Kushindwa kusimamisha uume hali inayojulikana kwa kitaalamu kama erectile dysfunction (ED) ni hali ambapo mwanaume anapata ugumu wa kusimamisha uume au kuuweka uume ukiwa umesimama vya kutosha kwa ajili ya kufanya tendo la ndoa.
Tatizo hili linaweza kutokea mara kwa mara au kuwa la muda mrefu na huathiri wanaume wa rika zote, ingawa kwa viwango tofauti. Wanaume vijana huathirika zaidi kwa sababu za kisaikolojia na mtindo wa maisha, wakati wanaume wazee huathirika zaidi kwa sababu za kifiziolojia (kimwili) kama vile magonjwa na mabadiliko ya homoni.
Leo katika mada yetu ya blogu hii tutazungumzia sababu zinazochangia mwanaume kushindwa kusimamisha uume. Ungana nami katika kuchambua sababu hizi.
A) Sababu Za Kifiziolojia:
1) Magonjwa Ya Moyo.
Matatizo ya mishipa ya damu, kama vile ugonjwa wa moyo au mishipa kuziba, yanaweza kupunguza mtiririko wa damu kwenda kwenye uume, hivyo kusababisha tatizo la kusimamisha uume.
2) Shinikizo La Juu La Damu (Hypertension).
Shinikizo la juu la damu huathiri mtiririko wa damu kwenda kwenye uume, na kuzuia au kupunguza uwezo wa kusimamisha uume.
3) Kisukari (Diabetes).
Kisukari kinaweza kuharibu neva na mishipa ya damu, hali inayoweza kuathiri mtiririko wa damu kwenye uume na uwezo wa kusimamisha uume.
4) Unene Kupita Kiasi.
Uzito wa kupita kiasi unahusishwa na tatizo la nguvu za kiume kutokana na athari zake kwenye mtiririko wa damu, uzalishaji wa homoni (testosteroni), na viwango vya afya kwa ujumla.
5) Matatizo Ya Homoni.
Upungufu wa homoni ya kiume ya testosteroni unaweza kuathiri hamu ya ngono na uwezo wa kusimamisha uume.
6) Magonjwa Ya Tezi Dume (Prostate Problems).
Upasuaji au magonjwa ya tezi dume kama vile saratani ya tezi dume, prostatitis yanaweza kuathiri mishipa na misuli inayosaidia kusimamisha uume.
7) Magonjwa Ya Mfumo Wa Neva (Neurological Conditions).
Magonjwa kama vile kiharusi, multiple sclerosis, au majeraha ya uti wa mgongo yanaweza kuathiri mawasiliano kati ya ubongo na uume, na hivyo kuathiri uwezo wa kusimamisha uume.
B) Sababu Za Kisaikolojia:
1) Msongo Wa Mawazo.
Msongo wa mawazo kutokana na kazi, familia, au matatizo ya kifedha unaweza kuathiri uwezo wa kusimamisha uume.
2) Hofu Ya Kushindwa (Sexual Performance Anxiety).
Wanaume wanaowaza sana kuhusu kutofanya vizuri kitandani (kushindwa kumfurahisha mwenzi) wanaweza kupata shida ya kusimamisha uume kutokana na wasiwasi.
3) Matatizo Ya Mahusiano.
Matatizo ya mahusiano, kama vile ugomvi au ukosefu wa mawasiliano mazuri na mwenzi kunaweza kuathiri kisaikolojia na kusababisha kushindwa kusimamisha uume.
5) Kujichua Kupita Kiasi Au Utumiaji Wa Ponografia.
Kwa baadhi ya watu, tabia ya kujichua kupita kiasi au kutegemea ponografia inaweza kuathiri uwezo wa kuwa na kusimama uume wakati wa tendo halisi la ndoa.
C) Mtindo Wa Maisha:
1) Uvutaji Wa Sigara.
Nikotini iliyopo kwenye sigara husababisha mishipa ya damu kuwa finyu (vasoconstriction), hivyo kuzuia mtiririko wa damu. Uume unahitaji mtiririko mzuri wa damu ili kusimama, hivyo mabadiliko haya yanapunguza uwezo wa mwanaume kupata ereksheni.
Uvutaji wa sigara unaweza kuharibu kuta za mishipa ya damu, na hivyo kupunguza ufanisi wa mtiririko wa damu mwilini. Uharibifu huu unachangia atherosclerosis, ambapo mafuta na kolesteroli hujilimbikiza kwenye kuta za mishipa ya damu, na kuzuia mzunguko wa damu.
Uvutaji wa sigara umehusishwa na kupungua kwa kiwango cha testosterone, homoni muhimu katika kudumisha hamu ya ngono na uwezo wa kusimamisha uume.
2) Unywaji Wa Pombe Kupita Kiasi.
Unywaji wa pombe kupita kiasi unaweza kusababisha kuongezeka kwa shinikizo la damu (hypertension) na matatizo ya mzunguko wa damu. Hii inaweza kuathiri mtiririko wa damu kwenye uume na kupelekea kushindwa kusimamisha uume.
3) Madawa Ya Kulevya.
Matumizi ya dawa za kulevya kama vile bangi, kokeini, na heroin yanaweza kuharibu mfumo wa neva na kupunguza uwezo wa kusimamisha uume.
4) Kutofanya Mazoezi.
Ukosefu wa mazoezi unaweza kusababisha unene kupita kiasi hali ambayo inaweza kupelekea matatizo ya mzunguko wa damu kama vile shinikizo la juu la damu na kuathiri uwezo wa kusimamisha kiume.
D) Matumizi Ya Dawa:
Baadhi ya dawa kama zile za kutibu shinikizo la juu la damu (antihypertensive drugs), dawa za sonona (antidepressants), na dawa za matibabu ya saratani zinaweza kuathiri uwezo wa kusimamisha uume kama matokeo tarajiwa (side effects).
E) Umri:
Utafiti unaonyesha kuwa uwezekano wa kukumbwa na tatizo hili huongezeka kadri mwanaume anavyozeeka (Ingawa si kila mwanaume mzee hupata tatizo hili), hii ni kutokana na kupungua kwa uzalishaji wa kiwango cha homoni ya kiume, testosterone, jambo ambalo linaweza kupunguza hamu ya tendo la ndoa na uwezo wa kusimamisha uume.
HITIMISHO:
Ikiwa unakabiliwa na tatizo la kusimamisha uume, ni muhimu kumwona daktari ili uchunguzi wa kina ufanywe na sababu halisi kutambuliwa. Matibabu yanatofautiana kulingana na sababu, na yanaweza kujumuisha dawa, ushauri nasaha, mabadiliko ya mtindo wa maisha, au upasuaji ikiwa ni lazima.
Leave a Reply