Dalili Za Sikoseli Kwa Mtoto.

Sikoseli Ni Nini?

Sikoseli ni ugonjwa wa kurithi unaoathiri seli nyekundu za damu, unaojulikana pia kama ugonjwa wa seli mundu (sickle cell disease). 

Katika hali ya kawaida, seli nyekundu za damu ni mviringo na rahisi kusafiri kwenye mishipa ya damu ili kusafirisha oksijeni mwilini. Hata hivyo, kwa watu wenye sikoseli, seli hizi nyekundu za damu hubadilika na kuwa na umbo la mundu (kama mwezi mwandamo).

Sikoseli

Matokeo yake ni kwamba seli hizi haziwezi kusafiri vizuri kwenye mishipa ya damu, na zinaweza kukwama kwenye mishipa midogo, jambo ambalo linaweza kuzuia mtiririko wa damu. Hii husababisha maumivu makali na matatizo ya kiafya kama vile uharibifu wa viungo, upungufu wa damu, na maambukizi mara kwa mara.

Lakini pia Seli hizi huwa na maisha mafupi zaidi kuliko seli nyekundu za kawaida, jambo linalopelekea upungufu wa damu (anemia), hali ambayo pia ni ya kawaida kwa wagonjwa wa sikoseli.

Dalili za sikoseli kwa mtoto huanza kuonekana mara nyingi baada ya umri wa miezi mitano au sita. Baadhi ya dalili hizo ni pamoja na;

1) Upungufu Wa Damu (Anemia).

Seli za sikoseli huvunjika haraka na kuacha mwili ukiwa na idadi chache ya seli nyekundu, hali inayoweza kusababisha uchovu na udhaifu kwa mtoto.

2) Maumivu Makali.

Watoto wanaweza kupata maumivu ya ghafla yanayojulikana kama “pain crisis,” ambayo yanaweza kutokea kwenye mifupa, kifua, au tumbo. Maumivu haya hutokana na seli za sikoseli zinazoziba mishipa ya damu.

3) Kuvimba Vidole.

Kuvimba vidole kunaweza kutokea kutokana na kutokana na mzunguko mbovu wa damu (ukosefu wa oksijeni) kwenye vidole, hali inayoweza kusababisha maumivu.

4) Kuchelewa Kukua.

Watoto wenye sikoseli wanaweza kuchelewa kukua na kubalehe kutokana na upungufu wa oksijeni na virutubisho muhimu mwilini.

5) Maambukizi Mara Kwa Mara.

Watoto wenye sikoseli wako katika hatari kubwa ya kupata maambukizi mara kwa mara kama vile nimonia kutokana na uharibifu wa mfumo wa kinga.

6) Uchovu Mara Kwa Mara.

Watoto wanaweza kujisikia uchovu mara kwa mara kutokana na upungufu wa seli nyekundu za damu.

Je ungependa kujifunza zaidi kuhusu sikoseli? Kama jibu ni NDIYO, bonyeza hapa: Yajue Mambo 7 Muhimu Kuhusu Ugonjwa Wa Siko Seli.

HITIMISHO:

Ni muhimu kwa wazazi wenye watoto walio na dalili hizi kutafuta ushauri wa kitaalamu ili kupata uchunguzi sahihi na matibabu yanayofaa. Matibabu ya mapema yanaweza kusaidia kuboresha ubora wa maisha ya mtoto mwenye sikoseli.