Ikiwa unatumia dawa fulani wakati wa kunywa pombe, hii inaweza kuathiri mwili wako kwa njia kadhaa kwani kumekua na kesi mbalimbali za vifo sababu ya watu kumeza dawa kisha kujisahau na kunywa pombe.Unywaji pombe na baadhi ya dawa kunamaanisha kuwa dawa hiyo inaweza isifanye kazi pia.
Hii ni imekuwa ni changamoto kubwa sana kwenye sekta ya afya, kwani kwa kawaida dawa yeyote anayopewa binadamu kutibu kitu fulani ni sumu, hivyo ikichanganywa na baadhi ya kemikali kama pombe huweza kudhuru na kuua kabisa.
Dawa 10 Ambazo Hupaswi Kuchanganya Na Pombe:
Zifuatazo ni dawa 10 ambazo hupaswi kuzitumia pamoja na pombe;
1) Dawa Za Kutibu Maambukizi Ya Bakteria.
Hizi ni dawa ambazo hutumika mara kwa mara kwenye jamii kutibu magonjwa mbalimbali kama vile kikohozi, kifua kikuu, vidonda vya tumbo nk. Dawa hizi hujulikana kwa kitaalamu kama Antibiotics. Mfano wa dawa hizo ni pamoja na flagyl, isoniazid, griseofulvin.
Matumizi ya dawa hizi na pombe huweza kusababisha kifo. Lakini pia kuna baadhi ya dawa za kutibu malaria kama vile Quinine na Artemether Lumefantrine (Dawa ya mseto) ni hatari zikitumika na pombe.
2) Dawa Za Kutibu Kisukari.
Dawa za kutibu kisukari ambazo hujulikana kwa kitaalamu kama Antidiabetic drugs mfano metformin tabs hutengenezwa kwa ajili ya kushusha kiwango kikubwa cha sukari mwilini. Hivyo matumizi ya dawa hizi na pombe husababisha hali ambayo hujulikana kwa kitaalamu kama lactic acidosis ambapo dalili ya hali hii ni maumivu ya misuli, tumbo kuuma na kusikia usingizi. Hali hii isipodhibitiwa hospitali husababisha kifo.
Soma pia hizi makala:
3) Dawa Za Kutibu Mafua Na Aleji.
Dawa za kutibu mafua na aleji hujulikana kwa kitaalamu kama Antihistamines mfano promethazine, chlorpheniramine maleate maarufu kama piriton, dawa hizi pia husababisha usingizi na uchovu kila zikitumika. Hivyo matumizi ya dawa hizi na pombe huongeza usingizi huu na uchovu mara dufu na kufanya mtu ashindwe kufanya kazi.
4) Dawa Za Kutibu Magonjwa Ya Akili.
Dawa za kutibu magonjwa ya akili kama vile chlorpromazine hutolewa kwa wagonjwa wa akili kupunguza dalili ya magonjwa hayo kwa kuwapa usingizi. Hivyo matumizi dawa hizi na pombe huongeza usingizi huu maradufu na kuwafanya washindwe kupumua hivyo huweza kusababisha kifo.
5) Dawa Za Kutibu Vidonda Vya Tumbo.
Mara nyingi vidonda vya tumbo hutibiwa na mchanganyiko wa dawa tatu ambazo hujulikana kwa kitaalamu kama triple therapy mfano cimetidine, metronidazole (flagyl), secnidazole au tinidazole. Mfano metronidazole ikitumika pamoja na pombe husababisha hali ambayo hujulikana kwa kitaalamu kama Disulfiram like reaction ambayo husababisha mapigo ya moyo kwenda mbio, kichefuchefu, kutapika, shinikizo la chini la damu, maumivu ya tumbo, maumivu ya kichwa, kuzimia na wakati mwingine kifo.
6) Dawa Za Usingizi.
Dawa za usingizi kama vile valium hutumika kwa wagonjwa wenye kushindwa kupata usingizi na wakati mwingine kwenye chumba cha upasuaji. Dawa hizi huleta usingizi mkali. Matumizi ya dawa hizi na pombe huongeza usingizi huu, hupunguza mapigo ya moyo, hupunguza uwezo wa kupumua, kupoteza fahamu na kifo lakini pia matumizi ya pombe na dawa za kifafa kama vile phenytoin hupunguza ufanisi wake na kupunguza uwezo wake wa kuzuia degedege (convulsion) za kifafa (epilepsy).
7) Dawa Za Kutibu Magonjwa Ya Moyo.
Hichi ni kikundi kikubwa cha dawa ambacho hutumika kutibu matatizo ya moyo. Matumizi ya dawa hizi na pombe wakati mwingine huingilia mfumo wa kazi wa mwili na kusababisha kizunguzungu na kuanguka wakati wa kusimama, mfano wa dawa izo ni pamoja na methyldopa, hydralazine na isosorbide mononitrate na dinitrate lakini pia matumizi ya pombe hupunguza uwezo wa dawa ya presha, propranolol na kuzuia uwezo wake wa kufanya kazi.
8) Dawa Za Kuzuia Damu Kuganda.
Kuna dawa ambazo hutolewa kwa wajawazito mara nyingi kulainisha damu ili isigande ambazo zinajulikana kwa kitaalamu kama Anticoagulants mfano warfarin, sasa matumizi ya pombe hufanya dawa hizi kushindwa kufanya kazi na kusababisha damu kuganda hivyo kuziba mishipa ya damu na kuleta kifo.
9) Dawa Za Kutibu Maumivu Makali.
kuna dawa za kutibu maumivu makali sana mfano morphine, pethidine, codeine, ambazo hutolewa kwa wagonjwa wenye maumivu makali kama ya kansa, uzazi na maumivu yatokanayo na ajali. Matumizi ya pombe huongeza wingi wa dawa hizi kwenye mfumo wa damu na kusababisha overdose yaani dawa kuwa nyingi mwilini pale inapomezwa na pombe hata kama ulimeza dozi sahihi.
10) Dawa za Kupunguza Msongo Wa Mawazo.
Dawa za kupunguza msongo wa mawazo hujulikana kwa kitaalamu kama Antidepressants mfano amitriptyline. Pombe huingilia kazi ya dawa izi na kufanya dawa hizo ziongezeke kwenye damu kwa kiasi kikubwa kuliko kawaida, hii humfanya mgonjwa alegee sana.
HITIMISHO:
Kutaja dawa hizi haimaanishi kwamba dawa zote ambazo sijataja hapa zinafaa kunywa na pombe, hapana. Kuna dawa bado zinafanyiwa utafiti kama zina madhara endapo zikitumika na pombe lakini pia ni vizuri kujenga tabia ya kutokunywa pombe kabisa kama uko kwenye dozi ya ugonjwa wowote na hata kama una ugonjwa ambao unataka kumeza vidonge maisha yote kama kisukari, presha, ukimwi, kifafa na kadhalika basi ni vizuri ukaacha pombe kabisa.
Leave a Reply