Magonjwa ya akili ni matatizo ya kiafya yanayoathiri mawazo, hisia, na tabia za mtu.
Magonjwa ya akili yanaweza kuwa na athari kubwa katika maisha ya kila siku ya mtu.
Kuna aina mbalimbali za magonjwa ya akili, na kila mmoja una sababu, dalili na matibabu yake.
Baadhi ya aina za magonjwa ya akili ni pamoja na:
1) Sonona (Depression).
Hii ni hali ya kudumu ya huzuni, kukosa hamu ya kufanya shughuli za kila siku, na kutojisikia vizuri kihisia. Inaweza kusababisha matatizo ya usingizi, mabadiliko ya uzito, na hata mawazo ya kujidhuru.
2) Shida Ya Wasiwasi (Anxiety Disorders).
Hii inajumuisha hali kama vile wasiwasi wa mara kwa mara (generalized anxiety disorders), hofu isiyo na msingi maalum kuhusu vitu au hali fulani (specific phobias), na mashambulizi ya hofu yasiyotarajiwa (panic attacks). Wasiwasi unaweza kuathiri uwezo wa mtu kushiriki kwenye shughuli za kawaida.
3) Schizophrenia.
Hii ni hali ambayo inasababisha matatizo katika kufikiri, kufahamu ukweli, na hisia. Watu wenye schizophrenia wanaweza kuwa na matatizo ya kuona au kusikia vitu visivyo vya kweli (hallucinations) au kuwa imani zisizo sahihi (delusions).
4) Matatizo Ya Kula (Eating Disorders).
Magonjwa haya ya akili yanahusisha tabia zisizo za kawaida kuhusu chakula na uzito. Aina zake ni pamoja na:
- Anorexia Nervosa: Kukataa kula kwa sababu ya hofu ya kuongezeka uzito.
- Bulimia Nervosa: Kula kupita kiasi kisha kujitapisha au kutumia vidonge vya kuzuia uzito.
- Binge Eating Disorder: kula kupita kiasi bila kujizuia.
5) Matatizo Ya Mfadhaiko Wa Baada Ya Mshtuko (Post-Traumatic Stress Disorder – PTSD).
Hali hii hutokea baada ya mtu kupitia tukio la kutisha au lenye mshtuko mkubwa. Inaweza kuathiri uwezo wa mtu kuishi kawaida kutokana na kumbukumbu mbaya za tukio hilo.
6) Magonjwa Yatokanayo Na Matumizi Mabaya Ya Dawa (Substance Use Disorders).
Haya yanahusisha matumizi mabaya ya dawa za kulevya au pombe, ambayo yanaweza kuathiri uwezo wa mtu kufanya kazi au kuhusiana na watu wengine.
7) Magonjwa Ya Tabia (Personality Disorders).
Haya ni magonjwa ya akili yanayoathiri jinsi mtu anavyofikiria, anavyohisi, au anavyohusiana na wengine na inaweza kujumuisha hali kama vile;
- Borderline personality disorder: Huambatana na mabadiliko ya hisia, kujiona duni, na kuwa na mahusiano yasiyo thabiti.
- Antisocial Personality Disorder: Kukosa huruma kwa wengine.
- Narcissistic Personality Disorder: Kujipenda kupita kiasi.
8) Shinikizo La Mawazo (Bipolar Disorder).
Huu ni ugonjwa ambao mtu hupitia vipindi vya furaha kupita kiasi (mania) na huzuni kubwa (depression). Hali hizi mbili zinaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa maisha ya mtu.
9) Obsessive-Compulsive Disorder (OCD).
Hii ni aina ya ugonjwa wa akili ambapo mtu anapata mawazo au hofu zisizozuilika (zinazoitwa “obsessions”) na hujaribu kuziondoa au kupunguza kwa kufanya vitendo vya mara kwa mara (vinavyoitwa “compulsions”), au taratibu fulani. Mawazo haya au vitendo hivyo vinaweza kuchukua muda mwingi na kuathiri maisha ya kila siku ya mtu. Kwa mfano kunawa mikono mara kwa mara au kuangalia mara kwa mara kama mlango umefungwa.
10) Attention Deficit Hyperactivity Disorder (ADHD).
Huu ni ugonjwa wa akili ambao husababisha changamoto katika umakini, mhamasiko, na kudhibiti tabia.
- Attention Deficit: Hii ina maana ya kukosa uwezo wa kuzingatia au kukosa umakini (attention) kwa mambo mbalimbali. Watu wenye ADHD mara nyingi wanakumbwa na changamoto katika kumaliza kazi, kufuata maelekezo, au kuzingatia mazungumzo.
- Hyperactivity: Hii inamaanisha kuwa na shughuli nyingi kupita kiasi, ambapo mtu anaweza kuwa na mhamasiko wa kupita kiasi, kujihusisha na shughuli zisizohitajika, au kutokuwa na utulivu.
- Disorder: Hii ni neno linalotumika kuashiria hali au ugonjwa ambao unaharibu uwezo wa mtu kuishi maisha ya kawaida.
Huu ugonjwa unaweza kuathiri watu wa rika zote, lakini mara nyingi huathiri sana watoto, hali ambayo inaweza kuathiri uwezo wao wa kujifunza, kufanya kazi shuleni, na kuhusiana na wenzao.
Soma pia hii makala: Yajue Magonjwa Ya Akili, Dalili Zake Na Jinsi Ya Kutibu.
HITIMISHO:
Kwa msaada wa ushauri na tiba ya magonjwa ya afya ya akili, tembelea hospitali iliyokaribu nawe uonane na daktari bingwa wa magonjwa ya afya ya akili (psychiatrist).
Leave a Reply