Kibofu cha mkojo kinapatikana sehemu ya chini ya maeneo ya tumbo na ni kiungo ambacho kina uwazi/tundu ndani yake.
Kazi Ya Kibofu Cha Mkojo:
Kukusanya na kuhifadhi mkojo unaotolewa na figo kabla ya kuutoa nje ya mwili wa binadamu.
Mchoro Wa Kibofu Cha Mkojo:
Kibofu cha mkojo kina kuta (layers) aina tatu za tishu ambazo ni pamoja na;
1) Mucosa Layer.
Hii ni kuta ya ndani kabisa ambayo ndio inayokutana na mkojo wa binadamu. Kuta hii nayo inakuta nyingi sana za seli au chembe chembe zinazo julikana kama transitional epithelium cells ambazo pia hupatikana kwenye sehemu ya mirija inayojulikana kama ureters, urethra na kwenye figo. Seli hizi zinazuia uvujaji wa mkojo kwenda kwenye sehemu nyengine ya mwili.
Ureter huingiza mkojo kutoka kwenye figo na urethra hutoa mkojo kutoka kwenye kibofu cha mkojo wakati wa kukojoa.
2) Lamina Propria.
Hii ni kuta ya katikati nyembamba sana kati ya kuta hizi tatu na ambayo mishipa ya damu na neva inapatikana hapa na ni muhimu sana wakati wa kupanga makundi ya saratani ya kibofu cha mkojo wakati wa tiba.
3) Muscularis Layer.
Hii ni kuta ya nje ambayo ndani yake kuna detrusor muscle na ndio kuta nene kati ya hizi tatu. Kazi yake kubwa ni kupumzisha kibofu cha mkojo ili mkojo uingie ndani na ukishajaa basi hukaza kibofu (contracts) na kufanya mkojo kutoka nje.
Nje ya hizi kuta tatu, kibofu cha mkojo kimezungukwa na mafuta ambayo hukinga kibofu kutokana na mtikisiko wowote na kukitenganisha na viungo vengine.
Saratani Ya Kibofu Cha Mkojo:
Saratani ya kibofu cha mkojo ni ugonjwa ambao unajumuisha ukuaji wa uvimbe kwenye kibofu cha mkojo. Saratani ya kibofu cha mkojo hujulikana kwa kitaalamu kama Bladder cancer.
Kuna saratani aina tatu kutokana na kuta hizi tatu zilizotaja hapo juu za kibofu cha mkojo ambazo ni pamoja na;
1) Urothelial Carcinoma (Transitional Cell Carcinoma).
Hii ndio aina ya saratani inayotokea kwa wingi na hutokea kwenye seli za transitional epithelium cells. Asilimia 90 – 95 ya saratani zote za kibofu cha mkojo huwa ni aina hii.
2) Squamous Cell Carcinoma.
Aina hii hutokea baada ya maradhi ya kwenye kibofu cha mkojo kwa muda mrefu kutokana na uwepo wa mawe kwenye kibofu cha mkojo (bladder stones) na huchukua asilimia 1- 2 ya saratani zote za kibofu cha mkojo. Huonekana sana maeneo ya mashariki ya kati na afrika. Aina hii ina uhusiano mkubwa na ugonjwa wa kichocho (schistosomiasis) cha muda mrefu.
3) Adenocarcinoma.
Hutokea baada ya inflammation ya kwenye kibofu cha mkojo kwa muda mrefu. Na huchukua asilimia 2 ya saratani zote za kibofu cha mkojo.
Soma pia hizi makala:
Mambo yanayochangia kupata saratani ya kibofu cha mkojo:
Yafuatayo ni mambo yanayo muweka mtu katika hatari ya kupata saratani ya kibofu cha mkojo ambayo ni pamoja na;
1) Uvutaji Wa Sigara.
Wavutaji sigara wako kwenye hatari ya kupata saratani hii mara mbili zaidi ya wale wasiovuta sigara.
2) Asili Ya Mtu.
Saratani hii huonekana zaidi kwa watu weupe kuliko watu weusi. Watu wa mashariki ya kati wanaasilimia ndogo zaidi.
