Kifafa cha mimba ni ugonjwa unaowapata wanawake wajawazito, hasa wenye mimba za kwanza (Primigravida).
Kwa walio wengi, ugonjwa huu hutokana na kupanda kwa msukumo wa damu (High blood pressure). Ugonjwa huu utokeapo, mgonjwa hupatwa na degedege (convulsion).
Ugonjwa huu unajulikana kwa kitaalamu kama Pre eclampsia.
Kifafa cha uzazi au wengine wanakiita kifafa cha mimba ni miongoni mwa matatizo yanayosababisha vifo vya wajawazito nchini.
Kifafa cha mimba kinaweza kutokea wakati wa ujauzito, wakati wa kujifungua au baada ya kujifungua.
Soma pia hii makala: Yajue Mambo 5 Muhimu Kuhusu Shinikizo La Juu La Damu.
Visababishi Vya Kifafa Cha Mimba:
Sababu la tatizo hili bado wataalamu wa tiba duniani hawajagundua, Ila kuna baadhi sababu zinahisiwa kusababisha tatizo hili ambazo ni pamoja na:
1) Mimba ya kwanza, hususani katika umri mdogo chini ya miaka 20 na mimba za uzeeni baada ya miaka 35.
2) Ugonjwa wa shinikizo la damu au kisukari kabla ya kubeba mimba.
3) Wanawake wenye wenza wengi (multiple sexual partners) wapo katika hatari ya kupata kifafa cha mimba.
4) Wanawake ambao wazazi, au ndugu zao wa karibu waliwahi kupatwa na matatizo ya kifafa katika mimba zao.
5) Wanawake waliopatwa na kifafa cha mimba zao za kwanza wapo katika hatari ya kupata kifafa hicho tena katika mimba zinazofuata.
6) Wanawake wenye mimba ya mapacha wapo katika hatari zaidi ya kupata kifafa cha mimba kuliko mimba ya mtoto mmoja.
7) Ugonjwa wa figo kwa mama mjamzito.
Dalili Za Kifafa Cha Mimba:
Kwa sababu shinikizo kubwa la damu kwa mjamzito ndio chanzo kikubwa cha kifafa cha mimba, mjamzito anaweza kuwa na dalili za changamoto zote mbili, yaani akawa na dalili za kuongezeka zaidi kwa presha ya damu (high blood pressure), kuvimba miguu na mikono. Dalili kuu za kifafa cha mimba ni pamoja kupoteza fahamu, degedege (convulsion) inayo ambatana na uwepo wa protini kwenye mkojo (proteinuria).
Dalili zingine ni kama ifuatavyo:
1) kuongezeka uzito kupita kiasi.
2) kichefuchefu na kutapika kupita kiasi.
3) Kupata shida wakati wa kukojoa (Dysuria).
4) Maumivu makali ya kichwa (severe headache).
5) kuvimba uso na vidole.
6) Kuona giza au kutoona vizuri (blurred vision).
Kumbuka: Mara nyingi kifafa cha mimba hutokea kwa mimba yenye umri wa wiki 20 na zaidi, na inaweza itokee wakati wa ujauzito au mara tu baada ya kujifungua.
Utambuzi Wa Kifafa Cha Mimba:
Endapo una historia ya kuugua presha, dakari anaweza kupendekeza vipimo kujua ukubwa wa tatizo lako. Kama hujawahi kuugua presha ataagiza vipimo pia kujua kwanini unapata kifafa. Vipimo hivyo ni pamoja na:
1) Kipimo Cha Damu.
Vipimo hivi ni kwa ajili ya kujua kiwango cha seli nyekundu za damu zilizopo na kipimo cha kugundua namna gani damu yako ina uwezo wa kuganda. Kipimo cha damu pia kitatumika kujua hali ya figo na ini lako kama vinafanya kazi vizuri.
2) Creatinine Test.
Creatinine ni taka mwili inayozalishwa na misuli yako. Kazi ya figo ni kuchuja creatinine kwenye damu, kama chujio la figo limeathirika manake creatinine itabaki kwenye damu. Kiwango kikubwa cha creatinine kwenye damu kinaweza kuashiria una preeclampsia.
3) Kipimo Cha Mkojo.
