Tezi Dume Ni Nini?

Tezi dume ni tezi ndogo iliyopo katika mfumo wa uzazi wa wanaume. Iko chini ya kibofu cha mkojo na inazunguka sehemu ya juu ya mrija wa mkojo (urethra), ambao hubeba mkojo kutoka kwenye kibofu cha mkojo na kuutoa nje ya mwili. 

picha ya tezi dume

Kazi yake kuu ni kutengeneza na kutoa majimaji ambayo yanachanganyika na mbegu za kiume (sperms) wakati wa kujamiiana, na hivyo kusaidia katika uzalishaji wa shahawa (semen).

Majimaji haya yana umuhimu mkubwa katika kulinda na kutoa lishe kwa mbegu, na pia yanaweza kusaidia katika kusafisha njia ya mkojo.

Tezi dume inaweza kuathirika na matatizo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na:

1) Benign Prostatic Hyperplasia (BPH).

Hali hii inahusisha kuongezeka kwa ukubwa wa tezi dume, na inaweza kusababisha matatizo ya mkojo.

2) Prostatitis.

Haya ni maambukizi ya tezi dume, ambayo yanaweza kusababisha maumivu na shida katika kukojoa.

3) Saratani Ya Tezi Dume.

Hii ni aina ya saratani inayowapata wanaume, na inaweza kuwa hatari ikiwa haitagundulika mapema.

Vipimo Vya Tezi Dume:

Vipimo vya tezi dume hutumika kugundua matatizo kama vile kuvimba kwa tezi dume (BPH), prostatitis, au saratani ya tezi dume. Vipimo hivi vinaweza kupendekezwa na daktari ikiwa kuna dalili kama vile matatizo ya kukojoa, maumivu, au dalili za saratani. Vipimo vikuu vya tezi dume ni pamoja na:

1) Digital Rectal Examination (DRE).

Hiki ni kipimo ambapo daktari huingiza kidole cha shahada (index finger) kilichovaa glavu kwenye puru (rectum) ya mgonjwa ili kuhisi ukubwa, umbo, na uthabiti wa tezi dume. Kipimo hiki kinaweza kusaidia kugundua uvimbe au hali isiyo ya kawaida kwenye tezi dume.

Digital Rectal Examination (DRE)

2) Prostate-Specific Antigen (PSA).

PSA ni protini inayozalishwa na seli za tezi dume. Kipimo cha damu hufanywa ili kupima kiwango cha PSA. Kiwango cha juu cha PSA kinaweza kuashiria uwepo wa saratani ya tezi dume, lakini pia kinaweza kuongezeka kwa sababu ya hali kama vile BPH au maambukizi ya tezi dume (prostatitis).

Prostate-Specific Antigen (PSA)

3) Transrectal Ultrasound (TRUS).

Hii ni ultrasound inayofanyika kwa kutumia kipimo maalum kinachoingizwa kwenye puru ili kuchunguza tezi dume kwa undani zaidi. Hutumiwa kuona ukubwa wa tezi na pia kugundua uwezekano wa saratani au uvimbe mwingine.

4) Prostate Biopsy.

Iwapo kuna shaka ya saratani baada ya vipimo vya awali, kipimo cha biopsy hufanyika. Sampuli ndogo za tishu kutoka tezi dume huchukuliwa na kuchunguzwa kwenye maabara ili kuona kama kuna seli za saratani.

Prostate Biopsy

Kujifunza zaidi kuhusu saratani ya tezi dume bonyeza hapa: Ifahamu Saratani Ya Tezi Dume: Mambo 7 Usiyo yajua.