3) Umri.
Huonekana zaidi kwa watu wenye umri zaidi ya miaka 40 lakini huweza kutokea kwenye umri wowote ule.
4) Jinsia.
Hutokea sana kwa wanaume mara mbili au tatu zaidi kuliko kwa wanawake.
5) Lishe.
Watu wanaokula kwa wingi nyama za kukaanga kwa mafuta na kutumia mafuta yatokanayo na wanyama wakati wa kupika wako kwenye hatari kubwa kupata saratani hii.
6) Historia Ya Saratani Ya Kibofu Cha Mkojo Kwenye Familia.
Inahusishwa na mabadiliko katika viashiria vya asili au jini (genes) aina ya HRAS, KRAS2, RB1, FGFR3.
7) Historia Ya Matumizi Ya Dawa Za Saratani Kama Vile Dawa Za Saratani Ya Matiti Nk.
Dalili Za Saratani Ya Kibofu Cha Mkojo:
Zifuatazo ni dalili za saratani ya kibofu cha mkojo ambazo ni pamoja na;
1) Kukojoa damu (gross haematuria) ambayo inaweza kuonekana kwa macho au kwa hadubini (microscopic haematuria).
2) Maumivu wakati wa kukojoa au kichomi wakati wa kukojoa (burning sensation).
3) Kukojoa mara kwa mara (frequency of urination).
4) Maumivu nyuma ya mgongo.
5) Kuhisi bado hujamaliza mkojo baada ya kukojoa awali.
6) Kuhisi mkojo ambao hautoki.
7) Kushindwa kujizuia kukojoa baada ya kukojoa awali (urgency).
8) Uvimbe wa saratani ndani ya kibofu cha mkojo.
Dalili na viashiria vengine ni pamoja na: Maumivu ya tumbo, upungufu wa damu mwilini, uzito kupungua, maumivu ya mifupa, kujikojolea.
Kumbuka: Baadhi ya dalili na viashiria hivi vinaweza pia kuonekana kwa wagonjwa wa saratani ya figo, tezi dume na cystitis.
Vipimo Vya Uchunguzi Wa Saratani Ya Kibofu Cha Mkojo:
Vifuatavyo ni vipimo vinavyotolewa katika hospitali ili kubaini saratani ya kibofu cha mkojo ambavyo ni pamoja na;
1) Cystoscopy.
Mpira unaoingiziwa kwenye mrija wa wa kutolea mkojo ambao una kamera mbele na taa ili kuchunguza kama kuna uvimbe wa saratani ya kibofu cha mkojo na kuchukua nyama kwa ajili ya uchunguzi wa kimaabara zaidi.
2) Bladder Biopsy.
Nyama iliyochukuliwa kwa kipimo hapo juu, huchunguzwa kwenye maabara ili kuthibitisha kama ni saratani.
4) Abdominal Pelvic Ultrasound.
Kuangalia kama kuna uvimbe kwenye kibofu cha mkojo au kwenye figo. Inaweza kugundua sababu nyengine ya kukojoa damu kutokana na uwepo wa mawe kwenye kibofu cha mkojo (bladder stones) au uvimbe kwenye tezi dume (prostate enlargement).
5) Urinalysis.
Hiki ni kipimo ch mkojo kinachoweza pia kugundua sababu ya kukojoa damu na kama kuna ugonjwa mwengine wowote wa kibofu cha mkojo.
6) Complete Blood Count (CBC).
Hiki ni Kipimo cha damu kinachotumika kuangalia wingi wa damu, kundi la damu iwapo mgonjwa atahitaji kuwekewa damu nk.
7) CT scan Na MRI.
Hiki kipimo husaidia katika uchunguzi wa saratani kwani hutoa maelezo mazuri na pia huweza kugundua saratani kama ipo kwenye figo, nyonga na sehemu nyingine mwilini.
8) Pyelography.
Hii ni aina ya x-ray ya kibofu cha mkojo ambayo hupigwa mgonjwa baada ya kuchomwa dawa maalumu (contrast dye) kwenye mishipa ya damu (Intravenous pyelography) au kwenye mrija wa kutoa mkojo (urethra) na hujulikana kama retrograde pyelography.
