“Mimba kutoka” inamaanisha mimba kuharibika au kuondolewa kabla ya kufikia muda wa kujifungua.
Mara nyingi, mimba inaweza kutoka mapema katika ujauzito, hasa katika kipindi cha miezi mitatu ya kwanza ya ujauzito (first trimester). Hali hii inaweza kusababishwa na mambo mbalimbali, kama vile matatizo ya kijenetiki, matatizo ya afya ya mama, au sababu nyingine za kimazingira.
Mimba kutoka (kuharibika) hujulikana kwa kitaalamu kama spontaneous abortion (miscarriage).
Hali ya kutoka kwa mimba inayotokea katika miezi mitatu ya mwanzo (wiki ya 1 – 12 ya ujauzito) hufahamika kama kutoka kwa mimba mapema (early miscarriage) wakati hali ya kutoka kwa mimba inayotokea katika miezi mitatu ya pili (wakati wa wiki 13 – 20 ya ujauzito) kufahamika kama kutoka kwa mimba kulikochelewa (late miscarriage).
Hali ya kufa kwa kijusi tumboni ambayo hutokea baada ya wiki ya 20 ya ujauzito hufahamika kama uzazimfu (stillbirth), yaani mtoto huzaliwa akiwa amekufa.
Je Utajuaje Mimba Imetoka?
Dalili za mimba kutoka (kuharibika) zinaweza kujumuisha:
1) Kutokwa Na Damu Nyingi Ukeni.
Kutokwa na damu ukeni kwa kiasi kikubwa kuliko kawaida, na inaweza kuwa na mabonge ya damu ni dalili ya mimba kutoka (kuharibika)
2) Maumivu Ya Tumbo Na Mgongo.
Maumivu makali katika sehemu ya chini ya tumbo na mgongo yanaweza kuwa ishara ya mimba kutoka.
3) Kupoteza Dalili Za Ujauzito.
Dalili za ujauzito kama vile kichefuchefu na kuvimba matiti zinaweza kupungua ghafla au kutoweka kabisa.
4) Kutokwa Na Majimaji Ukeni.
Kutokwa na majimaji ukeni yanayochanganyika na damu na harufu isiyo ya kawaida.
Soma pia hii makala: Dalili Za Hatari Kwa Mama Mjamzito.
HITIMISHO:
Kama unapata dalili hizo hapo juu, ni muhimu kufika hospitali au kituo cha afya haraka iwezekanavyo kwa ajili ya vipimo na ushauri kutoka kwa wataalamu wa afya. Vipimo vya kitaalamu kama vile uchunguzi wa damu na vipimo vya ultrasound vinaweza kuthibitisha kama mimba imetoka (kuharibika) au la.
Leave a Reply