Mjamzito:
Mwanamke anapokuwa mjamzito anashauriwa sana kula matunda katika mlo wake wa kila siku. Ulaji wa matunda kwa mjamzito una faida nyingi kwa mama mwenyewe pamoja na mtoto aliye tumboni kwa sababu matunda ni chanzo bora cha vitamini, madini na nyuzi nyuzi (dietary fibres).
Wakati wa ujauzito mama anahitaji virutubisho ambavyo hutokana pia na ulaji wa matunda zaidi kwa ajili ya maendeleo yake ya kiafya pamoja na mtoto aliye tumboni. Lishe bora itokanayo na ulaji wa matunda kwa mama mjamzito huimarisha afya ya mama na humsaidia mtoto aliye tumboni kukua vizuri kimwili na kiakili.

Leo katika makala yetu tutazungumzia baadhi ya matunda mazuri anayotakiwa kula mjamzito kwa ajili ya maendeleo yake ya kiafya pamoja na mtoto aliye tumboni, matunda haya ni pamoja na;
1) Parachichi.
Mama mjamzito anashauriwa kula parachichi kama sehemu ya mlo wake wa kila siku, kwa sababu parachichi ni chanzo kikubwa sana cha mafuta mengi mwilini maarufu kama fatty acids ambayo husaidia katika ukuaji wa ubongo, ngozi, misuli ya mtoto aliye tumboni. Pia ulaji wa parachichi kwa mama mjamzito humsaidia kuepukana na tatizo la kukosa/kupata choo kigumu.

Soma pia hii makala: Faida Za Parachichi Kwa Mjamzito.
2) Ndizi Mbivu.
Ndizi mbivu ni chakula kizuri sana wakati wa ujauzito. Ndizi mbivu zina viwango vikubwa vya madini ya kalishiamu na potasiamu ambayo yanamsaidia mama mjamzito kuepukana na changamoto ya kukaza kwa misuli ya miguu. Ikiwa mama mjamzito una hamu ya tunda lenye sukari lililo salama kwako na mtoto aliye tumboni, ndizi mbivu ni chaguo sahihi. Lakini kama una kisukari kilichosababishwa na ubebaji mimba (gestational diabetes), chagua kula ndizi za kupikwa (mbichi).

3) Tikiti Maji.
Tunda hili lina kiwango kikubwa cha maji kuliko tunda lingine lolote-92%. Ikiwa unapambana na tatizo la kukosa maji mwili wakati wa ujauzito, unashauriwa kula tunda hili. Tikiti maji lina madini ya potasiamu, zinki na foliki asidi kwa ajili ya kupambana na misuli ya miguu kukaza hasa wakati wa usiku na kusaidia ukuaji wa uti wa mgongo wa mtoto tumboni.

4) Machungwa.
Chungwa linaweza kuwa tamu au chachu, ladha hizi zina pendwa na wanawake wengi ambao wanasubuliwa na kichefuchefu wakati wa ujauzito. Machungwa yana kiwango kikubwa cha maji, ni chanzo kizuri sana cha vitamini C. Vitamini hii inachangia kukuza kinga ya mwili kwa mama mjamzito na mtoto aliye tumboni, na pia inasaidia kujenga tishu muhimu kwa ajili ya ukuaji wa kimwili wa mtoto aliye tumboni.

Soma pia hii makala: Faida Za Machungwa Kwa Mjamzito.
5) Embe.
Mama mjamzito anashauriwa pia kula embe kwani embe ni chanzo kizuri sana cha vitamini C. Vitamini C husaidia kuongeza kinga ya mwili kwa mama mjamzito na mtoto aliye tumboni.

6) Tufaha (Apple).
Mama mjamzito anashauriwa pia kula tufaha au apple katika mlo wake wa kila siku. Matunda haya yana vitamini A na C, maji ya kutosha na nyuzi nyuzi (dietary fibers) ambazo humsaidia mama mjamzito kuepukana na tatizo la kukosa/ kupata choo kigumu.

7) Peasi.
Peasi ni chanzo kizuri cha nyuzinyuzi zinazosaidia kupambana na tatizo la kukosa choo. Peasi pia ni chanzo kizuri cha vitamini C, pamoja na madini chuma, magnesiamu na foliki asidi. Ulaji wa tunda hili kwa mama mjamzito husaidia kuboresha afya mama mwenyewe na mtoto aliye tumboni.

8) Komamanga.
Komamanga lina kiwango kikubwa cha kirutubisho kiitwacho polyphenol. Tafiti pia zimeonesha kuwa ulaji wa komamanga wakati wa ujauzito unasaidia katika kuongeza kinga ya mwili kwa mtoto aliye tumboni.

HITIMISHO:
🍎 Kiasi Gani Cha Matunda Nile Nikiwa Mjamzito?
Kwa ujumla, mjamzito anaweza kulenga takribani vikombe 1½–2 vya matunda kwa siku, kutegemea mahitaji yake ya nishati, umri, uzito na kiwango cha shughuli. Muhimu zaidi ni kutofautisha aina za matunda.
Kikombe 1 cha matunda kinaweza kuwa:
- 🍌 Ndizi 1 ya wastani
- 🍊 Machungwa 1–2, kulingana na ukubwa
- 🥭 Embe takribani 1 dogo
- 🍎 Tufaha 1 dogo
- 🍐 Pera 1 ndogo
- 🍉 Vipande vya tikiti maji vilivyokatwa kiasi cha kujaza kikombe 1
- 🍓 Stroberi takribani kikombe 1
🕐 Unaweza kuyagawa hivi:
- Asubuhi: ndizi 1
- Mchana: chungwa 1 au embe
- Jioni: pera/tufaha au kikombe cha tikiti maji
Si lazima ule matunda yote kwa wakati mmoja. Matunda mazima ni bora kuliko juisi, kwa sababu yana nyuzinyuzi zaidi na kwa kawaida hayapandishi sukari ya damu haraka kama juisi.
⚠️ Kama una kisukari cha ujauzito.
Usiongeze matunda bila kuzingatia kiwango cha sukari kwenye damu. Ni vizuri kuyagawa katika sehemu ndogo na kufuata ushauri wa daktari au mtaalamu wa lishe.
Na pia osha matunda vizuri kabla ya kula.











Leave a Reply