9) Bone Scan.
Kipimo hiki hutumika kuangalia kama saratani imesambaa hadi kwenye mifupa.
10) Chest X-Ray (CXR).
Kipimo hiki hutumika kuangalia kama saratani imefika kwenye mapafu.
Makundi Ya Saratani Ya Kibofu Cha Mkojo:
Kabla ya mgonjwa kupewa tiba, ni muhimu kwa daktari kwanza kujitahidi kujua kundi (stage) la saratani aliyonayo mgonjwa. Saratani hii imepangwa katika makundi tofauti kulingana na kama inaweza kutibiwa kwa njia ya upasuaji, kama imeenea hadi kwenye tezi (lymph nodes) na kama saratani imesambaa kwenye sehemu nyingine mwilini. Makundi ya saratani ya kibofu cha mkojo ni kama yafuatavyo;
1) Stage 0.
Seli za saratani zinapatikana kwenye kuta ya ndani ya kibofu cha mkojo tu.
2) Stage I.
Seli za saratani zimeenea kutoka kwenye kuta ya ndani ya kibofu cha mkojo lakini hazijafika kwenye nyama (muscles) ya kibofu cha mkojo.
3) Stage II.
Seli za saratani zimefika kwenye nyama za kibofu cha mkojo lakini hazijafika kwenye tishu za mafuta zilizozunguka kibofu cha mkojo.
4) Stage III.
Seli za saratani zimefika kwenye tishu za mafuta zinazozunguka kibofu cha mkojo hadi kwenye tupu ya mwanamke (vagina), tezi dume (prostate), mfuko wa uzazi (uterus) lakini hazijafika kwenye tezi (lymph nodes) au kwenye viungo vengine mwilini.
5) Stage IV.
Seli za saratani zimefika kwenye tezi, nyonga, kuta za tumbo (abdominal wall) na viungo vengine mwilini.
6) Recurrent.
Saratani imejirudia kwenye kibofu cha mkojo au kwenye viungo vengine baada ya kutibiwa hapo awali. Saratani ya kibofu cha mkojo ina kawaida ya kusambaa kwenye tezi, na kupitia kwenye damu hadi kwenye mapafu, ini, mifupa na sehemu nyengine za mwili.
Umuhimu Wa Kupanga Makundi Ya Saratani.
1) Inasaidia kuchagua tiba sahihi ya saratani ya mgonjwa
2) Saratani iliyo ndani sana inauwezekano mkubwa wa kusambaa kwenye tezi na sehemu nyengine mwilini kuliko ile ambayo ipo juu.
3) Kadri namba ya kundi inapoongezeka ndio ugonjwa ulivyo mbaya zaidi na asilimia ya kuishi kwa muda mrefu hupungua.
4) Husaidia katika kuwapanga wagonjwa kwenye makundi na hivyo basi kuweza kuwafanyia utafiti kutumia matibabu mapya kwa urahisi zaidi.
Tiba Ya Saratani Ya Kibofu Cha Mkojo:
Saratani hii ni kati ya saratani zinazojulikana kuwa na asilimia kubwa ya kujirudia baada ya kutibiwa. Saratani ya kibofu cha mkojo ina uwezekano mkubwa wa kutibika kama itagundulika mapema. Tiba hutegemea;
1) Aina ya saratani.
2) Kundi la saratani (stage).
3) Historia ya kutibiwa saratani yoyote hapo awali.
4) Umri wa mgonjwa.
5) Afya ya mgonjwa (ili kuweza kujua kama mgonjwa atahimili aina ya tiba, kuna wagonjwa wengine huwa wanakuwa wamedhoofika sana).
Tiba imegawanyika kwenye;
1) Tiba ya mionzi (Radiotherapy).
2) Tiba ya dawa.
3) Tiba ya upasuaji.
4) Tiba ya immunotherapy ama biological therapy.
