Ijue Saratani Ya Matiti Kwa Wanawake Na Jinsi Ya Kujikinga.

Saratani ya titi ni saratani ambayo hutokea kwenye titi ambalo kwa kawaida lina sehemu ya kutengeneza maziwa ijulikanayo kama lobules na aina fulani ya mishipa inayounganisha hizi lobules na chuchu za titi. Saratani ya titi hujulikana kwa kitaalamu kama Breast cancer.

Sehemu kubwa  ya matiti iliyobakia inajumuisha mafuta na tishu ambazo kitaalamu hujulikana kama connective and lymphatic tissues. Saratani ya matiti inayotokea kwenye lobules huitwa Lobular Carcinoma In Situ (LCIS) na ile inayotokea kwenye milk ducts huitwa Ductal Carcinoma In Situ (DCIS).

Baadhi ya saratani ya matiti zinaongeza ukubwa kutokana na kuwa na vishikizi aina ya receptors zinazojulikana kama estrogen receptors kwenye seli zao ambazo husababisha ukuaji wa saratani ya matiti.

Kuna wanawake wengine wana viashiria vya asili vinavyojulikana kama HER2 positive breast cancer ambavyo husaidia seli kuongezeka, kugawanyika na kujirekebisha pale zinapoharibika. Kiashiria hiki kinaaminika ndicho kinachosababisha wanawake hawa kuwa na saratani ya matiti yenye madhara zaidi, pia kuwa na uwezekano mkubwa wa kujirudia kwa saratani baada ya tiba tofauti na wale ambao hawana kiashiria hiki cha HRE2.

Mambo Yanayochangia Wanawake Kupata Saratani Ya Matiti

Yafuatayo ni mambo yanayomuweka mwanamke katika hatari ya kupata saratani ya titi ambayo ni pamoja na;

1) Jinsia Ya Kike.

Ingawa, saratani ya matiti huweza kutokea kwa wote wanawake na wanaume, imeonekana kuwa wanawake ni waathirika wakubwa zaidi wa saratani hii ikilinganishwa na wanaume.

2) Umri.

Uwezekano wa kupata saratani hii huendana na umri wa mtu. Kadiri umri wa mtu unavyoongezeka ndivyo pia uwezekano wa kupata saratani hii unavyozidi kuwa mkubwa. Wanawake walio na umri wa kuanzia miaka 50 wapo kwenye hatari kubwa (mara 2 au 3 zaidi) kuliko walio na umri wa miaka 45.

3) Uasili Wa Mtu (Ethnicity).

Saratani ya matiti hutokea zaidi kwa wanawake wazungu kuliko wanawake wa kiafrika au wenye asili ya afrika (weusi).

4) Uzazi.

Wanawake ambao hawajazaa, Kutonyonyesha kabisa au kunyonyesha kwa muda mfupi wapo kwenye hatari kubwa ya kupata saratani ya matiti. Wanawake wanaopata ujauzito kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30 nao pia wapo kwenye hatari kubwa ya kupata saratani hii.

5) Historia Ya Saratani Ya Matiti Katika Familia.

Wanawake walio katika familia zenye historia ya ugonjwa huu wana uwezekano mkubwa wa kupata saratani ya matiti ukilinganisha na wale ambao hawana historia ya ugonjwa huu katika familia zao. Kwa mwanamke aliye na ndugu (mama, dada au mtoto) ambaye aliwahi kupata saratani hii kabla ya umri wa miaka 50, uwezekano wa mwanamke huyu kupata ugonjwa huu ni mara mbili ya yule ambaye hana historia hii.

6) Kuanza Hedhi Katika Umri Mdogo.

Wanawake wanaovunja ungo (kupata hedhi) kabla ya umri wa miaka 12 wapo kwenye hatari zaidi ya kupata ugonjwa huu.

7) Historia Ya Saratani Ya Matiti.

Wanawake ambao wamewahi kupata ugonjwa huu kwenye titi la upande mmoja hapo kabla, wana uwezekano mkubwa wa kupata tena saratani kwenye titi la upande mwingine hapo siku za usoni.

