Kifua Kikuu Ni Ugonjwa Gani?
Ugonjwa wa kifua kikuu ni ugonjwa wa kuambukiza ambao huathiri zaidi mapafu lakini pia unaweza kuathiri sehemu nyingine za mwili kama vile mifupa. Ugonjwa huu unajulikana kwa kitalaamu kama ‘Tuberculosis(TB)‘.
Kifua kikuu husambazwa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine kwa kupitia hewa wakati anapokohoa, kupiga chafya, au mate yake yakiwa hewani.
Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), TB inaambukiza watu milioni 10 na huua watu milioni 1.5 kila mwaka, na hivyo kuifanya kuwa muuaji wa pili wa magonjwa ya kuambukiza baada ya Covid-19.
Soma pia hizi makala:
- Ifahamu Saratani Ya Tezi Dume: Mambo 7 Usiyo yajua.
- Uti Kwa Wanawake: Zijue Sababu 3 Zinazopelekea Kuugua Uti, Tiba Mbadala Na Kinga.
Kifua Kikuu Husababishwa Na Nini?
Ugonjwa wa kifua kikuu, husababishwa na bakteria wanaojulikana kama Mycobacteria tuberculosis.
Kumbuka: Kuna aina nyingi za jamii ya Mycobacterium kama vile Mycobacterium tuberculosis (husababisha kifua kikuu), mycobacterium leprae (husababisha ugonjwa wa ukoma), mycobacterium bovis (huathiri ngombe na binadamu), mycobacterium africanum nk.
Mycobacterium bovis ambayo huathiri ngombe, inaweza kuambukiza binadamu kama atakula bidhaa zinazotokana na maziwa ya ngombe ambayo yameathirika na bakteria hawa kama vile siagi, mtindi, maziwa yenyewe, cheese, ice cream nk. Aina hii ya bakteria huathiri mapafu, tezi (lymph nodes), tumbo na sehemu nyingine za mwili.
Aina Za Ugonjwa Wa Kifua Kikuu:
Kuna aina kuu tatu(3) za ugonjwa kifua kikuu ambazo ni pamoja na;
1) Kifua Kikuu Kinachosababisha Madhara.
Aina hii ya kifua kikuu hutokea pale ambapo bakteria waliopo mwilini wapo hai na kinga ya mwili imeshindwa kuwadhibiti hawa bakteria wasisababishe madhara.
Watu hawa wanaweza kumuambukiza mtu yoyote kifua kikuu kwa njia ya kuvuta pumzi kama watakohoa, kutema mate, kupiga chafya, kupiga kelele iwapo watafanya vitendo hivi karibu na watu wasio na ugonjwa huu.
Aina hii ya kifua kikuu hujulikana kwa kitaalamu kama Active tuberculosis.
2) Kifua Kikuu Kisichosababisha Madhara.
Aina hii ya kifua kikuu hutokea endapo kinga ya mwili imeweza kuwadhibiti bakteria na kuwafanya kushindwa kusababisha madhara.
Mtu mwenye aina hii ya kifua kikuu, hana dalili za ugonjwa huu, hajisikii mgonjwa na hawezi kuambukiza mtu mwingine ugonjwa wa kifua kikuu.
Aina hii inaweza kujirudia baadae na kuathiri sehemu ya juu ya mapafu na hivyo kusababisha kikohozi cha kawaida ambacho baadae huongezeka na kusababisha kikohozi cha damu au makohozi, homa, kupungua hamu ya kula, kupungua uzito bila sababu ya msingi na kutokwa jasho kwa wingi kuliko kawaida wakati wa usiku.
Aina hii ya kifua kikuu hujulikana kwa kitaalamu kama Latent tuberculosis.
3) Kifua Kikuu Kinachosambaa Mwilini.
Aina hii ya kifua kikuu hutokea endapo kinga ya mwili imepungua na kusababisha ugonjwa wa kifua kikuu kuenea kupitia damu hadi sehemu nyingine za mwili kama mifupa, mishipa ya fahamu, ngozi, figo, kibofu cha mkojo, ngozi ya moyo (pericadium), mfumo wa uzazi, viunganishi vya mifupa (joints) na lymphatic system.
Husababisha homa, kupungua hamu ya kula, kuchoka na kupungua uzito.
Aina hii ya kifua kikuu hujulikana kwa kitaalamu kama Miliary tuberculosis.
Vihatarishi Vya Ugonjwa Wa Kifua Kikuu:
Mambo yafuatayo yanamuweka mtu katika hatari ya kupata ugonjwa wa kifua kikuu;
1) Kuishi sehemu zilizo na mrundikano wa watu kama mabweni, kambi za jeshi nk.
2) Kuzeeka.
3) Magonjwa yanayoathiri kinga ya mwili kama Kisukari nk.
4) Wafanyakazi wa huduma ya afya.
5) Unywaji pombe kupindukia.
6) Ugonjwa wa ukimwi.
7) Utapia mlo.
8) Wasafiri au watalii kutoka nchi zilizo na idadi kubwa ya ugonjwa wa kifua kikuu.
9) Baadhi ya dawa – Dawa za ugonjwa wa maumivu ya mifupa (athritis).
10) Wale wasio na makazi.
11) Umaskini au hali duni ya kipato (poor socio economic status).
Dalili Za Ugonjwa Wa Kifua Kikuu:
Zifuatazo ni dalili na viashiria vya ugonjwa wa kifua kikuu Ambazo ni pamoja na;
1) Kukohoa zaidi ya wiki 2-3 na kuongezeka kutoa makohozi.
2) Kukohoa damu.
3) Kupungua hamu ya kula.
