Kipimo Cha Mirija Ya Uzazi.

Kipimo cha mirija ya uzazi, kinachojulikana kama Hysterosalpingography (HSG), ni uchunguzi wa picha unaotumika kutathmini hali ya mirija ya uzazi ya mwanamke (fallopian tubes) na mfuko wa uzazi (uterus). 

Kipimo hiki pia hujulikana kama uterosalpingography.

Kipimo hiki kinatumika hasa kwa wanawake ambao wanapata shida ya kushika mimba ili kutathmini hali ya mirija ya uzazi (fallopian tubes) na mfuko wa uzazi (uterus).

Jinsi Mchakato Wa HSG Unavyofanyika:

1) Maandalizi.

Mgonjwa hupewa dawa za kupunguza maumivu kabla ya kipimo, kwani mchakato huu unaweza kusababisha usumbufu au maumivu kidogo.

2) Utaratibu.

Daktari ataanza kwa kuweka chombo cha kuenea kwenye uke (speculum) ili kuweza kuona mlango wa mfuko wa uzazi (cervix). Kisha, katheta ndogo huingizwa kwenye mlango wa mfuko wa uzazi na kioevu cha mionzi (contrast dye) huingizwa kupitia katheta hiyo.

3) Matokeo.

Baada ya contrast dye kuingizwa, picha za X-ray za eneo hilo zinapigwa ili kuona kama contrast dye imepita vizuri kwenye mfuko wa uzazi na mirija ya uzazi. Contrast dye inapotembea kwenye mirija ya uzazi, inapaswa kupita hadi kwenye tumbo la uzazi. Ikiwa mirija imeziba, contrast dye haitaweza kupita, hali ambayo itaonekana kwenye X-ray.

Mirija Ya Uzazi

Matumizi Ya HSG:

1) Kutathmini Ugumba.

HSG inasaidia kubaini sababu za ugumba, ikiwa ni pamoja na kuziba kwa mirija ya uzazi.

2) Kugundua Matatizo Ya Mfuko Wa Uzazi.

HSG Inatumika kugundua matatizo ya mfuko wa uzazi kama vile makovu kwenye mfuko wa uzazi.

3) Baada Ya Upasuaji.

HSG inaweza kufanywa baada ya upasuaji wa kuondoa vivimbe au urekebishaji wa mirija ya uzazi.

ingawa ni salama, kipimo hiki kinaweza kusababisha maumivu kidogo au kutokwa na damu kidogo baada ya mchakato, lakini dalili hizi hupotea baada ya muda.

Je ungependa kujua zaidi kuhusu kuziba kwa mirija ya uzazi?

Kama jibu ni NDIYO, bonyeza hapa: Mambo 6 Muhimu Usiyo yajua Kuhusu Kuziba Kwa Mirija Ya Uzazi Kwa Wanawake.

HITIMISHO:

HSG ni kipimo kinachotumika mara kwa mara katika utambuzi wa matatizo ya uzazi na mara nyingi huambatana na vipimo vingine ili kutoa picha kamili ya afya ya uzazi ya mwanamke.