Shingo Ya Kizazi.

Shingo ya kizazi, au cervix kwa Kiingereza, ni sehemu ya chini ya mfuko wa uzazi (uterus) ambayo inaunganisha mfuko wa uzazi na uke (vagina).

Shingo Ya Kizazi

 

Sehemu hii ina majukumu muhimu sana katika mfumo wa uzazi wa mwanamke ikiwa ni pamoja na:

1) Kupitisha Mbegu Za Kiume.

Wakati wa kujamiina shingo ya kizazi inaruhusu mbegu za kiume kupita kutoka ukeni (vagina) kuelekea mji wa uzazi (uterus), ambapo zinaweza kuungana na yai lililopevushwa (ovum). Ute unaozalishwa na shingo ya kizazi (cervical mucus) huzisaidia mbegu za kiume kusafiri kwa urahisi kupitia mji wa uzazi ili kuweza kuungana na yai lililopevushwa.

cervical mucus

2) Kupitisha Damu Ya Hedhi.

Wakati wa kipindi cha hedhi, shingo ya kizazi inaruhusu damu ya hedhi kutoka mji wa uzazi kuingia ukeni.

hedhi

3) Kuzuia Maambukizi.

Kuta za shingo ya kizazi zimebeba tezi (endocervical glands) ambazo huzalisha na hutoa kamasi (mucus) inayosaidia kuzuia bakteria na vijidudu vingine visipande juu hadi kwenye mji wa uzazi na viungo vingine vya uzazi.

4) Kulinda Mimba.

Wakati wa ujauzito, shingo ya kizazi inabaki imefungwa ili kulinda kijusi (fetus) dhidi ya maambukizi na kuimarisha mimba mpaka wakati wa kujifungua.

mimba

5) Kufunguka Wakati Wa Kujifungua.

Katika hatua za mwisho za ujauzito, shingo ya kizazi huanza kufunguka ili kumruhusu mtoto kupita wakati wa kujifungua.

Wakati Wa Kujifungua

Mambo Muhimu Ya Kuzingatia:

Ili kulinda shingo ya kizazi na kuhakikisha inabaki salama mwanamke unapaswa kuzingatia mambo yafuatayo:

1) Uchunguzi Wa Mara Kwa Mara.

Ni muhimu kwa wanawake kufanya vipimo vya mara kwa mara ili kugundua mabadiliko yoyote katika seli za shingo ya kizazi mapema. Kipimo cha Pap smear ni moja ya vipimo muhimu ambavyo hutumika kutambua mabadiliko haya.

2) Chanjo Ya HPV.

Kupata chanjo dhidi ya virusi vya HPV (HPV Vaccine) kunaweza kusaidia kupunguza hatari ya saratani ya shingo ya kizazi, kwani HPV ni moja ya visababishi vikuu vya saratani hii

3) Kujikinga Na Maambukizi.

Kutumia kondomu na kuepuka kuwa na wapenzi wengi (multiple sexual partners) kunaweza kusaidia kupunguza hatari za maambukizi yanayoweza kusababisha saratani.

HITIMISHO:

Kujifunza zaidi kuhusu saratani ya shingo ya kizazi na madhara yake bonyeza hapa: Haya Ndiyo Mambo 6 Muhimu Usiyo yajua Kuhusu Saratani ya shingo ya kizazi.