Msongo Wa Mawazo: Athari Za Msongo Wa Mawazo Kwa Mwanamke.

Msongo Wa Mawazo Ni Nini?

Msongo wa mawazo ni mfadhaiko wa akili anaoupata mtu kutokana na shida, taabu, dhiki, matatizo au changamoto zinazomkabili katika maisha ya kila siku.

Kwa kawaida mtu hupata msongo wa mawazo pale anaposhindwa au kukosa namna ya kukabiliana na jambo linalomsumbua.

Msongo Wa Mawazo

Dalili Za Mtu Mwenye Msongo Wa Mawazo:

Dalili za mtu mwenye msongo wa mawazo ni pamoja na:

1) Kujihisi Kukosa Tumaini Au Kukata Tamaa.

Mtu mwenye msongo wa mawazo huhisi kuwa hakuna suluhisho kwa matatizo yake, na huweza kupatwa na mawazo ya kutaka kukimbia matatizo au hata kujidhuru. Hali hii ni hatari na inahitaji msaada wa haraka wa kitaalamu.

2) Kukosa Usingizi (Insomnia).

Msongo wa mawazo huathiri uwezo wa mtu kulala vizuri. Mtu anaweza kupata shida kulala, kuamka mara kwa mara usiku, au kuamka mapema na kushindwa kurudi kulala. Kukosa usingizi huongeza uchovu na huathiri utendaji wa kila siku.

3) Kujihisi Kuchoka Na Kukosa Ari (Mood) Ya Kufanya Kazi.

Msongo wa mawazo huathiri uwezo wa kufanya kazi au kufurahia mambo ambayo awali yalikuwa yanavutia. Mtu anaweza kupoteza motisha ya kufanya kazi au shughuli za kila siku hali hii ikiambatana na hisia ya kutokujali au kutoona thamani ya juhudi zake.

anedonia

4) Wasiwasi Na Huzuni Ya Wa Kwa Mara.

Mtu mwenye msongo wa mawazo  anakuwa na hali ya wasiwasi wa kudumu, ambapo anahisi kuwa mambo hayaendi sawa au kuna hatari inayomkabili, hata kama hakuna msingi wa hofu hiyo. Huzuni inakuwa sugu, na mtu anaweza kupoteza hamu ya kufanya mambo aliyokuwa akiyafanya hapo awali.

5) Kubadilika Kwa Tabia.

Msongo wa mawazo huweza kusababisha mabadiliko ya ghafla ya tabia kama vile kutumia pombe au sigara kwa wingi, kutokujali muonekano, au kuwa mlevi wa mitandao ya kijamii kama njia ya kupunguza msongo wa mawazo.

6) Kujitenga Na Watu Wengine. 

Watu wenye msongo wa mawazo wanaweza kujikuta wakiepuka mikusanyiko ya kijamii au hata watu wa karibu kwa sababu ya kutokuwa na Ari (mood) ya kushirikiana au hisia ya kuwa mzigo kwa wengine.

Kujitenga Na Watu Wengine

7) Kutokuwa Makini Na Kusahau Sana.

Msongo huathiri uwezo wa ubongo kushughulikia taarifa. Mtu mwenye msongo wa mawazo hukosa umakini, hushindwa kukumbuka mambo muhimu, na huchanganyikiwa kirahisi.

amnesia

8) Kupungua Kwa Hamu Ya Kufanya Tendo La Ndoa.

Msongo wa mawazo huathiri homoni zinazohusiana na hamu ya tendo la ndoa. Mwanamke au mwanaume mwenye msongo wa mawazo anaweza kupoteza kabisa hamu ya kushiriki tendo hilo.

low libido

9) Kubadilika Kwa Hamu Ya Kula.

Watu wanaokumbwa na msongo wa mawazo mara nyingi hupata mabadiliko ya hamu ya kula chakula. Wengine wanaweza kupoteza kabisa hamu ya kula, wakati wengine wanakula kupita kiasi kama njia ya kupunguza mawazo.

10) Maumivu Ya Mwili Bila Sababu Ya Kiafya Inayoeleweka.

Mara nyingi, msongo wa mawazo unajidhihirisha kupitia maumivu ya kimwili kama vile maumivu ya kichwa, tumbo, au mgongo bila sababu ya kiafya inayoeleweka.

body ache

Athari Za Msongo Wa Mawazo Kwa Mwanamke:

Athari za msongo wa mawazo kwa mwanamke ni pamoja na:

1) Mabadiliko Ya Homoni.

Msongo wa mawazo husababisha mwili kutoa homoni za stress kama vile cortisol, ambazo zinaweza kuvuruga mzunguko wa homoni nyingine kama estrojeni na projesteroni, na kusababisha:

  • Mzunguko wa hedhi kuwa usio wa kawaida
  • Maumivu wakati wa hedhi (dysmenorrhea)
  • Kukosa hedhi kabisa (hypothalamic amenorrhea)
  • Kupungua kwa hamu ya tendo la ndoa (low libido)

2) Kuathiri Malezi Na Majukumu Ya Kifamilia.

Wanawake wengi ni walezi wa familia. Msongo wa mawazo huweza kupunguza uwezo wao wa kulea, kuwajali watoto, au kushirikiana na mwenzi. Hii huweza kusababisha migogoro ya kifamilia au kudumaa kwa uhusiano wa kifamilia.

3) Upungufu Wa Ufanisi Kazini Au Shuleni.

Msongo wa mawazo hupunguza uwezo wa kufikiri kwa makini, kupanga kazi, au kufanya maamuzi. Mwanamke mwenye changamoto hiyo anaweza kushindwa kutimiza majukumu yake ya kazi, kushuka kitaaluma au kujisikia kama amelemewa na kila kitu.

4) Kuathiri Afya Ya Akili.

Msongo wa mawazo huathiri utulivu wa akili na kusababisha matatizo kama vile:

  • Wasiwasi sugu (anxiety)
  • Sonona (depression)
  • Kutojiamini au kujiona duni
  • Mawazo ya kukata tamaa au kujiumiza

5) Matatizo Ya Ngozi.

Msongo wa mawazo unaweza kusababisha au kuchochea matatizo ya ngozi kama vile chunusi (acne), ukavu wa ngozi. Ngozi huathirika kutokana na mabadiliko ya homoni na kuongezeka kwa mafuta kwenye ngozi.

6) Kushuka Kwa Kinga Ya Mwili.

Homoni inayotolewa na mwili kutokana na msongo wa mawazo (cortisol) inapozidi kwa muda mrefu, huathiri uwezo wa mwili kupambana na magonjwa. Mwanamke huwa katika hatari zaidi ya kupata maradhi kama mafua ya mara kwa mara, na magonjwa ya ngozi kama vile chunusi (stress acne).

HITIMISHO:

Dalili za msongo wa mawazo zikitokea kwa muda mrefu au kwa viwango vikubwa, zinaweza kuathiri afya ya akili na mwili wa mtu kwa kiwango kikubwa. 

Kwa msaada zaidi kuhusu utatuzi wa changamoto ya msongo wa mawazo ni muhimu kuchukua hatua mapema kwa kuzungumza na mtaalamu wa afya ya akili (psychiatrist).