT-PCR) assay.

5) Virus isolation by cell culture.

Matibabu Ya Ugonjwa Wa Virusi Vya Marburg:

Ugonjwa huu hauna tiba ya moja kwa moja isipokuwa kushughulikia dalili zinazoonekana kwa wakati huo.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), ugonjwa wa virusi vya Marburg huwa na hadi 88% ya uwezekano wa kusababisha kifo.

Jinsi Ya Kujikinga Na Ugonjwa Wa Virusi Vya Marburg:

Pamoja na kuonekana mara chache sana kwa binadamu, ugonjwa huu unaweza kuambukiza kirahisi hasa kwa watumishi wa afya wanaohudumia wagonjwa pamoja na ndugu wa karibu wanaoishi na kutoa huduma kwa mtu mwenye ugonjwa huu.

Hivyo, namna nzuri ya kujikinga ni kuepuka ulaji/kukaa karibu na wanyama waliopo kwenye kundi la primates (Wanyama jamii ya nyani na sokwe) na popo ambao ndio hubeba sifa kubwa ya kuishi na virusi vya Marburg.

Aidha, watu wanaotoa huduma kwa mgonjwa wanapaswa kuvaa vifaa maalumu vya kujikinga mfano gloves, gauni maalumu na barakoa, kumtenga mgonjwa kwenye eneo lililodhibitiwa pamoja na kutakasa au kuangamiza kikamilifu masalia ya vifaa alivyotumia mgonjwa vyenye sifa ya kubeba vimelea ya ugonjwa.

jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa marburg

HITIMISHO:

Kwa ushauri na tiba ya magonjwa ya afya ya uzazi wasiliana nasi kwa simu namba 0625 305 487.