8) Unene Kupita Kiasi.

Tafiti nyingine zimeonesha kuwa, wanawake wanene wana uwezekano mkubwa wa kupata saratani ya matiti ukilinganisha na wale wa uzito mdogo au wa kati.

9) Uvutaji Wa Sigara.

Kuna matokeo yenye kukinzana kuhusu uhusiano wa uvutaji wa sigara na hatari ya kupata saratani ya matiti. Wakati baadhi ya tafiti zinaonesha uhusiano wa karibu kati ya uvutaji wa sigara na uwezekano wa kupata saratani ya matiti, tafiti nyingine zinaonesha majibu yenye kutofautiana kuhusu uhusiano wa uvutaji wa sigara na saratani ya matiti. Hata hivyo, kwa ujumla wanawake wanaojizuia kuvuta sigara wanakuwa na afya njema zaidi kuliko wale wanaovuta sigara.

10) Utumiaji Wa Pombe Kupita Kiasi.

Imeonekana kuwa wanawake wanaokunywa pombe zaidi ya chupa moja kwa siku wana uwezekano wa kupata saratani ya matiti kwa asilimia zaidi ya ishirini.

11) Matumizi Ya Dawa Za Kupanga Uzazi.

Kuna ushahidi kuwa saratani ya matiti ina uhusiano na matumizi ya muda mrefu ya vidonge vya kupanga uzazi.

12) Kuwepo Kwa Kiwango Kikubwa Cha Homoni Mwilini.

Kwa wale wanaotumia tiba ya homoni inayojulikana kama hormone replacement therapy, kwa sababu nyingine yeyote ile, au wale wenye kiwango kikubwa cha homoni kama vile oestrogen na progesterone mwilini mwao wapo kwenye hatari zaidi ya kuugua saratani ya matiti.

Soma pia hii makala: Mambo 4 Usiyo yajua Kuhusu Mvurugiko Wa Homoni Kwa Wanawake.

13) Kuwa Na Matiti Makubwa.

Wanawake wenye matiti makubwa (dense breast tissue) wana uwezekano mkubwa wa kupata saratani ya matiti. Hali hii hutokana na ukweli kuwa wakati mwingine ni vigumu sana kwa madaktari kutambua kama wana saratani au la kutokana na ukubwa wa matiti yao.

14) Historia Ya Tiba Ya Mionzi.

Wanawake ambao wamewahi kupata tiba ya mionzi hususani wakati wa ukuaji wa matiti, wapo kwenye hatari zaidi ya kupata ugonjwa huu. Hali hii husababishwa na ukweli kuwa mojawapo ya madhara ya mionzi ni kuongeza uwezekano wa kupata saratani ya aina yoyote.

15) Ulaji Wa Vyakula Vyenye Mafuta Mengi.

Tafiti zinaonesha kuwa, wanawake wanaopendelea kula vyakula vyenye mafuta mengi wapo kwenye hatari zaidi ya kupata ugonjwa huu.

16) Kukoma Hedhi Katika Umri Mkubwa.

Kwa kawaida wanawake huacha kupata hedhi wafikapo miaka 45-55, hali ambayo kitaalamu hujulikana kama menopause. Wanawake wanaochelewa kuacha kupata hedhi, kwa mfano wale wanaoendelea kupata hedhi wakiwa na zaidi ya miaka 45, wapo kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata saratani ya matiti.

Soma pia hii makala: Ukomo Wa Hedhi Kwa Wanawake Na Tiba Yake.

Je Saratani Ya Matiti Husambaa Vipi?

Kwa kawaida saratani ya matiti husambaa kwa njia tatu zifuatazo;

1) Kupitia Tishu.

Saratani ya matiti husambaa kwenye tishu za kawaida ambazo zimezunguka eneo la saratani.

2) Kupitia Mfumo Wa Limfu (Lymphatic System).

Saratani ya matiti huvamia mfumo wa lymph na kufuata mishipa yake hadi sehemu nyingine za mwili.

3) Kupitia Damu.

