Madhara Ya Pid.

Pid ni maambukizi katika viungo vya uzazi vya mwanamke. Maambukizi haya kutokea ikiwa bakteria wanaoambukiza kwa njia ya kujamiiana watasambaa kutoka kwenye uke kwenda kwenye mji wa mimba (uterus), mirija ya uzazi (fallopian tubes) na kwenye ovary (ambapo mayai ya mwanamke hupatikana).

Pid

Leo katika mada yetu ya blogu hii tutazungumzia madhara yatokanayo na maambukizi ya pid kwa wanawake. Ungana nami katika kuchambua madhara haya.

1) Maumivu Sugu Ya Nyonga.

Maumivu ya muda mrefu ya nyonga ni tatizo la kawaida kwa watu wenye PID. Utafiti unaonyesha kuwa takriban 20% ya watu wenye PID hupata maumivu ya muda mrefu katika nyonga zao. Maumivu haya yanaweza kuathiri shughuli za kila siku na ubora wa maisha.

2) Ugumba.

PID inaweza kusababisha uharibifu kwenye mirija ya uzazi, hivyo kusababisha ugumba. PID ni sababu mojawapo ya ugumba kwa wanawake.

3) Mimba Kutunga Nje Ya Kizazi (Ectopic Pregnancy).

Wanawake wenye historia ya PID wana hatari kubwa ya kupata mimba nje ya kizazi kwa sababu ya uharibifu na makovu kwenye mirija ya uzazi. Makovu hayo yanaweza kuzuia yai lililorutubishwa kuhamia kwenye mji wa mimba.

4) Pid Kujirudia (Recurrent Pid).

Wanawake waliopata PID mara moja wako kwenye hatari kubwa ya kupata hali hiyo tena katika siku zijazo ikiwa hawatopata matibabu ya uhakika (kushindwa kumaliza dozi) au ikiwa wenza wao (sexual partners) hawatopata matibabu. PID ya mara kwa mara inaweza kusababisha uharibifu zaidi kwenye viungo vya uzazi ikiwemo mirija ya uzazi na kuongeza hatari ya kupata matatizo kama vile ugumba au mimba kutunga nje ya kizazi.

5) Majipu Kwenye Via Vya Uzazi (Tubo-Ovarian Abscess).

PID isiyotibiwa inaweza kusababisha mkusanyiko wa usaha kwenye mirija ya uzazi na ovari, hali inayoweza kuwa hatari ikiwa majipu haya yatatumbuka (rupture).

6) Mabadiliko Ya Hedhi.

PID inaweza kusababisha mzunguko wa hedhi kutokuwa wa kawaida, ikiwemo damu kutoka kwa wingi au hedhi kuwa kidogo sana.

Jinsi Ya Kujikinga Na Pid:

Ili kujikinga na maambukizi ya pid mwanamke unashauriwa kufanya mambo yafuatayo ambayo ni pamoja na:

1) Tumia Kinga Wakati Wa Kujamiiana.

  • Tumia kondomu – Kondomu husaidia kuzuia maambukizi ya magonjwa ya zinaa yanayosababisha PID.
  • Epuka ngono zembe – Kuwa mwaminifu kwa mwenzi mmoja asiye na maambukizi hupunguza hatari.

2) Pima Magonjwa Ya Zinaa Mara Kwa Mara.

Fanya vipimo vya magonjwa ya zinaa, STI’s (Sexually Transmitted Infections) mara kwa mara, hasa kama una mpenzi mpya au mwenza wako ana wapenzi wengine.

3) Tibiwa Haraka Ikiwa Una Maambukizi Ya Zinaa.

Tiba ya haraka ya magonjwa ya zinaa (STI’s) kama vile kisonono na chlamydia inaweza kuzuia PID. Usichelewe kutumia dawa ulizoandikiwa na daktari.

4) Epuka Kujisafisha Uke Kupita Kiasi (Excessive Vaginal Douching).

Kujisafisha uke kupita kiasi kunaharibu mpangilio wa kawaida wa bakteria wazuri kwenye uke wajulikanao kama normal flora. Baadhi ya wanawake wanadhani kujisafisha sana uke husaidia kuondoa mambukizi, lakini ukweli ni kwamba uke umeumbwa na uwezo wa kujisafisha wenyewe (vagina is self cleansing). Kwa hiyo mwanamke anapotumia kemikali na spray kujisafisha uke unaua bakteria wazuri na kuongeza hatari ya kupata maambukizi ya ugonjwa wa pid.

5) Dumisha Usafi Binafsi.

Jali usafi wa uke kwa kuosha kwa maji safi na sabuni isiyo na kemikali kali. Pia, epuka kushiriki taulo au nguo za ndani (chupi) na mtu mwingine.

6) Epuka Kuwa Na Wapenzi Wengi (Multiple Sexual Partners).

Kupunguza idadi ya wapenzi wa kimapenzi (sexual partners) hupunguza hatari ya kuambukizwa magonjwa ya zinaa yanayosababisha PID.

HITIMISHO:

Ikiwa una dalili zozote zinazoashiria PID, ni muhimu uonane na daktari haraka kwa ajili ya uchunguzi na matibabu