Ugonjwa wa kisonono ni maambukizi ya bakteria wanaosambazwa kwa njia ya ngono na bakteria anayeitwa Neisseria gonorrhoeae.
Bakteria huyu hukua kwenye maeneo yenye joto na yenye unyevu, hii ni pamoja na kwenye mrija unaotoa mkojo mwilini (urethra). Kwa wanawake, bakteria huyu pia hupatikana kwenye via vya uzazi, hii hujumuisha mirija ya uzazi (fallopian tubes), mji wa mimba (uterus), na mlango wa mji wa mimba (cervix). Bakteria hawa vilevile wanaweza kukua hata kwenye macho.
Ugonjwa wa kisonono pia hujulikana kama ‘the clap’.
Ugonjwa wa kisonono unapatikana dunia nzima, unaathiri jinsi zote mbili, hasa vijana na watu wazima wanaojihusisha na ngono kwa wingi. Ugonjwa huu unawapata zaidi watu wenye uchumi duni (poor socio-economic status). Katika nchi nyingi zilizo endelea (developed countries) kiwango cha maambukizi kimepungua katika miongo hii miwili iliyopita.
Njia Zinazopelekea Kupata Ugonjwa Wa Kisonono:
Zifuatazo ni baadhi ya njia zinazopelekea mtu kupata maambukizi ya kisonono;
1) Kufanya ngono isiyo salama na mtu mwenye maambukizi ya ugonjwa huu hasa kupitia mdomo (oral sex), mkundu (anal sex).
2) Kupewa damu isiyo salama yenye maambukizi ya bakteria wanaosababisha ugonjwa huu.
3) Mwanamke mjamzito mwenye ugonjwa huu anaweza kumuambukiza mtoto wake wakati wa kujifungua. Mtoto aliyezaliwa anaweza kupata maambukizi ya macho ambayo hujulikana kama Gonococcal ophthalmia neonatorum na anaweza kuwa kipofu endapo atashindwa kupata matibabu mapema.
Picha Za Kisonono:
Watu Waliopo Kwenye Hatari Ya Kupata Ugonjwa Wa Kisonono:
Kuna uwezekano mkubwa wa kupata maambukizi ya kisonono kama;
1) Una washirika wengi wa ngono (multiple sexual partners).
2) Una mpenzi mwenye historia ya kupata magonjwa ya zinaa.
3) Hautumii kondomu wakati wa ngono.
4) Wewe ni mwanaume unayefanya ngono na mwanaume mwingine.
5) Unatumia madawa ya kulevya.
Dalili Za Ugonjwa Wa Kisonono:
Dalili za kisonono huanza kuonekana siku 2 – 5 baada ya kuambukizwa. Hata hivyo, kwa wanaume, dalili zinaweza kuchelewa mpaka mwezi. Watu wengine hawapati dalili kabisa. Wanaweza kuwa hawajui kabisa kwamba wameambukizwa ugonjwa huu, na kwa sababu hiyo hawatafuti matibabu. Hii huongeza uwezekano wa kupata matatizo na hatari ya kuambukiza wengine.
Dalili Za Kisonono Kwa Wanaume Ni Pamoja Na;
1) Maumivu wakati wa kukojoa.
2) Kukojoa mara kwa mara au kushindwa kuzuia mkojo (mgonjwa akibanwa mkojo, ni lazima akojoe haraka sana).
3) Kutoa uchafu kwenye uume (uchafu unaweza kuwa mweupe, njano, au rangi ya kijani).
4) Wekundu au kuvimba kwa urethra (huu ni mrija unaobeba mkojo kutoka kwenye kibofu kwenda nje ya mwili).
5) Kuvimba na kuuma kwa korodani.
Dalili Za Kisonono Kwa Wanawake Ni Pamoja Na;
1) Kutoa uchafu ukeni.
2) Maumivu wakati wa kukojoa.
3) Kukojoa mara kwa mara/mara nyingi.
4) Maumivu kwenye koo.
5) Maumivu wakati wa ngono.
6) Maumivu makali kwenye sehemu ya chini ya tumbo (kama maambukizi yataenea mpaka kwenye mirija ya uzazi).
7) Homa (Kama maambukizi yataenea mpaka kwenye mirija ya uzazi au eneo zima la tumbo).
Tahadhari: Kama una dalili za kisonono unapaswa kumuona daktari mapema iwezekanavyo.
Soma pia hizi makala:
- Mambo Muhimu Usiyo yajua Kuhusu Ugonjwa Wa Kaswende.
- Mambo 7 Muhimu Usiyo yajua Kuhusu Ugonjwa Wa Pangusa.
Vipimo Vya Maabara Vya Ugonjwa Wa Kisonono:
Ugonjwa wa kisonono hutambuliwa baada ya sampuli ya tishu au uchafu unaotoka ukeni/ kwenye uume kutiwa rangi (gram stain) na kisha kuchunguzwa chini ya darubini. Japo njia hii ya utambuzi ni ya haraka, lakini si ya kuaminika sana. Sampuli kwa ajili ya gram stain huchukuliwa: Kwenye mlango wa kizazi cha mwanamke, uchafu unaotoka kwenye uume, majimaji kutoka kwenye maungio ya mwili-joints.
