Dalili Za Mirija Ya uzazi Kuziba Ni Zipi?

Dalili za mirija ya uzazi kuziba (fallopian tube blockage) mara nyingi hazionekani moja kwa moja, na wanawake wengi wanaweza wasiwe na dalili zozote hadi wanapokumbana na changamoto za kushika mimba (infertility).

Mirija Ya uzazi

Hata hivyo, kuna baadhi ya ishara zinazoweza kuashiria tatizo hili ambazo ni pamoja na:

1) Ugumba (Infertility).

Dalili kuu ya mirija ya uzazi kuziba ni kushindwa kupata mimba baada ya kujaribu kwa mwaka mmoja au zaidi bila kutumia njia za uzazi wa mpango.

2) Maumivu Ya Tumbo Au Nyonga.

Maumivu ya mara kwa mara kwenye eneo la nyonga au maumivu ya tumbo chini ya kitovu, hasa yanayotokea wakati wa hedhi au kufanya tendo la ndoa, yanaweza kuwa dalili ya tatizo kwenye mirija ya uzazi.

Maumivu haya yanaweza kuonekana kwa wanawake wenye hali kama vile endometriosis au PID (Pelvic Inflammatory Disease), ambapo hali zote hizo zinaweza kusababisha kuziba kwa mirija ya uzazi.

3) Mabadiliko Katika Mzunguko Wa Hedhi.

Wanawake wengine wanaweza kukumbana na mabadiliko katika mzunguko wa hedhi, kama vile kupata hedhi isiyo ya kawaida au hedhi yenye maumivu makali hali inayojulikana kama dysmenorrhea.

4) Kutokwa Na Uchafu Ukeni.

Ingawa si dalili ya moja kwa moja ya kuziba kwa mirija ya uzazi, lakini kutokwa na uchafu usio wa kawaida ukeni, hasa ikiwa unaambatana na maumivu au harufu mbaya, kunaweza kuashiria maambukizi ambayo yanaweza kusababisha kuziba kwa mirija ya uzazi.

5) Maumivu Wakati Wa Tendo La Ndoa.

Baadhi ya wanawake wanaweza kuhisi maumivu wakati wa tendo la ndoa hali inayojulikana kama dyspareunia, ambayo yanaweza kuashiria maambukizi yanayoweza kusababisha kuziba kwa mirija ya uzazi .

HITIMISHO:

Ni muhimu kutafuta ushauri wa kitabibu ikiwa unakabiliwa na dalili hizo, ili kufanyiwa uchunguzi na kupata matibabu sahihi.