Tiba Ya Mionzi (Radiation Therapy):
Mionzi hutumika kuua seli za saratani. Tatizo la tiba hii ni kwamba inaua seli za saratani pamoja na seli za kawaida na hutumika kama njia mbadala ya tiba ya upasuaji. Matumizi yake ni kwenye saratani ndogo zilizoathiri nyama ya kibofu cha mkojo. Tiba hii ipo ya aina mbili;
1) Mionzi inayotolewa kwa kutumia mashine ya mionzi (external radiation).
2) Mionzi inayotolewa kwa kupachika kifaa cha kutolea mionzi ndani ya mwili kwa kukiingiza kupitia kwenye mrija wa kutoa mkojo (urethra) au kupitia upasuaji mdogo kwenye maeneo ya kibofu cha mkojo na kukiweka kifaa hicho ndani ya kibofu cha mkojo (Internal radiation).
Madhara ya tiba ya mionzi:
Madhara ya tiba ya mionzi ni kama yafuatayo;
1) Kujisikia uchovu au kuchoka.
2) Kichefuchefu.
3) Sehemu ya ngozi ambayo mionzi imepita kuwa kavu,nyeusi au nyekundu na kuwasha.
4) Matatizo ya mkojo.
5) Kupata maradhi kirahisi kwa kuwa inapunguza kinga mwilini.
6) Upungufu wa damu mwilini (anaemia).
6) Tupu kuwa kavu kwa wanawake (vaginal dryness).
7) Kwa wanaume-Uume au dhakari kushindwa kusimama au kusimika (impotence).
Tiba Ya Dawa (Chemotherapy):
Tiba hii inaweza kutumika pekee au pamoja na tiba ya upasuaji au ya mionzi au kutumika pamoja na tiba ya upasuaji na mionzi (kutumika dawa + upasuaji + mionzi). Pia inaweza kutumika kabla au baada ya tiba nyingine. Dawa za saratani ya kibofu cha mkojo ni Methotrexate (M), Vinblastine (V), Doxorubicin (A) Cisplatin (C) au MVAC. Kwa wale wenye matatizo ya moyo hupewa CMV.
Dawa zinaweza kutumiwa kwa wale wenye saratani iliyosambaa mwilini au wale ambao wapo kwenye makundi kuanzia Stage 0 hadi Stage III baada ya upasuaji ili kupunguza uwezekano wa kujirudia na tiba hii hujulikana kama adjuvant chemotherapy.
Pia dawa hizi zinaweza kutolewa kabla ya upasuaji ili kuongeza ufanisi wa upasuaji na kupunguza ukubwa wa uvimbe wa saratani na tiba aina hii hujulikana kama neoadjuvant chemotherapy.
Wagonjwa wa Stage 0 na Stage I wanaweza kupewa dawa kupitia mpira unaojulikana kama catheter na dawa hukaa kwa muda (masaa kadhaa) na hutolewa baadae kwa njia ya kukojoa, hii hufanyika mara moja kwa wiki na huendelea kwa muda wa wiki kadhaa.
Madhara Ya Tiba Ya Dawa:
Madhara ya tiba ya dawai ni pamoja na;
1) Kuchoka.
2) Kichefuchefu.
3) Kutapika.
4) Nywele kunyofoka.
5) Kupungikiwa na damu mwilini.
6) Kupungua hamu ya kula.
Madhara hutofautiana kati ya mgonjwa mmoja na mwengine.
Tiba Ya Upasuaji:
Kuna aina tatu za upasuaji ambazo ni pamoja na;
1) Trans Urethral Resection With Fulguration.
Aina hii inahusisha kuondoa uvimbe wa saratani kutoka kwenye kibofu cha mkojo na hutumiwa kwa wagonjwa wa Stage 0 na Stage I na baada ya upasuaji hupewa dawa za saratani.
2) Radical Cystectomy.
Inahusisha uondoaji wa kibofu chote cha mkojo, tezi pamoja na viungo vengine vya mwili kwa wale ambao saratani imeenea hadi kwenye nyama za kibofu cha mkojo au saratani ambayo haijaingia ndani lakini haipungui au kuleta matokeo mazuri kwa kutumia tiba nyengine.
