Upungufu wa damu kwa mjamzito ni hali inayotokea wakati kiwango cha hemoglobini katika damu kinapungua chini ya kiwango kinachohitajika (<11 g/dl), hasa wakati wa ujauzito. Hemoglobini ni protini inayopatikana kwenye seli nyekundu za damu na inasaidia kusafirisha oksijeni mwilini., hivyo upungufu wake unaweza kuathiri afya ya mama na mtoto.
Upungufu wa damu kwa mjamzito hujulikana kwa kitaalamu kama anaemia in pregnancy.

Sababu Kuu Za Upungufu Wa Damu Kwa Mjamzito:
Zifuatazo ni sababu kuu zinazochangia upungufu wa damu kwa mjamzito:
1) Upungufu Wa Madini Ya Chuma.
Wakati wa ujauzito, uhitaji ya madini ya chuma huongezeka ili kusaidia katika utengenezaji wa seli nyekundu za damu mpya kwa ajili ya mama na mtoto aliye tumboni. Hivyo basi, lishe duni, ufyonzwaji duni wa madini ya chuma mwilini, au mahitaji makubwa ya madini ya chuma wakati wa ujauzito husababisha upungufu wa damu.
Aina hii ya upungufu wa damu unaosababishwa na upungufu wa madini ya chuma wakati wa ujauzito hujulikana kwa kitaalamu kama iron deficiency anaemia.
2) Upungufu Wa Foliki Asidi (Vitamini B9).
Foliki asidi (vitamini B9) inahitajika kwa utengenezaji wa seli nyekundu za damu.
Ukosefu wa foliki asidi wakati wa ujauzito unaweza kusababisha upungufu wa damu na kuongeza hatari ya matatizo kwa mtoto, kama vile kasoro za mfumo wa neva (neural tube defects).
Aina hii ya upungufu wa damu unaosababishwa na upungufu wa foliki asidi wakati wa ujauzito hujulikana kwa kitaalamu kama folic acid deficiency anaemia.
3) Upungufu Wa Vitamini B12.
Vitamini B12 ni muhimu kwa utengenezaji wa damu na mfumo wa neva wa mtoto.
Lishe isiyo na vyanzo vya vitamini B12 kama vile maziwa, mayai, samaki, na nyama inaweza kusababisha upungufu wa damu wakati wa ujauzito.
Aina hii ya upungufu wa damu unaosababishwa na upungufu wa vitamini B12 wakati wa ujauzito hujulikana kwa kitaalamu kama vitamin B12 deficiency anaemia.
4) Magonjwa Na Maambukizi.
Magonjwa kama vile malaria, minyoo tumboni, na magonjwa sugu yanayoathiri utengenezaji wa seli nyekundu za damu yanaweza kusababisha upungufu wa damu kwa mjamzito.
5) Kupoteza Damu Kwa Kiasi Kikubwa.
Kutokwa na damu nyingi kabla au wakati wa ujauzito, kama vile kutokwa na damu nyingi wakati wa hedhi kabla ya mimba, huweza kusababisha upungufu wa damu.
6) Mimba Za Mara Kwa Mara.
Mimba za mara kwa mara ni moja ya sababu kuu za upungufu wa damu kwa mjamzito. Wakati mwanamke anapata ujauzito mara kwa mara bila kupumzika vya kutosha, mwili haupati muda wa kurejesha madini muhimu kama vile chuma, foliki asidi, na vitamini B12, ambayo ni muhimu kwa utengenezaji wa chembe nyekundu za damu.
Dalili Za Upungufu Wa Damu Kwa Mjamzito:
Dalili zinaweza kuwa tofauti kulingana na kiwango cha upungufu wa damu. Dalili za kawaida ni pamoja na:
1) Uchovu wa mara kwa mara (easy fatigability)
2) Kizunguzungu (dizziness)
3) Mapigo ya moyo kwenda kasi (heart palpitation)
4) Kupumua kwa shida (shortness of breath)
5) Ngozi, midomo (lips), na kucha kuwa na rangi iliyopauka (paleness)
Jinsi Ya Kuzuia Upungufu Wa Damu Kwa Mjamzito:
Ili kuzuia upungufu wa damu wakati wa ujauzito, mwanamke unashauriwa kufanya mambo yafuatayo:
1) Kula Vyakula Vyenye Madini Ya Chuma.
Mfano: Nyama nyekundu, samaki, maini, maharagwe, mboga za majani (spinach, mchicha).

2) Kula Vyakula Vyenye Foliki Asidi.
Mfano: Parachichi, ndizi, mboga za kijani kibichi, nafaka zilizoongezewa foliki asidi.

3) Kula Vyakula Vyenye Vitamini B12.
Mfano: Mayai, samaki, maziwa, nyama.

4) Kunywa Juisi Ya Matunda Yenye Vitamini C.
Vitamini C husaidia mwili kufyonza madini ya chuma vizuri zaidi. Hivyo, kula matunda yenye vitamini C kama maembe, machungwa, limau, na tikitimaji. Juisi ya machungwa ni nzuri sana kwa kuongeza ufyonzaji wa madini ya chuma.

5) Virutubisho Vya Madini Ya Chuma.
Daktari anaweza kupendekeza vidonge vya madini ya chuma (ferrous sulphate) kwa wajawazito ambao wanakosa madini haya kutoka kwenye chakula. Vidonge hivi vinasaidia kuongeza kiwango cha madini ya chuma mwilini, lakini ni muhimu kufuata maelekezo ya daktari ili kuepuka matumizi mabaya.

6) Kuepuka Vinywaji Vinavyoharibu Ufanisi Wa Kufyonza Madini Ya Chuma.
Vinywaji kama vile chai, kahawa vinaweza kupunguza uwezo wa mwili kufyonza madini ya chuma. Epuka kuvinywa mara moja baada ya mlo, na badala yake kunywa kinywaji cha vitamini C au maji ya kawaida.

7) Fuatilia Afya Yako Kwa Vipimo Vya Damu Mara Kwa Mara.
Pindi unapojisikia kupata dalili za upungufu wa damu, hakikisha unapata vipimo vya damu kwa wakati ili kugundua upungufu wa damu mapema na kupata matibabu. Daktari anaweza kupendekeza matibabu zaidi kama inahitajika.

HITIMISHO:
Kuzingatia lishe bora na kuwa na mtindo mzuri wa maisha ni njia bora ya kuzuia upungufu wa damu kwa mjamzito. Ikiwa unahisi dalili za upungufu wa damu, ni muhimu kushauriana na daktari haraka ili kupata matibabu yanayofaa.
Leave a Reply