4) Kupungua uzito kwa asilimia 10 ya mwili.
5) Kutokwa na jasho kwa wingi wakati wa usiku.
6) Uchovu.
7) Maumivu makali ya kichwa.
8) Maumivu ya kifua.
9) Kupumua kwa shida.
Vipimo Vya Ugonjwa Wa Kifua Kikuu:
Vifuatavyo ni vipimo vinavyotolewa hospitali kwa wagonjwa wa kifua kikuu;
1) Kipimo Cha Makohozi.
Makohozi huchukuliwa kwa siku tatu mfululizo muda wa asubuhi na kupelekwa maabara kufanyiwa uchunguzi ili kuweza kugundua kama mtu ana TB.
Kwa wale wagonjwa wasioweza kutoa makohozi au wale wenye TB ya tumbo basi hufanyiwa kipimo cha gastric lavage.
Kipimo hiki hujulikana kwa kitaalamu kama Sputum for Acid Fast Bacilli (AFB).
2) Picha ya X-ray ya kifua.
TB ya mapafu huweza kugundulika kutumia kipimo hiki.
Kipimo hiki hujulikana kwa kitaalamu kama Chest X-Ray (CXR).
3) Kipimo cha kwenye ngozi.
Kipimo hiki hufanywa na daktari. Daktari huchoma dawa ya protein purified derivatives (PPD) kwenye ngozi ya mgonjwa, kama kutatokea uvimbe zaidi ya 5mm (0.2 in) baada ya masaa 48, basi mgonjwa huyo ana TB.
Kipimo hiki kinaweza kutoa majibu ambayo si sahihi hasa kwa wale ambao wamepata chanjo ya ugonjwa wa kifua kikuu, wenye ugonjwa wa hodgkins lymphoma, sarcoidosis na hata utapia mlo. Majibu yake ni lazima yasomwe na daktari.
Kipimo hiki hujulikana kwa kitaalamu kama Tuberculin skin test (Mantoux test).
4) Kipimo cha PCR (Polymerase Chain Reaction assay).
Kipimo hiki kinahusisha utambuzi wa bakteria wanaosababisha kifua kikuu kupitia vina saba vyao (DNA of bacteria). Ni kipimo cha uhakika zaidi.
5) Kuotesha bakteria maabara (Bacteria culture).
Kipimo hiki huchukua muda mrefu na ni ghali.
Tiba ya ugonjwa wa kifua kikuu.
Tiba ya kifua kikuu inahusisha matumizi ya dawa za kifua kikuu kwa muda wa miezi sita au tisa.
Dawa hizi zinahusisha matumizi ya miezi 2 ya kwanza ya dawa aina ya isoniazid, rifampicin, pyrazinamide, na matumizi ya miezi 4 ya isoniazid, rifampicin na ethambutol au streptomycin.
Dawa hizi hutolewa chini ya uangalizi yaani mgonjwa anakunywa chini ya uangalizi wa mhudumu wa afya (Directly Observe Treatment, short course).
Tiba ya ugonjwa wa kifua kikuu inatolewa bure nchini kote Tanzania.
Upasuaji unaweza kufanyika kwenye mapafu kama dawa zimeshindwa kutibu kifua kikuu.
Madhara ya ugonjwa wa kifua kikuu:
Yafuatayo ni madhara yanayoweza kutokea endapo magonjwa mwenye kifua kikuu atashindwa kupata matibabu mapema;
1) Maumivu ya uti wa mgongo.
2) Magonjwa ya moyo (heart disorders).
3) Uharibifu kwenye viungo (joint damage).
4) Matatizo ya ini au figo (Liver/kidney problems).
Jinsi Ya Kujikinga Na Ugonjwa Wa Kifua Kikuu:
1) Chanjo ya ugonjwa wa kifua kikuu ipo na inasaidia kukinga TB (BCG Vaccine) na imeleta mafinikio katika kukabiliana na kifua kikuu. Kawaida hutolewa kwa watoto baada ya kuzaliwa.
2) Kuziba pua na mdomo kwa kitambaa (mask) ili kujikinga na kifua kikuu.
3) Kufanya mazoezi mara kwa mara ili kuimarisha kinga ya mwili.
4) Kupata usingizi wa kutosha.
5) Kwenda hospitali kufanya vipimo mara kwa mara. Inashauriwa kufanya kipimo cha ngozi angalau mara moja kwa mwaka.
6) Kuimarisha kinga ya mwili kwa kula vyakula venye virutubisho vyote muhimu kwa afya bora.
7) Kutumia dawa aina ya isoniazid (INH) kwa wale walio kwenye hatari ya kuambukizwa kifua kikuu.
8) Shirika la afya duniani (WHO) linapendekeza wagonjwa wa ukimwi (HIV) ambao wana Latent TB wapewe dawa ya isoniazid (INH) kama kinga dhidhi ya kifua kikuu kila inapohitajika.
9) Kuepuka mikusanyiko au mrundikano wa watu kama vile kwenye mabweni, kambi za jeshi, baa nk.
10) Kuishi kwenye nyumba ambayo ina mfumo mzuri wa kuingiza na kutoa hewa yaani iwe na madirisha makubwa na ya kutosha.
Tb Ya Mifupa Na Dalili Zake:
HITIMISHO:
Ikiwa utahisi una dalili na viashiria vya ugonjwa wa kifua kikuu, tembelea hospitali au kituo cha afya kilichokaribu na wewe ili kuanza tiba mapema na kuepuka madhara yatokanayo na ugonjwa huu.
Ni mimi mwenye kujali afya yako Dr Isaya Febu.
Leave a Reply