Saratani ya matiti inaweza kusambaa kupitia damu kwa kuvamia mishipa ya damu ya vena na capillaries (veins and capillaries) na kusafiri kutumia damu hadi sehemu nyingine za mwili.

Dalili Za Saratani Ya Matiti:

Saratani hii kwa kawaida haina dalili katika hatua za mwanzo. Wanawake katika hatua za mwanzo za ugonjwa huu hawana maumivu au dalili nyingine zozote. Uchunguzi wa awali ndio utakao wezesha kuugundua ugonjwa huu katika hatua hiyo, mabadiliko yaletwayo na saratani ya matiti ni pamoja na;

1) Kivimbe katika titi au kwenye makwapa.

2) Mabadiliko ya umbo na ukubwa wa titi.

3) Kutokwa na majimaji au damu katika chuchu ama chuchu kuingia ndani ya ziwa.

4) Mabadiliko katika rangi ya ngozi ya titi (kuonekana kama sehemu ya nje ya ganda la chungwa).

Vipimo Vya Saratani Ya Matiti:

Pamoja na mgonjwa kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu na wataalamu wa afya kuweza kutambua uwepo wa tatizo hili, anaweza pia kufanyiwa vipimo vifuatavyo ili kusaidia kutambua ugonjwa huu;

1) X-Ray Ya Matiti.

Kipimo hiki pia hujulikana kwa kitaalamu kama Mammogram ambacho kina uwezo wa kuonyesha ulipo uvimbe kwenye matiti.

2) Breast Ultrasound.

Kipimo hiki kinasaidia kutambua iwapo uvimbe uliopo ndani ya matiti umejaa maji ama la ili ufanyiwe vipimo zaidi.

breast ultrasound

3) Fine Needle Aspiration And Cytology (FNAC).

Kipimo hiki hufanywa kwa kuchukua sehemu ya uvimbe (Aspiration) kwa kutumia aina fulani ya sindano (fine needle) na kisha kupeleka maabara sehemu iliyochukuliwa kwa ajili ya kutafitiwa zaidi ili kugundua uwepo wa hii saratani.

4) Breast Biopsy. 

Kipimo hiki kinausisha upasuaji mdogo unaofanywa kwenye titi lililoathirika kwa ajili ya kuchukua sehemu ya titi (surgical biopsy) na kisha kuipeleka maabara kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

5) Sentinel Lymph Node Biopsy (SLNB).

Kipimo hiki hufanywa ili kujua kama saratani imesambaa hadi kwenye tezi.

sentinel lymph nodes biopsy

Tiba Ya Saratani Ya Matiti:

1) Upasuaji.

Lengo kuu la upasuaji ni kuondoa saratani kwenye titi pamoja na tezi (lymph nodes). Zipo aina kadhaa za upasuaji unaoweza kufanywa kwenye titi lililogundulika kuwa na saratani. Aina hizo ni pamoja na;

a) Lumpectomy.

Huu ni upasuaji unaofanywa kuondoa sehemu ya saratani pamoja na sehemu ya titi ambayo haijaathirika kwa saratani. Hii hufuatiwa na tiba ya mionzi (radiotherapy) kwa muda wa kati ya wiki 6 au 7. Mgonjwa anayefanyiwa aina hii ya upasuaji anakuwa na uwezekano wa kuishi muda mrefu sawa na anayefanyiwa upasuaji wa kuondoa titi lote lililoathirika.

lumpectomy

b) Simple/Total mastectomy.

 Hii ni aina ya upasuaji unaohusisha uondoaji wa titi lote lililoathirika kwa ugonjwa wa saratani.

c) Modified radical mastectomy.

Hii ni aina ya upasuaji unaohusisha uondoaji wa titi lote lililoathirika pamoja na kundi lote la tezi (lymph nodes) chini ya mkono (axilla) bila kuhusisha uondoaji wa misuli ya kifua.

Kumbuka: Kwa ujumla, lumpectomy na mastectomy, zote zinahusisha uondoaji wa kundi la tezi ambalo lipo karibu na uvimbe wa saratani (regional lymph nodes).

2) Tiba Ya Mionzi.

