Ujue Uhusiano Kati Ya Rhesus Factor Na Ujauzito.

Bila shaka umewahi kuwasikia wataalamu wa afya wakisisitiza umuhimu wa wenza kufanya vipimo mbalimbali kabla ya kuamua kuwa pamoja kwa ajili ya kutengeneza familia (kuzaa).

Moja ya vipimo vinavyosisitizwa ni cha makundi ya damu na Rhesus factor.

Kipimo hiki ni muhimu sana kwa sababu utofauti wake baina ya wenza unaweza kuathiri watoto watakaozaliwa na hivyo lengo la kuwa na muendelezo wa familia lisifikiwe hivyo kuzua migogoro baina ya wana ndoa, ndugu au watu wengine wa karibu mara nyingi ikihusianishwa ni uchawi.

Binadamu wameundwa na makundi manne ya damu, yaani A, B, AB na O.

Makundi haya hutengenezwa katika seli nyekundu za damu (Red Blood Cells) au RBCs.

Nje ya kundi husika la damu, chembe hizi nyekundu za damu zinaweza kuwa ama kutokuwa na protini maalumu juu yake iitwayo Rhesus factor.

rhesus factor

Seli yako ya damu ikiwa na protini hii tunasema wewe una Rhesus factor positive (Rh+) na kwa yule ambaye seli zake hazina protini hii tunasema ni negative (Rh-).

Kazi ya Rhesus factor (antigen) ni kuimarisha ukuta wa seli nyekundu za damu lakini kazi nyingine huupa mwili taarifa juu ya kitu kigeni kinachoweza kuudhuru mwili (foreign body) ili mwili uweze kutengeneza kinga (antibodies) za kuulinda dhidi ya mashambulizi tarajiwa.

Rh Factor Na Ujauzito:

Itakapotokea mwanamke ana group la damu ambalo halina protini ya Rhesus (Rh-) akakutana na mwanaume ambaye yeye group lake la damu lina protini hii (Rh+) na mwanamke kupata ujauzito na mtoto huyu akarithi vinasaba vya baba yaani Rh+ inaweza kuleta tatizo kwani endapo utatokea mwingiliano wa damu ya mtoto na ya mama ikitokea mimba imetunga nje ya kizazi (ectopic pregnancy), kutoka damu kipindi cha ujauzito (placenta previa/abruptio placenta) au wakati wa kujifungua. Mwingiliano huu hutengeneza hali ijulikanayo kwa kitaalamu kama Rh Incompatibility.

Rhesus Factor Na Ujauzito

Hii hutokea pale ambapo seli nyekundu za damu za mama (Rh-) zitagusana na seli nyekundu za mtoto (Rh+) hivyo seli za kinga za mama (antigen) zitatambua seli za mtoto kama kitu kigeni kinachotaka kumdhuru na hivyo zitazalisha seli kinga (antibodies) ili kushambulia seli za Rh+.

Kwahiyo mtoto huyu wa kwanza atazaliwa salama kabisa bila tatizo kwake, lakini itakapotungwa mimba nyingine yenye Rh+ mimba hii haitaweza kukua kwani mfumo wa kinga wa mama utaitambua kama kitu kigeni na hivyo mwili utafanya kila kitu kuhakikisha unaiharibu, kuiua na kuitoa.

Hivyo seli nyekundu za mtoto aliyeko tumboni zitaharibiwa vibaya na hivyo ujauzito wa mtoto huyu na wanaofuatia (Rh+) kushindwa kukua na kuharibika.

Kumbuka: Ikiwa mwanamke huyu aliwahi kupata ujauzito akautoa/ukaharibika au mimba kutunga nje ya kizazi na mwingiliano wa damu ya mtoto ambaye alitarajiwa kuwa (Rh+) na damu yake yenye (Rh-) kutokea basi mimba zote zinazofuata za watoto zenye Rh+ zitaharibika.

Kwa maana hiyo inaweza kuwa mimba yake ya kwanza aliyoamua kuzaa na kulea lakini mimba hii itaharibika sababu awali alishapata mimba kama hiyo.

Japo mtoto hakuzaliwa ila damu zilishagusana na hivyo mwili wake kutengeneza kinga dhidi ya ujauzito mwingine wa kufanana na huo (Rh+).

Sasa swali la kujiuliza: Je wakikutana watu kama hawa wenye Rh factor tofauti hawapaswi kuoana/ kupata watoto? jibu ni WANAWEZA KUZAA.

Inapotokea wamepima makundi yao ya damu na kukutwa ni Rh+ na Rh- kabla ya kuamua kuzaa ambapo mwanamke akiwa mjamzito atapaswa kuchomwa sindano maarufu kama Anti-D / (Rho) au RhoGAM wiki ya 28 ya ujauzito na mara baada ya kujifungua.

Sindano hii inapaswa kuchomwa pia ikiwa mama mjamzito amepoteza ujauzito (miscarriage), mimba imetunga nje ya kizazi (ectopic pregnancy) au limetokea tukio lolote la kumsababishia kutoka damu kipindi cha ujauzito kabla ya kujifungua.

Nini Umuhimu Wa Sindano Hii?

Sindano hii huzizuia seli kinga za mama kuzalisha antibodies ambazo zingeweza kuja kushambulia seli za ujauzito unaofuata wa mtoto ambaye ni Rh+ na kwa kufanya hivyo mimba nyingine zote zitakazokuja ambazo ni za Rh+ zitaweza kukua na kuzaliwa bila ya tatizo lolote kwa mama au kwa mtoto.

Kumbuka: Ikiwa mama ni Rh- na mtoto ni Rh- hakuna madhara kwao.

HITIMISHO:

Ni matumaini yangu elimu hiyo fupi hapo juu imekusaidia kuelewa jambo hilo kwa lugha rahisi na itakusaidia kufanya maamuzi sahihi kabla ya kuamua kuwa na mtoto na mwenza wako, kama si wewe basi hata watu wako wa karibu. Unashauriwa kufanya VIPIMO mbalimbali kabla ya kuamua KUZAA.