Culture (sampuli huchukuliwa na kupandwa kwenye sahani maalumu ya maabara, njia hii huwaruhusu bakteria kukua – utambuzi hufanyika kwa urahisi wakikua ), njia hii ni ya kuaminika zaidi. Sampuli kwa ajili ya culture huchukuliwa kwenye: Kizazi na mlango wa kizazi cha mwanamke, uchafu unaotoka kwenye uume, kooni kwa wanaume na wanawake, njia ya haja kubwa kwa wanaume na wanawake, majimaji kutoka kwenye maungio ya mwili- joints, damu.
Matokeo ya awali ya culture hutoka baada ya masaa 24 na matokeo thabiti ndani ya masaa 72.
Matibabu Ya Ugonjwa Wa Kisonono:
Kuna malengo mawili katika kutibu ugonjwa wa kisonono. Lengo la kwanza ni kutibu maambukizi ya mgonjwa. Lengo la pili ni kuwatafuta na kuwapima watu wengine wote ambao wamefanya ngono na mgonjwa, ili kuwatibu na kuzuia maambukizi zaidi. Usijitibu mwenyewe bila kuonwa na daktari kwanza. Mtoa huduma wa afya ataamua ni matibabu gani yaliyo bora zaidi. Matibabu yanayopendekezwa ni pamoja na;
Dawa Za Kutibu Kisonono:
a) Sindano moja ya ceftriaxone 125 mg au kumeza dozi moja ya cefixime 400mg.
b) Dozi moja ya Azithromycin 2g inaweza kutumika kwa watu wenye mzio (allergy) wa ceftriaxone, cefixime, au penicillin.
Kumbuka: Mgonjwa anapaswa kurejea hospitalini baada ya siku 7. Vipimo vitafanywa tena, kuhakikisha maambukizi yamekwisha. Watu wote waliofanya ngono na mgonjwa wanapaswa kutafutwa ili wapimwe na kutibiwa. Hii hupunguza kuenea kwa kisonono.
Madhara Ya Ugonjwa Wa Kisonono:
Kwa kawaida, maambukizi ya kisonono ambayo hayajaenea kwenye damu au maeneo mengine hupona vyema baada ya kutumia antibiotiki. Kisonono ambayo imeenea ni tatizo kubwa, lakini pia hupona baada ya matibabu.
Ikiwa mgonjwa wa kisonono hatashindwa kupata matibabu haraka basi madhara yafuatayo yanaweza kutokea ambayo ni pamoja na;
A) Madhara Kwa Wanaume:
1) Mgonjwa anaweza kupata makovu yanayoweza kusababisha kuziba kwa njia ya mkojo (urethra)- hii inaweza kusababisha shida wakati wa kukojoa.
2) Jipu (usaha kwenye urethra).
3) Matatizo wakati wa kukojoa.
4) Maambukizi kwenye njia ya mkojo (U.T.I).
5) Kushindwa kwa figo kufanya kazi (kidney failure).
B) Madhara Kwa Wanawake:
1) Kuharibika kwa mirija ya uzazi (salpingitis ) – hii inaweza kusababisha ashindwe kupata mimba au kusababisha mimba itungwe nje ya mji wa mimba (ectopic pregnancy).
2) Ugumba (kukosa uwezo wa kuwa mjamzito).
3) Maumivu wakati wa ngono (dyspareunia).
4) Wanawake wajawazito wenye kisonono wanaweza kuwaambukiza watoto wao wakiwa tumboni au wakati wa kuzaliwa.
Jinsi Ya Kuzuia Ugonjwa Wa Kisonono:
Zifuatazo ni njia za kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa kisonono ambazo ni pamoja na;
1) Toa matibabu kwa wagonjwa.
2) Tibu wapenzi wa wagonjwa pia.
3) Toa elimu kuhusu ngono salama (health education).
4) Dhibiti magonjwa ya ngono kwa wanaouza miili (Malaya) kwa vipimo vya kila mwezi na kutoa matibabu, kuwagawia kondomu.
5) Kuchunguza wanawake wajawazito na kutoa matibabu mapema ili kuzuia kuambukiza mtoto.
6) Kupaka dawa aina 1% tetracycline kwenye macho ya mtoto baada tu ya kuzaliwa.
HITIMISHO:
Ugonjwa wa kisonono huambukizwa kwa kushiriki ngono na mtu aliyeambukizwa, hivyo unashauriwa kutokuwa na wapenzi wengi (multiple sexual partners) kwani kuwa na wapenzi wengi ni miongoni mwa tabia hatarishi zinazochangia mtu kupata maambukizi ya kisonono.Pia jitahidi kutumia kondomu wakati wa kushiriki ngono. Kwa msaada wa ushauri na tiba wasiliana nasi kwa simu namba 0625 305 487.
4 Comments