Mionzi inaweza kutumika kuharibu seli za saratani zilizobaki kwenye matiti, kifua (chest wall), au/na eneo la chini ya mkono mara baada ya upasuaji kufanyika. Mionzi pia inaweza kutumika kupunguza ukubwa wa uvimbe wa saratani kabla ya kufanyika kwa upasuaji.

3) Tiba Ya Saratani Kwa Njia Ya Dawa (Systemic Therapy).

Tiba ya aina hii inahusisha matumizi ya kemikali maalum za kutibu saratani (chemotherapy) pamoja na matumizi ya homoni (hormonal therapy).

Tiba kwa kutumia homoni (Adjuvant hormonal therapy) hutumika ili kuua seli za saratani ambazo hazikugundulika hapo awali na ambazo yawezekana zimesambaa sehemu nyingine za mwili. Tiba hii hutolewa baada ya kufanyika kwa upasuaji wa kuondoa uvimbe wa saratani.

Aina hii ya tiba hutegemea na ukubwa wa uvimbe, matokeo ya vipimo vya kimaabara vya saratani (histological results), na iwapo saratani imesambaa hadi kwenye tezi za kwenye kwapa la mgonjwa ama la. Tiba hii pia yaweza kutolewa kwa mgonjwa ambaye saratani imeshasambaa mwilini kwake kwa muda mrefu, na ambaye hawezi kufanyiwa upasuaji. Baadhi ya kemikali zinazotumika kutibu saratani ya matiti ni cyclophosphamide, methotrexate, na fluorouracil. Kwa kawaida dawa hizi hutolewa kwa kujumuisha dawa 2 au 3 kwa wakati mmoja.

Kumbuka:

kama ilivyo kwa dawa nyingine za kutibu magonjwa mengine tofauti na saratani, kemikali (dawa) hizi za saratani pia zina madhara mbalimbali kwa mtumiaji. Madhara haya huletwa na ukweli kuwa, pamoja na kuwa kazi kuu ya kemikali hizi ni kuua seli zenye saratani, hutokea pia kuua na kuathiri seli za kawaida yaani zisizo na ugonjwa wa saratani kama vile seli zilizo kwenye mdomo, nywele, pua, kucha, utumbo na hata sehemu za siri za mwanamke.

Hata hivyo tofauti na seli za saratani, seli za kawaida huwa na uwezo wa kujizaa tena, kukua na kurudi katika hali yake ya kawaida wakati zile za saratani hazina uwezo huo. Madhara ya dawa hutofautiana kati ya mgonjwa mmoja na mwingine.

Jinsi Ya Kukikinga Na Saratani Ya Matiti:

Mwanamke unashauriwa kufanya mambo yafuatayo ili kujikinga na saratani ya matiti;

1) Kujichunguza mwenyewe mara kwa mara kwa mara.

2) Uchunguzi wa kitabibu wa matiti kila mwaka.

3) Uchunguzi wa matiti kwa njia ya mashine ya mionzi (mara moja kwa mwaka kwa wenye miaka zaidi ya 40).

4) Wanawake wote wenye umri kuanzia miaka 21 wajichunguze matiti yao siku ya 5-7 baada ya kumaliza hedhi mbele ya kioo.

Hatua  5 Rahisi Za Kujichunguza Matiti:

  • Jiangalie katika kioo ukiwa umesimama wima na umeweka mikono kiunoni.
  • Angalia kama kuna mabadiliko katika umbo au rangi ya ngozi ya titi na kama       

          AU

  • Ukiwa umesimama au umelala chali tumia mkono pamoja na kipaji cha vidole vya mkono wa kulia kuchunguza titi la kushoto na mkono wa kushoto kuchunguza titi la kulia kwa njia ya mzunguko.
  • Kwa upole kamua chuchu ya kila titi na chunguza kama kuna ute ulio changanyika na damu.
  • Muone daktari kama kuna uvimbe au ute ulio changanyika na damu au hali yoyote ulioiona wakati wa kujichunguza.

HITIMISHO:

Kwa ushauri na tiba ya magonjwa ya afya ya uzazi wasiliana nasi kwa simu namba 0625 305 487.

“We care for your health. “