Ini Ni Nini?
Ini ni kiungo muhimu sana ndani ya miili yetu, hufanya kazi zaidi ya 500 ; moja ya kazi ni kuchuja na kuondoa sumu kutoka kwenye damu.
Homa ya ini ni hali ya kuvimba kwa ini, ambalo ni moja ya viungo muhimu zaidi mwilini. Homa ya ini hujulikana kwa kitaalamu kama Hepatitis.
Homa ya ini ni janga linaloua kimya kimya kulingana na takwimu za vifo vya dunia inakadiriwa kirusi cha homa ya ini aina ya B pekee huua watu 600,000 hivi kila mwaka.
Kwa wastani zaidi ya watu bilioni mbili, yaani, asilimia 33 hivi ya watu wote ulimwenguni, wameambukizwa virusi vya HBV (Hepatitis B Virus), na wengi wao hupona baada ya miezi michache. Watu milioni 350 hivi huendelea kuwa na virusi hivyo mwilini, wengi huishi bila dalili na kuendelea kuambukiza watu wengine.
Leo katika mada yetu ya blogu hii tutazungumzia sababu kadhaa zinazochnagia mtu kupata homa ya ini. Ungana nami katika kuchambua sababu hizi.
1) Maambukizi Ya Virusi.
Virusi vya hepatitis ndiyo sababu kuu ya homa ya ini na vimegawanyika katika aina tano ambazo ni pamoja na:
a) Hepatitis A Virus (HAV).
Huambukizwa kupitia chakula au maji yaliyochafuliwa na kinyesi cha mtu aliyeambukizwa. Ni ya muda mfupi na kawaida haikusababishi uharibifu wa kudumu wa ini.
b) Hepatitis B Virus (HBV).
Huambukizwa kupitia damu, majimaji ya mwili (mfano, majimaji ya uke, manii, au mate), au kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa kuzaliwa.
Inaweza kuwa sugu na kusababisha kansa ya ini (hepatocellular carcinoma) au makovu kwenye ini (liver cirrhosis).
c) Hepatitis C Virus (HCV).
Huambukizwa hasa kupitia damu, mfano, kwa kushirikiana sindano.
Mara nyingi huwa sugu na husababisha uharibifu mkubwa wa ini.
d) Hepatitis D Virus (HDV).
Hutokea tu kwa watu waliokwisha kuambukizwa na Hepatitis B, na huongeza ukali wa maambukizi.
e) Hepatitis E Virus (HEV).
Huenea kupitia maji au chakula kilichochafuliwa (contaminated water/food), hasa katika maeneo yenye usafi duni.
2) Matumizi Ya Pombe Kwa Muda Mrefu.
Matumizi ya pombe kwa muda mrefu husababisha uharibifu wa seli za ini, na kusababisha homa ya ini ya pombe (alcoholic hepatitis).
Hii inaweza kuendelea na kuwa ugonjwa sugu wa ini kama vile liver cirrhosis.
3) Matumizi Ya Dawa Na Kemikali.
Dawa za kupunguza maumivu (mfano, paracetamol) zinazotumika kupita kiasi zinaweza kuharibu ini.
Matumizi ya dawa za kulevya au kuathiriwa na kemikali zenye sumu kunaweza kusababisha uvimbe wa ini.
4) Magonjwa Ya Kinga (Autoimmune Hepatitis).
Hii hutokea pale ambapo mfumo wa kinga wa mwili hushambulia seli za ini kimakosa (ikiona seli za ini kama tishio), na kusababisha kuvimba kwa ini.
5) Magonjwa Ya Kurithi (Genetic Disorders).
a) Wilson’s Disease.
Hali ambapo shaba inajilimbikiza mwilini (extra copper), na ini linakosa uwezo wa kuondoa shaba hii, na kusababisha homa ya ini.
b) Hemochromatosis.
Hii ni hali ambapo chuma kinajilimbikiza mwilini (iron overload), husababisha madhara kwa ini na viungo vingine.
6) Maambukizi Ya Bakteria Au Vimelea.
Bakteria kama Leptospira na vimelea kama Schistosoma vinaweza kusababisha homa ya ini, ingawa hii ni nadra.
Maambukizi haya hutokea hasa katika maeneo yenye mazingira ya usafi duni (poor sanitation).
Jinsi Ya Kujikinga Na Homa Ya Ini:
Hatua za kujikinga na homa ya ini ni pamoja na kuzingatia mambo yafuatayo:
- Chanjo dhidi ya hepatitis A na B ni njia nzuri ya kujikinga.
- Kuepuka matumizi ya pombe kupita kiasi.
- Kuepuka kutumia dawa zisizohitajika na kuhakikisha matumizi sahihi ya dawa.
- Kula vyakula safi na kuepuka chakula kilichochafuliwa na aflatoxins.
- Kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara ili kugundua maambukizi mapema.
HITIMISHO:
Ikiwa una dalili za homa ya ini, kama vile kichefuchefu, uchovu, maumivu ya tumbo, au macho na ngozi kuwa ya njano (jaundice), ni muhimu kutafuta msaada wa matibabu haraka.
Leave a Reply