PID Kwa Mama Mjamzito.

Pid Ni Nini?

Pid ni maambukizi katika viungo vya uzazi vya mwanamke ikiwemo mji wa mimba (uterus), mirija ya uzazi (fallopian tubes), na ovari (ovaries).

Pid Inasababishwa Na Nini?

Zifuatazo ni sababu zinazochangia mwanamke kupata ugonjwa wa pid ambazo ni pamoja na:

1) Magonjwa Ya Zinaa (STIs).

Hii ndiyo sababu kuu ya PID. Magonjwa ya zinaa kama vile gonorrhea (kisonono) na chlamydia husababisha zaidi ya nusu ya kesi (cases) za PID. Wanawake wanaopata maambukizi haya ya zinaa wako katika hatari kubwa ya kupata PID ikiwa hayatatibiwa mapema.

pid

2) Historia Ya Kuugua Ugonjwa Wa Pid.

Hii pia ni mojawapo ya sababu zinazoweza kuchangia mwanamke kupata ugonjwa wa pid, ambapo mwanamke ambaye umeshawahi kuugua pid kabla anaweza kuugua tena ugonjwa huo, hii ni kutokana na ugonjwa huo kutotibiwa vizuri hapo awali.

3) Matumizi Ya Vipandikizi Vya Ndani Ya Mfuko Wa Uzazi.

Matumizi ya vipandikizi (kitanzi) vya ndani ya mfuko wa uzazi vijulikanavyo kwa kitaalamu kama intrauterine contraceptive device (IUCD) kama njia mojawapo ya uzazi wa mpango yanaweza kuchangia mwanamke kupata maambukizi ya ugonjwa wa pid kwani wakati mwingine kitanzi huweza kuwahifadhi bakteria wanaotokana na magonjwa ya zinaa kwa urahisi.

kitanzi

4) Kujisafisha Uke Kupita Kiasi (Excessive Vaginal Douching).

Kujisafisha uke kupita kiasi kunaharibu mpangilio wa kawaida wa bakteria wazuri kwenye uke wajulikanao kama normal flora. Baadhi ya wanawake wanadhani kujisafisha sana uke husaidia kuondoa mambukizi, lakini ukweli ni kwamba uke umeumbwa na uwezo wa kujisafisha wenyewe (vagina is self cleansing). Kwa hiyo mwanamke anapotumia kemikali na spray kujisafisha uke unaua bakteria wazuri na kuongeza hatari ya kupata maambukizi ya ugonjwa wa pid.

vaginal douching

5) Kufanya Ngono Bila Kutumia Kinga.

Kufanya ngono bila kutumia kinga (kondomu) kunaongeza uwezekano wa mwanamke kupata magonjwa ya zinaa kama vile kisonono, kaswende, pangusa n.k. Bakteria wanaotokana na magonjwa hayo ya zinaa  husambaa kutoka kwenye Uke kwenda kwenye mji wa mimba (uterus), mirija ya uzazi (fallopian tubes) na kwenye ovary (sehemu ambapo mayai ya mwanamke hupatikana) na hivyo kusababisha ugonjwa wa pid.

6) Mwanamke Kuwa Na Wapenzi Wengi (Multiple Sexual Partners).

Mwanamke kuwa na mpenzi (mwanaume) ambaye ana wanawake wengi nje kunaongeza uwezekano wa mwanamke uyo kupata ugonjwa wa pid, hii ni kutokana na hatari ya kupata maambukizi ya magonjwa ya zinaa kama vile kisonono, kaswende, pangusa kutokana na uwepo wa ngono zembe baina ya wapenzi hao.

multiple sexual partners

Dalili Za Pid Kwa Mjamzito:

Mama mjamzito anayesumbuliwa na maambukizi ya pid anaweza kupata dalili zifuatazo:

1) Maumivu Ya Tumbo Chini Ya Kitovu.

Mama mjamzito mwenye maambukizi ya pid anaweza kupata maumivu ya tumbo chini ya kitovu, mara nyingi maumivu haya yanaweza kuwa makali au ya wastani na yanaweza kuja na kuondoka.

2) Kutokwa Na Uchafu Usio Wa Kawaida Ukeni.

Uchafu huu unaweza kuwa mzito, kuwa na rangi isiyo ya kawaida (kama kijivu au kijani), na mara nyingi hunuka vibaya.

3) Maumivu Wakati Wa Kukojoa.

Mrija wa kutolea mkojo nje ya mwili (urethra) unaweza kuathiriwa na PID, hivyo kukojoa kunaweza kuwa na maumivu au kuhisi kama kuna kuungua.

4) Homa Au Joto La Mwili Kupanda.

Homa isiyoelezeka au kuhisi baridi kali inaweza kuwa ishara ya maambukizi makubwa.

5) Maumivu Wakati Wa Kujamiiana.

Ikiwa mama mjamzito ana PID, anaweza kuhisi maumivu makali wakati au baada ya kujamiiana.

6) Kujisikia Uchovu.

Kuongezeka kwa uchovu na kukosa nguvu inaweza kuwa ishara ya PID, hasa kama imeambatana na maumivu na homa.

Madhara Ya Pid Kwa Mjamzito:

Kwa mama mjamzito, PID inaweza kuwa na athari kubwa kwa afya ya mama na mtoto aliye tumboni. Baadhi ya madhara yanayoweza kutokea ni pamoja na:

Madhara Kwa Mtoto.

1) PID inaweza kusababisha kuharibika kwa mimba (miscarriage) au kuzaa mtoto kabla ya wakati (preterm birth).

2) Maambukizi yanaweza kufika kwenye kondo la nyuma (placenta), jambo linaloweza kuathiri ukuaji wa mtoto na kusababisha mtoto kuzaliwa na uzito mdogo (low birth weight).

Madhara Kwa Mama.

1) PID inaweza kuongeza hatari ya kupata mimba nje ya mfuko wa uzazi (ectopic pregnancy).

 2) PID inaweza kusababisha kovu au mabadiliko kwenye mirija ya uzazi, hali inayoweza kufanya mama kutopata mimba tena baadaye.

3) Inaweza kusababisha maumivu ya kudumu ya nyonga (chronic pelvic pain) na kuongezeka kwa hatari ya kuzaa kwa upasuaji (C-section).

HITIMISHO:

Ni muhimu mama mjamzito kupata matibabu haraka akishukiwa kuwa na PID ili kuzuia madhara hayo. Matibabu ya PID mara nyingi huhusisha matumizi ya dawa za antibiotic, ambazo lazima zichaguliwe kwa uangalifu ili zisiwe na athari kwa mtoto.

Ni vyema kumshauri mama mjamzito aende hospitalini kwa uchunguzi na ushauri zaidi mara tu akihisi dalili kama vile maumivu ya tumbo la chini, kutokwa na uchafu usio wa kawaida, au maumivu wakati wa kukojoa.