Daktari anaweza pia kupendekeza kipimo cha mkojo kuona kiwango cha protini kilichopo kwenye mkojo.
Kama una viashiria vya kupata kifafa cha mimba, daktari atafuatilia hali yako kwa ukaribu ili kuhakikisha kuwa dalili zako hazizidi na kupelekea shida hii.
Kujifungua ndio tiba thabiti kwa mtu mwenye dalili kali zinazo ashiria kuwa atapata degedege, hili hufanyika ili kuzuia kupata kifafa cha mimba. Mwanamke akijifungua tatizo hili linakwisha. Kuendelea kubeba ujauzito ukiwa na tatizo hili inaweza kuwa hatari kwa mama na mtoto.
Daktari anaweza kufuatilia hali yako kwa ukaribu wakati wa dalili kali, ili kuruhusu mimba yako kukua mpaka kufikia wiki 32 – 34 au kama dalili sio kali sana mpaka wiki 36 – 37. Kusubiri hivi humpatia muda mtoto aliye tumboni kukua kabla hajazaliwa na kupunguza matatizo yanayotokana na kuzaa mtoto njiti.
Unaweza kupewa madawa ili kudhibiti dege dege. Magnesium sulfate ni dawa salama kwa mama na mtoto.
Daktari anaweza kukupatia dawa ya kupunguza shinikizo la damu, lakini unaweza kutakiwa kuzaa kama shinikizo lako la damu halitashuka hata baada ya kupewa dawa.
Matibabu Ya Kifafa Cha Mimba:
Kifafa cha mimba ni ugonjwa wa dharura (medical emergency condition), hivyo madaktari na manesi watakusanyika kwa pamoja kumhudumia mgonjwa.
Baada ya degedege kuisha na kupatiwa dawa za presha, mama ataanzishiwa dawa za uchungu (oxytocics) hata kama mimba ilikuwa bado hajfikia umri wa kujifungua, kwa kuwa kuna ulazima wa kuokoa maisha ya mama kwanza (mother’s life first) mama anaweza pia kujifungua kwa kufanyiwa upasuaji kama patakua na uhitaji wa kufanya hivyo.
Madhara Ya Kifafa Cha Mimba:
Yafuatayo ni madhara yanayoweza kutokea endapo mama mjamzito mwenye kifafa cha mimba atashindwa kupata matibabu haraka ambayo ni pamoja na:
1) Wakati wa kifafa cha mimba kuna uwezekano mkubwa zaidi wa kondo la nyuma (placenta) kubanduka na kutoka kwenye mfuko wa uzazi, hali hii kwa kitalaamu hujulikana kama placental abruption ambapo mwanamke mwenye tatizo hili hutokwa damu nyingi zaidi na hata kupelekea kifo.
2) Uwezekano wa mtoto kuzaliwa akiwa njiti na matatizo yanayoambatana na hali hiyo huongezeka.
3) Mgonjwa anaweza kupata tatizo la damu kushindwa kuganda linaloitwa disseminated intravascular coagulation (DIC). Tatizo hili linaweza kusababisha mama kuvuja damu nyingi na hata kufa.
Jinsi Ya Kuepuka Kifafa Cha Mimba:
Mama mjamzito anashauriwa kufanya mambo yafuatayo ili kuepuka kupata kifafa cha mimba ambayo ni pamoja na:
1) Ni muhimu kwa wanawake wote wajawazito kupata huduma za matibabu mapema na kwa mwendelezo. Hii itasaidia utambuzi wa mapema na matibabu kwa viashiria vya kifafa cha mimba kabla tatizo halijawa kubwa zaidi.
2) Kutibu viashiria (preeclampsia) kunaweza kuzuia tatizo hili.
HITIMISHO:
Kama ilivyoandikwa hapo juu, kifafa cha mimba ni ugonjwa wa dharura (medical emergency condition), hivyo basi mama mjamzito mwenye tatizo hili analazimika kuwaishwa haraka hospitali ili kunusuru afya yake na mtoto aliye tumboni.
Lakini pia, kwa uhitaji wa updates, vitabu (e-books) bure kuhusu afya jisajili (subscribe) kupitia email yangu kwa kubonyeza hii link: https://isayafebu.beehiiv.com/subscribe
Leave a Reply