Fangasi Sehemu Za Siri Kwa Mwanaume.

Fangasi Kwa Mwanaume:

Fangasi kwenye uume (fungal infections in men) ni maambukizi yanayosababishwa na fangasi wa aina mbalimbali, hasa Candida albicans. Maambukizi haya huathiri ngozi ya uume na maeneo ya karibu, na mara nyingi huambukizwa kutokana na usafi duni wa sehemu za siri.

Candida albicans

Maambukizi ya fangasi sehemu za siri kwa mwanaume uhusisha:

1) Tinea Cruris (Jock Itch).

Hii ni aina ya fangasi wa ngozi inayoathiri maeneo ya ndani ya mapaja, korodani, na karibu na uume ambayo inasababishwa na fangasi waitwao Trichophyton rubrum (dermatophytes). Mara nyingi jasho na kutovaa nguo za ndani safi au zinazopitisha hewa (boksa zinazobana) huchangia sana mwanaume kupata aina hii ya fangasi.

Dalili za aina hii ya fangasi ni pamoja na:

  • Muwasho mkali sehemu za siri na mapajani (Madoa mekundu ya duara yanayowasha sana).
  • Ngozi kuwa na ukavu au kuchubuka (kutoa magamba).

2) Candida Balanitis.

Ni kuvimba kwa kichwa cha uume (glans) kutokana na maambukizi ya fangasi. Aina hii ya fangasi huathiri zaidi wanaume wasiotahiriwa.

Candida Balanitis
fangasi kwenye uume

Dalili za aina hii ya fangasi ni pamoja na:

  • Kuwashwa na kuvimba kichwa cha uume.
  • Harufu mbaya sehemu za siri.
  • Maumivu ya uume au hisia ya kuchoma wakati wa kukojoa au wakati wa tendo la ndoa.
  • Kutokwa na uchafu chini ya govi wenye harufu mbaya.
  • Wekundu na hatari ya uvimbe wa sehemu ya govi.

3) Fungal Folliculitis (Fangasi Kwenye Vinywele Vya Sehemu Ya Siri).

Hili ni aina ya maambukizi ya fangasi yanayoathiri vinyweleo karibu na uume au kwenye korodani. Fangasi wanaohusika sana ni kundi la Candida albicans na Malassezia (pia huitwa Pityrosporum).

Sababu na Vichochezi vinavyopelekea aina hii ya fangasi ni pamoja na:

  • Kuwa na unyevunyevu na joto sehemu za siri (kutokana na jasho, nguo za kubana, tabia ya kukaa muda mrefu).
  • Kutumia nyembe au njia ambazo zinasababisha vinyweleo kukatwa na kurudi ndani, hasa bila usafi.
  • Upungufu wa kinga mwilini, lakini hata watu wenye afya njema wanaweza kupata tatizo hili.

Dalili za aina hii ya fangasi ni pamoja na:

  • Vimbe ndogo nyekundu (papules) zinazoweza kuwa na usaha (pustules), kuuma, kuwasha au kuchoma.
  • Ngozi katika eneo la mapaja ya ndani, au uume inaweza kuwa na upele au kuungua.
  • Upele unaweza kuonekana kama chunusi ndogo zinazozunguka vinywele.
  • Katika baadhi ya kesi, malengelenge madogo ya usaha hutokea na ngozi kuwa na harara au maumivu.

Madhara Ya Fangasi Sehemu Za Siri Kwa Mwanaume:

Fangasi sehemu za siri kwa mwanaume, ingawa inaweza kutibika kirahisi, inaweza kusababisha madhara ikiwa haitatibiwa au ikiwa maambukizi yamekuwa sugu. Madhara yatokanayo na fangasi sehemu za siri kwa mwanaume ni pamoja na:

1) Maambukizi Makali Na Ya Muda Mrefu.

Maambukizi ya fangasi sehemu za siri kwa mwanaume yasipotibiwa yanaweza kuwa makali zaidi na kusababisha maumivu na usumbufu mkubwa kama vile kupata miwasho na kujikuna mara kwa mara sehemu za siri. Maambukizi haya yanaweza kuwa sugu na kujirudiarudia.

2) Phimosis Na Paraphimosis.

Maambukizi ya fangasi sehemu za siri kwa mwanaume yanaweza kusababisha govi kuwa na uvimbe na kuuma, hali inayojulikana kama phimosis (govi kushindwa kurudi nyuma kabisa kutoka kwenye kichwa cha uume) au paraphimosis (govi kushindwa kurudi mbele baada ya kurudi nyuma). Mara nyingi madhara haya ya fangasi huwapata wanaume ambao hawajapata tohara.

Phimosis Na Paraphimosis.

3) Kudhoofisha Mfumo Wa Kinga Ya Mwili.

Maambukizi sugu ya fangasi sehemu za siri kwa mwanaume yanaweza kuashiria au kuchangia kudhoofisha mfumo wa kinga ya mwili, hali ambayo inaweza kuwa hatari zaidi kwa watu wenye magonjwa kama vile kisukari au HIV.

4) Uwezekano Wa Kueneza Maambukizi Kwa Wenza.

Fangasi sehemu za siri kwa mwanaume inaweza kuenezwa kwa wenza wake anaoshiriki nao ngono, na hivyo kusababisha maambukizi kwa wenza na hata kujirudiarudia kwa maambukizi kati ya wenza wake.

5) Madhara Ya Kisaikolojia.

Maumivu, muwasho sehemu za siri, na usumbufu wa kujikuna mara kwa mara vinaweza kuathiri maisha ya kila siku ya mwanaume, kuleta aibu, kujitenga kijamii, na matatizo ya kiakili kama vile wasiwasi na msongo wa mawazo (sonona).

HITIMISHO:

Kwa uhitaji wa tiba ya uhakika na njia bora za kujikinga na maambukizi ya fangasi sehemu za siri kwa mwanaume bonyeza hapa: Dawa Ya Fangasi Sugu Kwa Mwanaume.