Lijue Tatizo La Mimba Kutunga Nje Ya Kizazi (Ectopic Pregnancy).

Mimba kutunga nje ya kizazi  ni tatizo ambalo limetokea kuathiri wanawake mbalimbali. Kwa kawaida, isipokuwa mara chache sana, mimba zinazotunga nje ya kizazi hazina uwezo wa kukua kuwa mtoto kamili. Aidha, mimba hizi ni hatari kwa afya ya mama mjamzito kwa vile humfanya kupoteza damu nyingi na hatimaye kusababisha kifo. Tatizo la mimba kutunga nje ya kizazi hujulikana kwa kitaalamu kama “ectopic pregnancy”.

Aidha, zaidi ya asilimia 95% ya mimba zinazotunga nje ya kizazi hutokea kwenye mirija ya uzazi (fallopian tubes). Mimba zinazotunga kwenye mirija ya uzazi husababisha kiinitete (embryo) kujipachika katika kuta zake na hivyo kusababisha mishipa ya damu inayopita karibu na mirija ya uzazi kupasuka na damu kutoka kwa wingi hali ambayo isiposhughulikiwa mapema husababisha madhara zaidi na hata kifo.

ectopic pregnancy

Jinsi Tatizo La Mimba Kutunga Nje Ya Kizazi Linavyotokea:

Kwa kawaida mbegu ya kiume na yai la kike hukutana katika mirija ya uzazi (fallopian tubes) na mimba hutungwa. Kiinitete (embryo) husafri polepole kwenda kwenye mji wa uzazi ambako hujipandikiza kwenye mji wa mimba (uterus) na mimba huanza kukua. Katika tatizo hili la mimba kutunga nje ya kizazi mbegu ya kiume na yai huungana kutengeneza kiinitete, badala ya kupandikizwa kwenye mji wa mimba, kiinitete huenda kujipandikiza sehemu nyingine tofauti na mji wa mimba. Kiinitete kinaweza kujipandikiza kwenye mirija ya uzazi, ovari, kwenye shingo ya uzazi na ndani ya tumbo (abdominal cavity). Mimba nyingi za nje ya kizazi hujipandikiza kwenye mirija ya uzazi ambapo huwa na hatari ya kupasuka (rupture) kadri mimba inavyokua.

Mara chache sana mimba zinazotunga nje ya kizazi huweza kukua mpaka mwisho, nyingi huishia kupasuka (rupture) na kuondolewa kwa upasuaji.

Sababu Za Mimba Kutunga Nje Ya Kizazi:

Zifuatazo ni baadhi ya sababu hatarishi zinazochangia mimba kutunga nje ya kizazi ambazo ni;

1) Matatizo Katika Mirija Ya Uzazi:

Matatizo kwenye mirija ya uzazi yanayoweza kusababisha mimba kutunga nje ya kizazi ni pamoja na;

  • Maambukizi katika mfumo wa uzazi wa mwanamke (PID)
  • Matumizi ya vitanzi vya kuzuia mimba (Intra-uterine contraceptive devices)
  • Kuoteana kwa tishu za uterus kwenye viungo vingine vya uzazi au endometriosis.

Soma pia hii makala: Ujue Ugonjwa Wa PID(Pelvic Inflammatory Disease).

2) Uvutaji Sigara.

Uvutaji sigara kwa mwanamke una uhusiano mkubwa na utungaji wa mimba nje ya kizazi. Imeonekana kwamba wanawake wanaopendelea kuvuta sigara mara kwa mara wana hatari ya kupatwa na tatizo hili mara tano zaidi ya wale wasiovuta kabisa. Hali hii husababishwa na nikotini iliyomo ndani ya sigara. Kwa kawaida nikotini huchochea kusinyaa kwa mirija ya uzazi hali iletayo kuziba kwa mirija hiyo na hivyo kufanya kiinitete kushindwa kupita kwenye mirija ya uzazi kuingia kwenye mji wa mimba na kufanya mimba kutunga nje kizazi.

3) Upasuaji Wa Tumbo Uliofanyika Zamani.

Operesheni yeyote inayohusu mirija ya uzazi inaongeza uwezekano wa mimba kutunga nje ya kizazi kwa vile mirija ya uzazi huwa imesinyaa kutokana na operesheni hiyo.

4) Matumizi Holela Ya Baadhi Ya Dawa.

Matumizi ya baadhi ya dawa zenye homoni husababisha kupungua kwa uwezo wa mirija ya uzazi kusukuma kiinitete kuelekea kwenye mji wa mimba na hivyo kuleta uwezekano wa utungaji wa mimba nje ya kizazi. Dawa hizo ni kama dawa za kuzuia mimba zenye homoni za kike za progesterone, na dawa za kusaidia uzazi aina ya clomiphene.

Kumbuka: Sababu zingine hatarishi zinazopelekea mimba kutunga nje ya kizazi ni pamoja na; Kutoa mimba zaidi ya 3, teknolojia saidizi za uzazi (assisted reproduction), umri wa zaidi ya miaka 35 kwa wanawake.

Dalili Za Mimba Kutunga Nje Ya Kizazi:

Katika wiki za mwanzo za ujauzito, mimba iliyotunga nje ya uterus huwa na dalili sawa na za mimba ya kawaida. Dalili hizi ni pamoja na mwanamke kukosa hedhi, kujaa kwa matiti, kichefuchefu, na uchovu wa mwili. Hali hii hufanya ugunduzi wa mimba iliyotunga nje ya kizazi kuwa mgumu katika hatua zake za awali.