- Kwa wanaume upasuaji huu pia unahusisha kuondoa tezi dume pamoja na mishipa inayopitisha shahawa kutoka kwenye tezi dume kwenda kwenye dhakari au uume (seminal vesicles) na hivyo kuathiri ufanyaji wa mapenzi.
- Kwa wanawake, mfuko wa uzazi (uterus), mayai (ovaries), na sehemu ya tupu (part of vagina) pia huondolewa na hivyo mwanamke kutoweza kupata hedhi pamoja na kutoshika mimba maishani mwake. Pia huathiri ufanyaji wa mapenzi na mambo ya mkojo.
Kumbuka:
Baada ya kuondoa kibofu cha mkojo, mgonjwa anaweza kuwekea mfuko wa kuhifadhia mkojo ambao unakuwa nje ya mwili na atahitaji kuubadilisha mara kwa mara na kuutunza kuwa msafi na kuzuia maambukizi. Mgonjwa huyu atahitaji ushauri nasaha pamoja na kumuona daktari mara kwa mara ili aangalie sehemu iliyowekwa mpira na hali ya mgonjwa mwenyewe. Au sehemu nyengine ya kuhifadhia mkojo hutengenezwa ndani ya mwili wa mgonjwa zinazojulikana kama ileal conduit na continent urinary reservoir.
3) Segmental Or Partial Cystectomy.
Sehemu ya kibofu cha mkojo huondolewa kwa upasuaji hasa kwa wagonjwa wenye saratani ambayo haina hatari kubwa ya kusambaa.
Tiba Ya Immunotherapy Au Biological Therapy:
Tiba hii ni ya maji ambayo yamechanganyika na chanjo aina ya BCG, ambayo mgonjwa hupewa kwa kutumia mpira aina ya catheter ambao unaingizwa kwenye mrija wa kutoa mkojo (urethra) na huchochea kuamsha kinga ya mwili (stimulate immune system) ili itoe kemikali zinazosaidia kupambana na chembechembe au seli za saratani.
Madhara Ya Tiba Ya Immunotherapy:
Madhara ya tiba ya immunotherapy ni pamoja na;
1) Kichefuchefu.
2) Homa.
3) Kuhisi baridi (chills).
Madhara haya ni kwa muda mfupi tu.
Maendeleo Ya Mgonjwa Baada Ya Kupata Tiba:
Asilimia 90 ya wagonjwa wenye saratani ambayo bado haijaingia ndani sana huishi zaidi ya miaka mitano baada ya tiba. Asilimia tano ya wale walio na saratani ambayo imesambaa mwilini huishi kwa muda wa miaka miwili baada ya kupata tiba. Saratani inayojirudia ni hatari zaidi na hutoa matokeo mabaya kwa wagonjwa kwani wengi hawaishi muda mrefu baada ya kupata tiba.
Madhara Ya Saratani Ya Kibofu Cha Mkojo:
Baadhi ya madhara ya saratani ya kibofu cha mkojo ni pamoja na;
1) Upungufu wa damu mwilini.
2) Kushindwa kuzuia mkojo na hivyo kujikojolea.
3) Kupungua kwa tundu kwenye mrija wa kutolea mkojo (urethral stricture).
4) Kuvimba kwa ureters kutokana na mkojo kushindwa kwenda kwenye kibofu cha mkojo.
Jinsi Ya Kujiunga Na Saratani Ya Kibofu Cha Mkojo:
Yafuatayo ni mambo ambayo mtu anashauriwa kuyafanya ili kujikinga na saratani ya kibofu cha mkojo;
1) Acha kuvuta sigara.
2) Kunywa maji kwa wingi angalau lita 1 na nusu kwa siku ili kusaidia kuondoa kemikali zinazosababisha saratani mwilini. ‘’Kumbuka kunywa maji mpaka wakati unapokojoa mkojo unatoka bila rangi yoyote’’.
3) Kwa wale wanaofanya kazi viwandani, saluni, nk, hakikisha unajikinga kutokana na madhara ya kemikali zinazosababisha saratani.
HITIMISHO:
Kwa msaada wa ushauri, vipimo na tiba ya magonjwa ya afya ya uzazi wasiliana nasi kwa simu namba 0625 305 487.
Leave a Reply