Hata hivyo dalili ya awali ya kuonesha kuwa mimba imetunga nje ya kizazi ni kuwepo kwa maumivu makali na damu kutoka ukeni. Maumivu yanaweza kuwa kwenye nyonga, tumbo au wakati mwingine kwenye mabega au shingo (iwapo kiwango cha damu inayotoka kwenye mirija iliyopasuka ni kingi sana mpaka kugusa kiwambo cha hewa).

Maumivu haya huweza kuwa makali na yanayokata kama kisu, na yanaweza kuwa upande mmoja zaidi wa nyonga ingawa si lazima yawe upande ulio na mimba.

Dalili zingine ni pamoja na;

  • Kizunguzungu na kuzimia kwa sababu ya kupoteza damu kwa wingi.
  • Shinikizo la damu kuwa chini, na
  • Maumivu ya chini ya mgongo.

Utambuzi Wa Mimba iliyotunga Nje Ya Kizazi:

Mimba iliyotunga nje ya kizazi huweza kugunduliwa kwa;

1) Daktari kusikiliza historia ya mgonjwa na kufahamu dalili zake na kumfanyia uchunguzi wa mwili (physical examination).

2) Kufanya vipimo kadhaa vinavyoonesha kuwepo kwa tatizo hilo. Vipimo hivyo ni pamoja na;

a) Kupima damu kwa ajili ya kuangalia kiwango cha homoni ya HCG (Human Chorionic Gonadotropin).

b) Kupima kiwango cha homoni ya progesterone ambayo kwa mama mwenye ectopic pregnancy huwa chini (chini ya 15ng/mls) zaidi ya mwenye mimba ya kawaida.

c) Ultrasound ambayo husaidia kutambua mimba ilipotungwa.

ultrasound
Pregnant woman getting ultrasound from doctor

Matibabu Ya Mimba Kutunga Nje Ya Kizazi:

Matibabu ya mimba kutunga nje ya kizazi yamegawanyika katika sehemu mbili ambazo ni;

1) Matibabu Kwa Kutumia Dawa.

Faida kubwa ya kufanya uchunguzi mapema ni kuwa inaongeza uwezekano wa kuokoa maisha ya mama, kuokoa mirija ya uzazi isipasuke na hivyo kuongeza uwezekano wa kupata mimba kwa njia ya kawaida siku za usoni. Iwapo, mimba bado ni ndogo sana na kiwango cha HCG (Human Chorionic Gonadotropin) bado kipo chini mno, daktari anaweza kushauri kusubiri huku akimfuatilia mgonjwa kwa ukaribu sana. Wakati mwingine, mwili huwa na uwezo wa kuifyonza mimba changa ndani kwa ndani na hivyo kuondoa hatari ya kuwepo kwa ectopic pregnancy.

Hali kadhalika, mama anaweza kupewa dawa aina ya methotrexate, ambayo ina uwezo wa kuzuia mimba kukua zaidi. Wakati dawa hii inapotolewa, ni muhimu pia kufuatilia kiwango cha HCG (Human chorionic Gonadotropin) ili kujiridhisha kuwa kimeshuka mpaka kufikia sifuri ili kuwa na uhakika kuwa mimba haipo tena.

Baadhi ya madaktari pia hutumia njia ya kuchoma dawa ya sumu ya potassium chloride kwenye mimba ili kuifanya isinyae na hatamaye kufyonzwa na mwili. Matibabu haya hufanyika chini ya uangalizi wa kipimo cha ultrasound.

2) Matibabu Kwa Kutumia Upasuaji.

Iwapo mrija tayari umepasuka, upasuaji wa dharura hufanyika kwa ajili ya kuzuia kupotea zaidi kwa damu. Sehemu ya mirija iliyopasuka huondolewa na mshipa wa damu uliopasuka hufungwa. Athari za matibabu kwa njia hii ni kuwa, huondoa uwezo wa mrija ulioathirika kupitisha yai tena maishani na hivyo kupunguza uwezekano wa mama kupata mimba siku za usoni.

Madhara Ya Mimba Kutunga Nje Ya Kizazi:

Mama mjamzito anaweza kukabiliana na athari kadhaa pale ambapo mimba itakuwa imetunga nje ya mfuko wa uzazi ambazo ni pamoja na;

a) Mimba aliyobeba kuharibika.

b) Mirija ya uzazi kupasuka na kusababisha kuvuja kwa damu nyingi kunakoweza kukachangia kutokea kwa kifo.

Hivyo mama Mjamzito anapaswa kupatiwa huduma ya haraka punde tu akapobainika kuwa mimba yake imetunga nje ya mfuko wa uzazi ili kuepukana na madhara hayo.

Njia Za Kuzuia Mimba Kutunga Nje Ya Kizazi:

Yawezekana kupunguza uwezekano wa mimba kutunga nje ya kizazi kwa kuzuia na kujiepusha na vihatarishi vinavyosababisha hali hiyo. Njia hizo ni kama;

1) Kujikinga na maambukizi katika mfumo wa uzazi wa mwanamke kwa kujiepusha na ngono zembe, au kupunguza idadi ya wapenzi wa kufanya nao ngono.

2) Kuacha kutumia holela dawa za homoni bila kupata ushauri wa daktari.

3) Kujiepusha na uvutaji wa sigara.

HITIMISHO:

Kwa ushauri na tiba ya magonjwa ya afya ya uzazi kwa wanaume na wanawake wasiliana nasi kwa simu namba 0625 305 487.